Kuua Wadudu Wanaoleta Uchafu Na Madhara Inafaa?

 

Kuua Wadudu Wanaoleta Uchafu Na Madhara Inafaa?

 www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam Alaikum wa Rahmatullah wa Barakatuh,

Naomba Fatwa juu ya haya masuala ya kuua wadudu kama sisimizi, mende, siafu, nzi, na pia wanyama wadogo kama vile panya, mjusi na wengineo. Utakuta hao ni wachafu na watia kero sana. Je sheria inaruhusu kuwaua  kwa kutumia INSECTICIDE ama sumu za kuwaua. Naomba ufafanuzi...shukran na Jazakumullah kheir...

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika hilo ni suala ambalo limezungumziwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zake tofauti kuwa inafaa kuwaua baadhi ya wanyama wenye kuleta madhara. Hivyo, kwa kutumia Qiyaas (kulinganisha) hawa wadudu wengine nao itakuwa inafaa kuwaua ili wasilete madhara katika jamii kwa njia moja au nyingine.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ameruhusu kuuliwa kwa nyoka na nge [Abu Daawuwd].

 

 

 Na amekwenda zaidi (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa idhini kuuliwa baadhi ya wanyama hata Muislamu akiwa katika Ihraam na katika eneo tukufu la Msikiti wa Haram sehemu ambayo hairuhusiwi kuuliwa kwa wanyama. Amesema (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam): “Mnaweza kuwaua nyoka, nge, panya, mbwa mwenye kuuma, kipanga na wanyama pori wenye kuwavamia wanadamu” [(Abu Daawuud].

 

 

Na katika riwaayah ya al-Bukhaariy: “Mnaweza kuwaaua panya, nge, kipanga, kurabu na mbwa mwenye kichaa mkiwa katika Ihraam”. Na ikamjulimsha nyoka katika riwaayah nyingine.

 

Kwa hiyo, wanyama au wadudu wenye kuleta madhara wanaweza kuuliwa.

 

Pia ‘Ulamaa wamefutu swali kama hilo. Bonyeza kiungo kifuatacho:

 

Imaam Ibn Baaz - Kuua Vidudu Vyenye Madhara Nyumbani Kama: Mende, Mbu, Nzi...

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share