Nini Hukmu Ya Kupiga Kura Kuchagua Wabunge Wakawakilisha Utungaji Sheria Zisizo za Allaah?

    

SWALI LA KWANZA:
Asalmu Alaykum.Mfumo wa Demokrasia umejengwa juu ya kumpinga Mungu,kutokana na akidah yake ya kutenganisha dini na maisha.Jukumu la WABUNGE/WAWAKILISHI ni kutunga sheria.je kwa muisamu kushiriki au kuwakilishwa katika utungaji sheria ni halali?
 

 

SWALI LA PILI:

 

Assalamu Aleikum
Kwa vile nimesoma katika masuali mchanganyiko kwamba unaweza kuchagua mbunge au mgombea kura yoyote kwa kuangalia unafuu utakaopatikana katika Uislamu pindi akichaguliwa, suala ambalo ningependa kuuliza jee wewe mpigaji kura utakuwa katika hali gani kumchagua mbunge ambaye kazi yake ni kutunga sheria za viumbe hali ya kuwa Allaah amemuhukumu yule ambaye anahukumu pasina kutumia kitabu chake kuwa ni kafiri, dhalim au fasik kwa hiyo haitokuwa umeshiriki katika hayo?

 


 

 

 

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Katika kujibu maswali haya mawili muhimu na ambayo yamekuwa ni gumzo miongoni mwa Waislamu na yamezua ikhtilafu miongoni mwa Waislamu baina ya mwenye kupinga kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi na baina ya wenye kujuzisha kushiriki katika mchakato huo wa Demokrasia.

 

Katika kujadili na kuangalia hoja za pande zote mbili ni muhimu kwanza tukaelewa kuwa, mazingira ya awali ya kuibuka mjadala huu yametokea katika nchi zenye Waislamu wengi na ambazo Katiba zake zinasema wazi kuwa Dini ya Dola ni Uislamu na  sheria za Uislamu ni moja miongoni wa vyanzo vya sheria zinazotumiwa na nchi hizo, nimeona vema tulielewe hilo mwanzo kwani mara nyingi huwa tunakosea tunapohamisha matatizo toka eneo lenye mazingira tofauti na kuyaleta matatizo hayo katika maeneo yetu, na hatimae kuyatafutia ufumbuzi matatizo hayo kwa hoja na vigezo visivyo fanana na mazingira yetu.

 

Hata hivyo, tutajaribu kuangalia hoja zilizotumiwa na pande zote mbili zenye kusigana kuhusiana na uhalali au uharamu wa kushiriki katika mchakato wa uchaguzi wa kidemokrasia na kuingia kwenye mabunge ambayo kazi yake kuu ni kutunga sheria za kuhalalisha na kuharamisha.

 

 

 

HOJA ZA WANAOPINGA:

 

Wanaopinga kushiriki katika mchakato wa kuchagua au kugombea nafasi katika mabunge wanatoa hoja zifuatazo:

 

 

1.     Anasema Allaah katika Qur-aan:

 

“Naye Amekwisha kuteremshieni katika Kitabu hiki ya kwamba mnaposikia Aayah za Allaah zinakataliwa na kufanyiwa istihzai, basi msikae pamoja nao hata waingie katika mazungumzo mengine, (mtakapokaa) mtakuwa kama wao. Hakika Allaah Atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika jahannamu.” [4: 14]

 

Ushahidi uliopo katika Aayah ni kuwa katika haya mabunge watu hukaa kutunga sheria nyingine na kuzifanyia istihzai sheria za Allaah na mara nyingine hata kuzikashifu, hivyo kwa Muislamu kushiriki katika kikao cha aina hii ni haraamu mpaka ahakikishe kuwa wameingia katika mazungumzo mengine, na kama atashiriki basi nae atakuwa kama wao, miongoni mwa wanafiki na makafiri.

 

 

2.     Anasema Allaah:

 

“Na wewe (Muislamu kama kweli Muislamu sio mnafiki) unapowaona wale wanaozungumza (kuzikadhibisha) Aayah zetu, basi jitenge nao mpaka wazungumze maneno mengine. Na kama shetani akikusahaulisha (ukakaa nao) na wamo katika mazungumzo haya) basi baada ya kutanabahi usikae pamoja nao (hawa) watu madhalimu.” [6: 68]

 

Aidha ushahidi uliopo katika Aayah hii unatia nguvu ushahidi wa mwanzo kuhusu kukaa mbali na vikao na watu wanaozifanyia istihzai sheria za Allaah.

