010-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Sutrah Na Yanayokata (Yanayotengua) Swalah

 

 

 

 

SUTRAH[1] NA KUWAJIBIKA KWAKE

 

"Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisimama karibu na sutrah, ili iweko (umbali wa) dhiraa tatu baina yake na ukuta”[2] na "baina ya sehemu ya sujuud na ukuta (kulikuweko) nafasi ya kuweza kupita kondoo”[3].

 

Alikuwa akisema,

((Msiswali isipokuwa mbele ya Sutrah, na msimuachie mtu kupita mbele yenu, lakini kama mtu akiendelea (kujaribu kupita) basi mzuwieni kwani yuko pamoja na rafiki)) (yaani Shaytwaan).[4]

 

Alikuwa akisema,

((Mmoja wenu akiswali mbele ya Sutrah, basi awe karibu yake ili Shaytwaan asiweze kuivunja Swalah yake)).[5]

 

 

Mara nyingine "Alikuwa anaswali mbele ya nguzo ya msikiti.”[6]

 

Alipokuwa anaswali (kwenye sehemu ya wazi ambako kulikuwa hakuna kitu cha kutumia kiwe Sutrah) alikuwa akiuchomeka mkuki ardhini mbele yake kisha akiswali kuuelekea na watu wakiwa nyuma yake.[7] Mara nyingine "alikuwa akiweka kipando chake (mnyama) kisha akiswali kukielekea kipando chake.[8] Lakini hii sio sawa na Swalah katika sehemu ya mapumziko ya ngamia[9] ambayo "ameikataza”[10] na mara nyingine "alikuwa akichukua tandiko lake (la ngamia) akiliweka kwa urefu kisha akiswali kuelekea nchani mwake.”[11]

 

Na alikuwa akisema,

((Mmoja wenu akiweka mbele yake kitu kama fimbo nchani (mwishoni) mwa tandiko la mnyama, basi aswali na asijali mtu yeyote atakayepita mbele yake)).[12]

 

Mara moja "Aliswali akiuelekea mti”[13] na wakati mwengine "Alikuwa akiswali mbele ya kitanda ambacho Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) alikuwa amelala (akiwa amejifunika shuka).”[14]

 

Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa haachii kitu chochote kupita baina ya Sutrah yake, kwa hiyo mara moja "alikuwa anaswali na kondoo alipokuja na kukimbia mbele yake alimkimbiza mpaka akalibonyeza tumbo lake katika ukuta (kisha akapita nyuma yake).”[15]

 

 

Vile vile mara moja "wakati anaswali Swalah ya fardhi, alikunja ngumi yake. Na alipomaliza (kuswali) watu walimwambia, "Ewe Mjumbe wa Allaah, kuna jambo limetokea wakati wa Swalah?" Akasema, ((Hapana isipokuwa Shaytwaan alitaka kupita mbele yangu, nikamkaba mpaka nikahisi ubaridi wa ulimi wake katika mkono wangu. Naapa kwa Allaah! Ingelikuwa sio ndugu yangu Sulaymaan kunitangulia[16]. Ningelimfunga (Shaytwaan) katika nguzo moja ya msikiti ili watoto wa Madiynah waweze kutembea mbele yake. (kwa hiyo yeyote atakayeweza kuzuwia kitu kumuingilia baina yake na Qiblah afanye hivyo).”[17]

 

Pia alikuwa akisema,

 

((Mmoja wenu anaposwali mbele ya kitu kama Sutrah baina yake na watu na mtu akitaka kupita mbele yake, basi amsukume kwa shingo yake)) (na amfukuze kadiri anavyoweza) (katika riwaya nyingine, ((amzuie mara mbili na akikataa (akishikilia kutaka kupita mbele) basi agombane naye kwani hakika huyo ni Shaytwaan)).[18]

 

Vile vile alikuwa akisema,

((Ikiwa mtu aliyepita mbele ya mtu mwenye kuswali amejua (kuwa ni dhambi) juu yake (kufanya hivyo), basi ingelikuwa ni bora kwake kusubiri arubaini kuliko kupita mbele)). Na nyongeza katika riwaya nyingine yasema, (Abu An-Nadr kasema, "Sikumbuki khaswa kama alisema ni siku arubaini, au miezi au miaka").[19]

 

 

 

YANAYOKATA (YANAYOVUNJA) SWALAH

 

Alikuwa akisema,

((Swalah ya mtu inavunjika (inakuwa baatwil) kunapokuwa hakuna kitu kama ncha ya tandiko (la mnyama) mbele yake (vitu vitatu) mwanamke (baleghe)[20] punda au mbwa mweusi)) Abu Dharr akasema, "Nilisema, Ewe Mjumbe wa Allaah, kwa nini mbwa mweusi na sio mwekundu?" Akasema, ((Mbwa mweusi ni Shaytwaan)).[21]

 

 [1] Sutrah – "Kinga ya kuzuia" katika Swalah, inakusudia kitu cha kuwekwa mbele ya sehemu ya kusujudu kukinga ili asipite mtu au chochote mbele yake kama ilivyoelezewa katika somo hili.

[2] Al-Bukhaariy na Ahmad.

