Mu'aawiyah Bin Abi Sufyaan (رضي الله عنه)

Mu'awiyah Bin Abiy Sufyaan (Radhwiya Allaahu 'Anhu)

 

Imekusanywa Na: Muhammad Faraj Salim As-Sa’iy (Rahimahu Allaah)

 

 

Nasaba yake

 

Jina lake ni Mu’awiyah bin Abu Sufyaan 'Sakhar' bin Harb bin Umayyah bin Abdi Shams bin Abdi Manaaf bin Qusay bin Kilaab. Na mama yake ni Hind bint ‘Utbah bin Rabiy'ah bin Abdi Shams bin Abdi Manaaf bin Qusay.

Dada yake Mu’awiyah ni mke wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘‘alayhi wa Sallam), na jina lake ni Mama wa Waislamu Ummu Habibah Ramlah binti Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘‘anha).

 

Imepokelewa kuwa siku moja Abu Sufyaan (baba yake Mu’awiyah) alikwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘‘alayhi wa Sallam) kumuomba mambo matatu. Abu Sufyaan alisema kumuambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘‘alayhi wa Sallam):

 

"Nakuomba mambo matatu".

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akamuuliza:

"Yepi hayo?"

Akasema:

"Uniamrishe nipigane dhidi ya makafiri kama nilivyokuwa nikipigana dhidi ya Waislamu".

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akasema:

"Nimekubali".

"La pili umuache Mu’awiyah awe mwandishi wako."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akasema:

"Nimekubali".

La tatu alimtaka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) amuoe binti yake ‘Azza binti Abi Sufyaan, lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alikataa kwa sababu wakati huo alikuwa keshamuoa binti yake mwengine 'Ummu Habibah' Ramlah binti Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘‘anha).

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akamuambia:

"Ama hilo si halali kwangu."

 

Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mwandishi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam), na pana hitilafu baina ya Maulamaa iwapo alikuwa mwandishi wa Wahyi au alikuwa akimuandikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) barua zake za kawaida tu.

 

 

Umbile lake

Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mrefu, mweupe, mwenye uso wa kupendeza, na alikuwa na nywele nyeusi na ndevu zenye kung'ara kama dhahabu kutokana na rangi ya manjano aliyokuwa akipenda kuzipaka ndevu zake kwayo, jambo ambalo wakati ule lilikuwa ni la kawaida.

 

 

Kusilimu kwake

Zimepokelewa riwaya nyingi kuwa Mu’awiyah alisilimu kabla ya baba yake - Abu Sufyaan, lakini hakujitambulisha kwa kumuogopa baba yake aliyekuwa mkuu wa Maquraysh

Na katika riwaya nyingine inasemekana kuwa alisilimu siku ile ya 'Fat-hu Makkah', siku Waislamu walipouteka mji wa Makkah.

Katika kitabu cha Siyar a’alaam an-Nubalaa, imenukuliwa hadithi yenye udhaifu kutoka kwa Mas’ab az-Zubairiy kuwa Mu’awiyah bin Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:

 

"Moyo wangu ulipendezwa na Uislamu tokea siku ile ya Mapatano ya Hudaybiyay (kabla ya 'Fat-hu Makkah'), na nilipomuhadithia mama yangu akaniambia:

"Usije ukaenda kinyume na baba yako."

"Nikaamua kutomuambia mtu kuwa nimekwishasilimu, lakini baba yangu alijua, na siku moja akaniambia: "Ndugu yako ni bora kuliko wewe, kwa sababu anafuata dini yangu." Nikaudhihirisha Uislamu wangu siku ile Waislamu walipouteka mji wa Makkah."

 

 

Baadhi ya sifa zake

Imepokelewa kuwa siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alipokuwa safarini pamoja na kundi la watu, na katika mazungumzo wakaitaja nchi ya Shaam 'Syria'. Mmoja akasema: "Vipi tutaiweza Shaam wakati Warumi wako huko?"

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) aliyekuwa ameshika fimbo akaipiga begani mwa Mu’awiyah aliyekuwa pamoja nao katika msafara huo, kisha akasema: "Allaah Atakutoshelezeni nao kwa huyu."