 

 

3.     Anasema Allaah katika Aayah nyingine:

 

Basi (ewe Mtume) Endelea na uongofu kama ulivyoamrishwa (wewe) na wanaoelekea kwa (Allaah) pamoja nawe, wala msiruke mipaka. Hakika Yeye Anayaona yote mnayoyatenda. Wala msiwategemee (mkawa pamoja nao) wale wanaodhulumu (nafsi zao kwa maasi) usije ukakuguseni moto. Na hamtakuwa na mlinzi mbele ya Allaah; kisha nyinyi hamtasaidiwa (na yeyote huko) [11: 112-113]

 

Ushahidi uliopo katika Aayah hii ni makaripio makali ya kutowategemea na kuwaegemea wale wanopituka mipaka ya Allaah, au kufanya nao kazi pamoja hali ya kuwa wanazidhulumu nafsi zao, na kazi ya wabunge au wawakilishi katika nchi zetu ni kufuata siasa na sera za vyama vyao katika kupanga na kutunga sheria, jambo ambalo kwa Muislamu kwa mujibu wa Aayah limekemewa vikali.

 

 

4.     Anasema Allaah:

 

“…Katika hivyo mna madhara makubwa na (baadhi ya) manufaa kwa (baadhi ya watu) Lakini madhara yake ni makubwa kuliko manufaa yake…” [2: 219] 

ushahidi unaopatikana katika Aayah hii, ni madai ya kuwa kwa kushiriki katika mabunge na mabaraza ya wawakilishi kuna faida inapatikana, kwani Waislamu wanapokuwa humo wanaweza kuzuia baadhi ya shari kwa kuzuia upitishaji wa sheria zenye madhara na Uislamu, au kushawishi kupitisha sheria zenye manufaa na binadamu, kwa mujibu wa Aayah hii, hata tukikubali kimjadala kuwa kuna manufaa kushiriki katika mabunge, lakini ni dhahiri kuwa madhara yake ni makubwa kuliko manufaa yake, na ukweli ni kuwa wabunge Waislamu huingia mabungeni kwa tiketi za vyama vyao na kutetea ilani za uchaguzi za vyama vyao na wala hawaingii kutetea Uislamu.

 

5.     Baadhi ya Waislamu wanadhania kuwa kwa kuingia katika mabunge itafika siku moja wabunge Waislamu watakuwa wengi na watafanikiwa kupitisha matumizi ya sharia za Kiislamu katika nchi yao, na hizi ni ndoto kusema kweli, kwani mfumo wa kisiasa katika nchi zetu, hauruhusu hilo kutokea, na wabunge au wawakilishi hutoa viapo vya kulinda sera za vyama vyao na hupitishwa na vyama hivyo kugombea kutokana na ukereketwa wa itikadi za chama na sio dini.

 

6.     Hoja nyingine ni kuwa Mtume hakuwahi kushiriki katika mabunge kama haya, pamoja na kuwa Ma-Quraysh walikuwa na jumba lao la uwakilishi liitwalo Daaru An-Nadwa, Mtume alikuwa ana uwezo wa kujiunga na Bunge hili na kuwaathiri Ma-Quraysh waukubali Uislamu, lakini hakufanya hivyo.

 

7.     Aidha kushiriki katika mabunge haya ni kutia nguvu serikali ya kikafiri iliyopo madarakani na kuipa uhalali.

 

8.     Hoja yao ya mwisho ni kuwa kutoshiriki katika uchaguzi na kutokubali kujiunga na mfumo huu unaopingana na Sheria za Allaah ndio msimamo sahihi.

 

 

Huo ndio msimamo wa wanaopinga kushiriki katika mchakato mzima wa kuchagua na kuchaguliwa katika mabunge na mabaraza ya wawakilishi na hizo ndizo dalili zao na hoja zao.

 

 

 

HOJA ZA WANAOJUZISHA:

 

Wanaojuzisha kushiriki katika mchakato wa kuchagua na kuchaguliwa na kushiriki katika mabunge na mabaraza ya wawakilkishi katika nchi tofauti za Kiislamu, hoja zao zinaegemea katika maslahi ya Uislamu yanayopatikana katika kushiriki, ukilinganisha na maovu yatakayopatikana kwa Waislamu kususia kushiriki katika vyombo hivi muhimu katika nchi, kwa hoja zifuatazo:

 

1.     Kwa kushiriki katika mabunge haya, Muislamu anaweza kupinga miswada ya sheria inayopingana na kutoa hoja kwa wabunge juu ya hukmu ya Uislamu kuhusiana na kadhia mbali mbali zinazotafutiwa ufumbuzi, na hii ni njia moja ya kufanya Da’awah kama tulivyoamriwa na Allaah:

 

“Waite watu katika njia ya Mola kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora…” [16: 125] 

Hoja yao hapa ni amri ya kulingania watu kwenye Uislamu kwa hekima na kujadiliana na wasiokuwa Waislamu kwa njia bora. Hivyo kushiriki katika mabunge haya kwa nia ya kufikisha ujumbe na kujadiliana kwa njia ya nzuri ni kufikisha ujumbe wa Allah. 