[3] Al-Bukhaariy na Ahmad.

[4] Ibn Khuzaymah katika Swahiyh yake (1/93/1) na Isnaad iliyothibitika.

[5] Abu Daawuud, Bazzaar (ukurasa 54 Zawaaid) na Al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh na Adh-Dhahaabiy na An-Nawawiy wameikubali.

[6] Al-Bukhaariy.  Sutrah ni lazima kuweko kwa Imaam au mtu anayeswali peke yake hata katika msikiti mkubwa.  Ibn Haani amesema katika Masaa'il yake kutoka Imaam Ahmad (1/66) "Abu 'Abdillaah (Imaam Ahmad Ibn Hanbal) aliniona siku moja wakati naswali bila ya Sutrah mbele yangu na nilikuwa katika (Swalah ya) Jama'ah (kubwa) msikitini, kwa hiyo akaniambia, "Weka kitu kama Sutrah".  Nikamchukua mtu kama Sutrah. Hii inaonyesha kwamba Imaam Ahmad hakutofautisha baina ya msikiti mkubwa au mdogo katika mas-ala ya Sutrah. Na hii hakika ni sahihi, lakini hili ni jambo ambali limedharauliwa na watu wengi pamoja na ma-Imaam wa misikiti katika kila nchi nliyotembea pamoja  na nchi za Arabuni ambazo nimeweza kutembea katika mwezi wa Rajab wa mwaka huu (1410).  Kwa hiyo ma-Ulamaa waambie watu na kuwanasihi jambo hili, na kuwafahamisha sheria yake na kwamba pia inahitajika kuweko katika misikiti miwili mitukufu.

[7] Al-Bukhaariy, Muslim na Ibn Maajah.

[8] Al-Bukhaariy na Ahmad.

[9] Yaani ni sehemu yao ya kupiga magoti.

[10] Al-Bukhaariy na Ahmad.

[11] Muslim, Ibn Khuzaymah (92/2) na Ahmad.

[12] Muslim na Abu Daawuud.

[13] An-Nasaaiy na Ahmad kwa Isnaad Swahiyh.

[14] Al-Bukhaariy, Muslim na Abu Ya'laa (3/1107).

[15] Ibn Khuzaymah katika Swahihy yake (1/95/1) At-Twabaraaniy (3/140/3) na Al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh na Adh-Dhahabiy kaikubali.

[16] Inakusudiwa Du'aa ifuatayo ya Nabii Sulaymaan (عليه السلام) ambayo alijibiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kama ilivyo katika Qur-aan.  ((Akasema: Mola wangu Mlezi! Nisamehe na unipe ufalme usio mwelekea yeyote baada yangu. Hakika Wewe ndiye Mpaji)) ((Basi Tukaufanya upepo umtumikie, ukenda kwa amri yake, popote alipo taka kufika)) ((Na tukayafanya mashaytwaan yamtumikie, wote wajenzi na wapiga mbizi))   ((Na wengine wafungwao kwa minyororo)) [Swaad, 38: 35-38].

[17] Ahmad, Daaraqutniy na At-Twabariy kwa Isnaad ya Swahiyh na iliyo na maana kama hii ni Hadiyth inayopatikana katika Al-Bukhaariy na Muslim na wengineo kutoka kwa mapokezi ya Maswahaba mbali mbali.  Na mojawapo ya Hadiyth ambayo kundi la Maqadiyani hawaiamini kwani hawaamini (ulimwengu wa) majini ambao wametajwa katika Qur-aan na Sunnah.  Desturi yao ni kukanusha maandishi yaliyo mashuhuri sana. Kama kutoka kwenye Qur-aan wanabadilisha maana yake mfano, maneno ya Subhaana Wa Ta’ala ((Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza)) [72:1] wanasema kwamba ina maana "kikundi cha binaadamu" na kulifanya neno la 'majini' kuwa inakaribia na maana ya 'binaadamu'. Kwa hiyo wanacheza na lugha na dini.  Na kama kutoka katika Sunnah basi kama inawezeka kwao kubadilisha kwa tafsiyr ya uongo wanafanya hivyo, au sivyo wanaona ni wepesi  kukiri kuwa ni uongo hata kama Maimaam wa Hadiyth wote  na Ummah mzima kabla yao wamekubaliana na usahihi wake, (tunawaambia kuwa hilo wanalilikataa hapo) kuwa hapana, hiyo ni mutawaatir (imekuja kwa mapokei mengi haina shaka yoyote).  Allaah Awahidi.

 

[18] Al-Bukhaariy na Muslim na riwaya zaidi ni kutoka kwa Ibn Khuzaymah (1/94/1).

[19] Al-Bukhaariy na Muslim.

[20] Ina maana baleghe, na maana ya 'inavunjika' ni kuwa 'haifai tena' (baatwil).  Ama kuhusu Hadiyth "Hakuna kinachovunja Swalah" hiyo ni Hadiyth dhaifu na nimeionyesha katika Tamaam Al-Minnah (Ukurasa 306).

[21] Muslim, Abu Daawuud na Ibn Khuzaymah (1/95/2).

Share