 

Baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) kufariki dunia. Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) waliendelea kulieneza neno la Allaah Mashariki ya ardhi na Magharibi yake, huku wakiziteka nchi baada ya nchi kwa ajili ya kuusambaza mwito wa 'Laa ilaaha Illah Llah'.

 

Syria iliyokuwa chini ya utawala wa Byzantine wakati huo ilitekwa na majeshi ya Kiislamu, na Khalifah wa Waislamu aliweka magavana wawili; Abu ‘Ubaydah na Yaziyd bin Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuihukumu nchi hiyo kubwa. Na Yaziyd alipofariki dunia, ‘‘Umar bin Al-Khatw-twaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimchagua Mu’awiyah kuwa gavana wake, kisha akaiweka Shaam yote chini ya uongozi wa gavana mmoja tu, Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu). Na alipotawala ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuacha Mu’awiyah aendelee kuihukumu Shaam yote.

 

Anasema Imam Adh dhahabiy katika Siyar aalam an Nubalaa:

"Mfanyie hesabu zako vizuri yule aliyechaguliwa na ‘‘Umar, kisha ‘‘Uthmaan akamuacha aendelee. Alikuwa mtu anayependa kuweka kila kitu wazi, asiyependa kufichaficha, aliwapenda watu wake nao wakampenda kwa sababu ya upole na ukarimu wake, juu ya kuwa baadhi yao walipata tabu kwake, lakini hivi ndivyo wafalme walivyo.

Walikuwepo Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) waliokuwa bora zaidi kuliko yeye, lakini mtu huyu aliweza kuutawala ulimwengu kwa kuziteka nchi nyingi za makafiri, na kuzifungua nyoyo nyingi kutokana na kupindukia mipaka katika upole wake, kwa umahiri wake na kwa akili yake yenye uwezo wa kuyapima mambo na kutoa uamuzi na rai sahihi katika wakati sahihi."

 

Imepokelewa pia kuwa siku moja mtu alimuambia Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"Mu'awiyah anaswali witri raka'ah moja tu."

 

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyekuwa upande wa Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika vita dhidi ya Mu'awiyah akasema:

"Muache, kwa sababu yeye ni swahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam)." Al-Bukhaariy 3765

 

Anasema Ibn Hajar katika kuisherehesha hadithi hii:

"Yeye ni swahaba, maana yake ni kuwa; asingefanya hivyo isipokuwa alimuona swahibu yake ambaye ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam)." Fat-hul Baariy/Kitab al-Manaaqib

 

Na katika riwaya nyingine, alipoulizwa Ibn ‘Abbaas:

"Nini rai yako juu ya Amiri wa Waislamu (Mu'awiyah), ameswali witri raka'ah moja tu."

Akasema:

"Yeye ni aalim." Al-Bukhaariy 3765 mlango wa Fadhila za Maswahaba

 

 

Siku moja Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliambiwa maneno makali tena ya ujeuri na mmoja katika raia zake, na alipoulizwa:

"Kwa nini hutoi amri akatandikwa bakora?"

Akajibu:

"Ninamsitahi Allaah Asinione kuwa siwezi kuwastahamilia raia zangu". Minhaaj As-Sunnah - Ibn Taymiyah - Juzuu ya 4 ukurasa wa 384

 

Anasema Ibn Kathiyr:

"Na hii ndiyo sababu iliyowafanya watu wa Shaam kumpenda sana na kufungamana naye kwa hamasa kubwa na kujitolea kwa hali na mali bila kurudi nyuma alipowataka wainuke na kudai kilipwe kisasi cha kuuawa kwa ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu)."

Al-Bidaayah wan- Nihaayah 131

 

 

Jihaad Yake

Zimepokelewa baadhi ya riwaya kuwa Mu’awiyah ndiye aliyemuua Musaylimah al-Kadhaab, (Mtume wa uongo), na alipata sifa nyingi sana katika vita vya Yarmuwk kutokana na ujasiri wake, na yeye ndiye aliyekuwa jemadari mkuu wa majeshi ya Kiislamu yaliyoiteka nchi ya Qisariya wakati wa Ukhalifa wa ‘‘Umar bin Al-Khatw-twaab (Radhiya Allaahu ‘anhu). Na wakati wa Ukhalifa wa ‘‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mu'awiyah ndiye aliyeongoza majeshi ya baharini ya Waislamu yaliyoiteka nchi ya Cyprus, na alishiriki pia katika kuziteka nchi nyingi za Kinasara.