2.     Kutoa miswada ya sheria yenye lengo la kubadilisha kanuni zinazopingana na sheria za Kiislamu na kuwahamasisha wabunge kuzipitisha, na hii ndio kazi ya kuamrisha mema iliyotajwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth yake mashuhuri aliposema:

 

“Atakayeona jambo ovu miongoni mwenu, basi aubadilishe kwa mikono yake, kama atashindwa basi kwa ulimi wake, kama atashindwa basi kwa moyo wake, na huo ni udhaifu wa imani”.

 

Hivyo basi, ikiwa kwa ajili ya kuondoa uovu ni lazima kushiriki katika mchakato wa kuchagua na kuchaguliwa, basi jambo hilo litakuwa ni wajibu kwa Muislamu kushiriki. 

3.     Wabunge na Wawakilishi wa Nchi wanapewa heshima na nchi zao, na kuna sheria inayowalinda wasishitakiwe, basi ni vema Waislamu waitumie fursa hiyo katika kufanya Da’awah bungeni na nje ya bunge, na kutumia heshima hiyo wanayopewa na nchi katika kuutetea Uislamu na Waislamu. 

4.     Kwa kuwa moja ya kazi ya Mbunge ni kuikosoa serikali na watendaji wake, basi mbunge Muislamu anaweza kuwa mkali kwa serikali na kiongozi mwenye dhamana inapokiuka haki za Waislamu au kuwaonea, au kuwabagua, bali anaweza kuitaka serikali nzima kujiuzulu na kutumia ushawishi wake kufanikisha hilo. Kwa hoja hii ni muhimu kwa Waislamu kushiriki kwa wingi katika mabunge kwa kuchaguliwa na Waislamu ili wakatetee haki zao huko.

 

Hizo ndio hoja za pande mbili zinazosigana, na kama tulivyoona pande zote zina hoja zinazokubalika, na kujadilika,  lakini kama tulivyotangulia katika utangulizi wa majibu yetu hapo juu kuwa, mazingira ya nchi na nchi yanatofautiana, katika nchi ambazo zaidi ya asilimia 90 ya raia wake ni Waislamu, na Katiba ya nchi inatambua kuwa Uislamu ni moja miongoni mwa vyanzo muhimu vya sheria, na katiba yake ikaruhusu uundwaji wa vyama vyenye mielekeo ya Kiislamu, basi kushiriki katika  mchakato mzima wa uchaguzi kunaweza kuwa na faida kwa Uislamu na Waislamu, hata kama nchi hiyo kwa asilimia kubwa haitumii sheria za Kiislamu katika kuendesha mambo yake.

 

Lakini katika nchi ambazo zinajiita za kisekula (hazina dini) na Waislamu katika nchi hizo wako chini ya asilimia 60 na mfumo wake hauruhusu uundwaji wa vyama vyenye mielekeo ya kidini au wagombea binafsi, basi uwezekano wa kuingia bungeni kwa ajili ya Uislamu na Waislamu utakuwa mdogo sana, kwani mgombea atawajibika kufuata sera za chama chake kilichompa tiketi ya kuwa mbunge, na ndani ya bunge atatetea haki kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi wa chama husika. Na hata kama atawaambia Waislamu kuwa wampe kura zao ili akatetee haki zao bungeni, hatasema hivyo hadharani, na ukweli atakuwa anawahadaa ili watu wamchague lakini hatokuwa na uwezo wa kuwasaidia hata kama atataka, kwani mfumo utambana.

 

Hivyo basi kwa mtazamo wetu, ili kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kuwe ni halali katika nchi kama za kwetu za Afrika Mashariki, inabidi mambo yafuatayo yapatikane:

 

1.     Awepo kiongozi mmoja wa Waislamu katika nchi, anayekubalika na Waislamu kwa elimu yake, mapenzi yake ya dini, ucha Mungu wake, na Jihaad zake katika Da’awah.

 

2.     Kiongozi huyu atakuwa na mamlaka ya kuamrishwa na kutiiwa na Waislamu.

 

 

3.     Kiongozi huyu pamoja na shuuraa yake watakuwa na dhimma ya kuweka makubalianao na viongozi wa juu wanaogombea nafasi za uraisi na kuwapa matakwa ya Waislamu katika manifesto iliyoandaliwa na kuchukua ahadi kwao kuwa kama Waislamu watamchagua basi atatekeleza manifesto hiyo.

 

4.     Kiongozi huyu ndio atakaewapa idhini Waislamu washiriki au wasishiriki katika uchaguzi, na kama watashiriki basi wampe kura zao nani.

 

 

5.     Atafuatilia utekelezaji wa makubaliano kwa niaba ya Waislamu na serikali, na kutoa taarifa kwa umma juu ya utekelezaji wa makubaliano hayo.

 

Kama mazingira haya yatakuwepo, basi kushiriki katika kuchagua na kuchaguliwa kutakuwa na maana.

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

Share