 

Imepokelewa katika hadithi sahihi kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) amesema:

"Wa mwanzo kuteka nchi kwa njia ya bahari imewawajibikia 'imewalazimikia'". Al-Bukhaariy 122/6 Mlango wa Jihad na Siyar

 

Anasema Ibn Hajar: "Imewawajibikia, maana yake ni kuwa wametenda kitendo kilichowajibisha kuingizwa Peponi."

 

Anasema Yaziyd bin ‘Ubaydah: "Mu'awiyah aliiteka nchi ya Cyprus katika mwaka wa ishirini na tano baada ya kuyashinda vibaya majeshi ya baharini ya Byzantine."

 

Na hili lilikuwa jeshi la mwanzo la baharini la Kiislamu lililoundwa wakati wa Ukhalifa wa ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alishiriki pia katika vita vya Hunayn akiwa upande wa Waislamu. Vita hivi vilifuatilia kutekwa kwa Makkah, na katika ngawira ya vita hivyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alimgawia Mu’awiyah ngamia mia moja. Na kutokana na kushiriki kwake vita vya Hunayn Mu'awiyah anaingia katika kundi la walioteremshiwa utulivu na Allaah siku hiyo.

 

Allaah Anasema:

"Kisha Allaah Akateremsha utulivu Wake juu ya Mtume Wake na juu ya walioamini. Na Akateremsha majeshi (ya Malaika) ambayo hamkuyaona." At-Tawbah – 9

 

Mu'awiyah alishiriki pia katika vita dhidi ya waliortadi wakati wa Ukhalifa wa Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) vilivyotokea mara baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) kufariki dunia, na alishiriki pia katika vita vya kuziteka nchi za Swayda, Arqah, Jubayl, Beirut na nyingi nyingine.

 

Katika mwaka wa 60 Hijri, mfalme wa Warumi aliingiwa na tamaa alipowaona ‘Aliy na Mu'awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhum) wamejishughulisha na vita vya wenyewe kwa wenyewe, akajaribu kuteka baadhi ya miji iliyokuwa chini ya utawala wa Kiislamu. Historia haitosahau barua ya Mu'awiyah aliyomuandikia mfalme huyo wa Warumi akimuambia:

"Wallahi kama hutofunga virago vyako ukarudi ulikotoka ewe uliyelaaniwa', nitapatana mimi na mtoto wa ami yangu dhidi yako, kisha tutakuja kukutoa katika nchi zako zote, kisha tutaifanya yote ardhi iwe dhiki kwako juu ya wasaa wake."

 

Hofu iliingina ndani ya moyo wa mfalme yule wa Kirumi aliyeamua kuondosha majeshi yake katika miji yote aliyoiteka na kurudi kwao huku akiomba suluhu. Al-Bidaayah wan-Nihaayah 119/8

 

 

Ugavana wake

Alipokuwa gavana wa Shaam, Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiwapenda raia wake na wao wakimpenda. Alihukumu nchi ya Shaam kama ni gavana muda wa miaka ishirini, na miaka ishirini mingine alihukumu akiwa Khalifa wa Waislamu, na wakati wa utawala wake hajawahi kutokea aliyempinga. Bali watu wote walikuwa kitu kimoja nyuma yake.

 

‘‘Umar bin Al-Khatw-twaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoitembelea nchi ya Syria, alipokelewa na gavana Mu’awiyah aliyekuja na jeshi kubwa la wapanda farasi waliovaa vizuri sana.

 

‘‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamuambia:

"Hivi ndivyo ulivyo? Unanifanyia mapokezi mkubwa kama haya wakati yamenifikia mashitaka kuwa watu hawaruhusiwi kuingia nyumbani kwako kwa ajili ya kufikisha malalamiko yao. Kwa nini unafanya hivi? Nitakupa adabu ya kutembea kwa miguu tena bila ya viatu kutoka hapa mpaka Hijaaz (Saudia)".

Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamuambia:

"Ewe Amiri wa Waislamu, tuko katika nchi iliyojaa majasusi wa maadui zetu, kwa hivyo lazima tuwaonyeshe nguvu zetu kwa ajili ya kuwatisha. Utakachoniamrisha nitakutii na utakachonikataza nitakiacha".

 

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Daawuud kuwa;

Siku moja Abu Maryam Al-Azdiy aliingia kwa Mu’awiyah akamuambia:

"Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akisema:

"Mtu akijificha asionane na watu wake na kujiepusha na kuwasaidia katika shida zao, na Allaah pia Atajiepusha naye mtu huyo na hatomsaidia katika shida zake".

Anasema: "Hadithi hii ilimfanya Mu’awiyah abadilike akawa yeye ndiye mwenye kufuatilia watu na kuwasaidia". At-Tirmidhy

 

Imepokelewa pia kuwa siku moja Mu’awiyah alipotoka nje kwa ajili ya kukutana na watu wake, watu walimnyanyukia. Mu’awiyah akawaambia:

"Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akisema:

"Yeyote anayependa kunyanyukiwa, basi ajitayarishie makazi yake Motoni". Ahmad - Abu Daawuud – At-Tirmidhy na wengineo.

 

 

Vita baina ya makundi mawili

Baada ya Khalifa wa tatu wa Waislamu ‘‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuuliwa, dola ya Kiislamu ilibaki bila kiongozi muda wa siku tano, na aliyekuwa akitamba huku akiamrisha na kukataza wakati wote huo pale Madina alikuwa Al-Ghafiqiy bin Harb mtu aliyemuua Khalifa ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Watu walimuendea ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) mara mbili kumtaka awe Khalifa wao, na mara zote hizo alikataa. Lakini walipomuendea mara ya tatu ilimbidi akubali kwa ajili ya kuukoa Ummah kutokana na fitna kubwa iliyowakabili wakati ule.

 

Ahlus-Sunnah wanaamini kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni Swahaba bora kupita wote baada ya Abubakar na ‘‘Umar na ‘‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhum), juu ya kuwa wapo waliokhitalifiana baina ya ‘Aliy na ‘‘Uthmaan yupi aliyemzidi mwenzake.

 

Hitilafu iliyotokea baina ya ‘Aliy na Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhum) ni kuwa Mu’awiyah alikataa kufungamana na Khalifa mpya ‘Aliy mpaka kwanza awakamate wauaji wa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu), wakati ‘Aliy alimtaka Mu'awiyah afungamane naye kwanza ili Ummah uweze kuungana tena na kusikilizana na kuwa kitu kimoja, na kuuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kuiepusha dola ya Kiislamu kugeuzwa kuwa tonge jepesi linaloweza kumegwa na kumezwa kwa wepesi na adui, baada ya hapo wataweza kuzungumza juu ya wauaji.

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alituma barua kwa njia ya mjumbe aitwaye Jariyr bin ‘Abdullah kumpelekea Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu), aliyekuwa gavana wa Shaam, na ndani ya barua hiyo aliandika:

"Bisimillahi Rahmaani Rahiym,

Amma baad, kwa vile watu wote wamefungamana nami katika mji wa Madina, basi nawe pia uliyeko huko Shaam unalazimika kufungamana nami. Na hii ni kwa sababu watu waliofungamana nami ni wale wale waliofungamana na Abubakar na ‘Umar na ‘Uthmaan. Kwa hivyo aliyehudhuria hana haki ya kulikataa na asiyehudhuria hana haki ya kulipinga. Kwa hakika ushauri ni wa Muhaajirin na Answaar (Watu wa Makkah na wa Madina). Wanapokubaliana wote juu ya mtu na kumchagua kuwa ni Imaam wao, na Allaah Anaridhika na uchaguzi wao

Nimemtuma kwako Jariyr, naye ni katika watu wa Imani na watu waliohajir, kwa hivyo fungamana nami - Walaa quwwata illa billaah!!" Nahjul-Balaaghah- uk. 427 mlango wa 6

 

Baada ya kuisoma barua hiyo, Mu’awiyah aliwataka watu wote wakusanyike msikitini kwa ajili ya kuwashauri. Akapanda juu ya mimbari kuwahutubia, na yafuatayo ni miongoni mwa aliyosema:

"Hii ni barua ya ‘Aliy akinitaka nifungamane naye, na mimi kama mjuavyo nimerithishwa nchi ya Shaam na ‘‘Umar, kisha nikarithishwa na ‘‘Uthmaan, na ‘Uthmaan kama mnavyojuwa ameuliwa kwa kudhulumiwa.

 

Na Allaah Anasema:

"Na mwenye kuuawa kwa kudhulumiwa, basi Tumempa nguvu mrithi wake huyo, akitaka ataomba kwa Hakimu kuwa amuuwe kama alivyomuuwa mtu wake na akitaka atamsamehe". Bani Israaiyl – 33

 

Kwa hivyo ninataka nyinyi wenyewe muniambie uamuzi wenu katika jambo hili".

Wote kwa pamoja wakasema:

"Bali tunataka damu yake isipotee bure!!".

 

Mu’awiyah alimuandikia ‘Amru bin Al-‘Aas (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa amekwishastaafu wakati huo, na alikuwa akiishi katika nchi ya Palestina kumtaka ushauri na kutaka msaada wake.

 

Zimepokelewa hadithi nyingi kwa njia mbali mbali kuwa siku moja Abu Muslim Al-Khulani alikwenda kwa Mu’awiyah akiwa na kundi la watu na kumuuliza:

"Ewe Mu’awiyah, unashindana na ‘Aliy kwa sababu unadhania kuwa wewe ni sawa naye?"

Mu’awiyah akajibu:

"Wallahi mimi najua kuwa yeye ni bora kuliko mimi na mwenye haki zaidi kuliko mimi. Lakini nyinyi wenyewe hamuelewi kuwa ‘Uthmaan ameuliwa kwa kudhulumiwa na kwamba mimi ni mtoto wa ami yake, na nina haki ya kudai kisasi cha damu yake? Muambieni anikabidhi waliomuua na mimi nitamkabidhi kila kitu".

 

Wakamuhadithia ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), ambaye hakujibu kitu, jambo lililowafanya watu wa Shaam wazidi kujitayarisha kivita.

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliondoka Al-Kuufa kuelekea Shaam akiwa na jeshi kubwa la watu wapatao mia moja elfu, na mapambano makali yalitokea baina ya makundi mawili hayo mahali panapoitwa Swiffiyn, na maelfu ya Waislamu walipoteza roho zao, jambo lililosababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya Ummah na hatimaye kujitokeza kundi lingine lililojulikana kwa jina la Khawaarij, na ndani ya kundi hilo alitokea muuaji wa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Mwanangu huyu ni bwana

Baada ya vita vya Swiffiyn kusimamishwa, na mapatano kufikiwa baina ya makundi mawili hayo, na kabla ya sulhu kukamilika, ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliuliwa alipokuwa akiwaamsha watu Swalah ya alfajiri, na aliyemuua alikuwa mtu kutoka kundi la Khawaarij aitwae ‘Abdur-Rahmaan bin Muljim al Muradiy.

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na kawaida ya kutoka peke yake bila ya ulinzi kuwaamsha watu Swalah ya alfajiri, na kwa ajili hiyo ilikuwa rahisi kwa muuaji huyo kumshambulia kwa upanga alioulaza ndani ya sumu muda wa mwezi mzima.

 

Waislamu wakamchagua mwanawe Al-Hasan bin ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Khalifa wao, na baada ya kutawala muda wa miezi sita, Al-Hasan aliamua kujiuzulu kwa hiari yake na kumuachilia Ukhalifa Mu’awiyah bin Abi Sufyaan kwa ajili ya kuupatanisha Ummah.

 

Na katika mwaka wa 41Hijriyah, Al-Hasan na Mu'awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhum) baada ya kupatana waliingia kwa pamoja mji wa Al-Kuufah wakiwa wamepanda farasi wao, na kwa ajili hiyo wakaweza kuurudisha Ummah kwa mara nyingine chini ya bendera moja, na kuviepusha vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe, na juu ya yote Al-Hasan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifanikiwa kuisadikisha kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) aliposema juu yake:

"Mwanangu huyu ni bwana, na huenda Allaah Akamjaalia kuwa mpatanishi wa makundi mawili matukufu ya Waislamu". Al-Bukhaariy na wengine

 

Al-Hasan mwana wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambae Mashia wanaitakidi kuwa ni Imaam wa pili aliyekingwa (Al-Ma’aswuum) alifanya suluhu na Mu'awiyah na kumuachia uongozi wa kuwaongoza Waislamu katika Utawala wao, Sheria zao, Ibada zao na katika Jihaad yao dhidi ya makafiri, na hii ni dalili wazi kuwa Mu'awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mtu mwema na kwamba Imaam wa pili wa Waislamu katika itikadi za Mashia aliridhika naye kwa kumkabidhi uongozi wa Ummah.

Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa kila anapomuona Al-Hasan bin ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akimuambia:

"Marhaban mwana wa Mtume wa Allaah."

Na anapomuona mwana wa Az-Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akimuambia:

"Marhaban ewe mwana wa ami yake Mtume wa Allaah na mwanafunzi wake." Al-Bidaayah wan-Nihaayah - Juzuu ya nane - Uk. 137

 

 

Katika kitabu kinachoheshimiwa sana na Mashia kilichoandikwa na Sharif Ridha kiitwacho 'Nahjul-Balaaghah', imenukuliwa ndani yake barua aliyoiandika ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) inayosema:

"Tulipambana na wenzetu watu wa Shaam (jeshi la Mu’awiyah), na imenidhihirikia kuwa Muabudiwa wetu wa haki ni mmoja na Mtume wetu ni mmoja na wito wetu katika Uislamu ni mmoja wala hatukanushi kuwa wao ni wenye kumuamini Allaah na Mtume wake na wala hatukanushi kuwa sisi pia tunamuamini Allaah na Mtume wake. Isipokuwa tumekhitilafiana juu ya damu ya ‘Uthmaan tu, ambayo mimi nimetakasika nayo (niko mbali nayo)." Nahj Al Balaghah uk. 525 mlango wa (58) 'Barua alizotuma miji mbali mbali kuhusu vita vya Swiffiyn.' Chapa ya Qum-2005

 

 

Mu'awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliingia vitani dhidi ya majeshi ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa ijtihadi yake akizitegemea hadithi mbali mbali za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam).

 

Imepokelewa kuwa siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam), alisema kumuambia ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"Ewe ‘Uthmaan! Siku Allaah Atakapokupa uongozi wa mambo haya, kisha wanafiki wakakutaka uivue nguo aliyokuvisha, usije ukakubali kuivua."

 

Anasema Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha):

"Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alimuambia ‘Uthmaan maneno haya mara tatu." At-Tirmidhy na Ibni Majah katika mlango wa Fadhila za Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) nambari 112

 

Imepokelewa pia kuwa aliposimama msitari wa mbele katika jeshi la Mu’awiyah, Ka’ab bin Murrah (Radhiya Allaahu ‘anhum) alisema:

"Lau kama si maneno niliyomsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akitamka, nisingepigana nikiwa upande wa Mu’awiyah kwa ajili ya kulipa kisasi cha ‘Uthmaan bin ‘Affaan. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) siku hiyo alizungumza juu ya 'fitan' - (mitihani na vita vya wenyewe kwa wenyewe), na alipokuwa akizungumzia mambo hayo alipita mtu akiwa amejifunika uso. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akasema:

"Mtu huyu siku hiyo atakuwa katika uongofu". Nikamfuata mtu huyo ili nimjue nani. Alikuwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan. Nikamkabili Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na kumuuliza: "Huyu?"

Akaniambia:

"Ndiye."

At-Tirmidhiy kutoka kwa Abi al Ash'ath as-Swana’aniy - mlango wa Al Fadhaail hadithi nambari 3704

 

 

Kutokana na hadithi hizi, ilimbainikia Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) pamoja na waliokuwa naye, kuwa wamo katika haki, hasa kwa vile wauaji wa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) walikuwemo ndani ya jeshi la ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Na kwa sababu hizi Mu’awiyah alimuandikia ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akimuambia:

"‘Uthmaan ni mtoto wa ami yangu, na ameuliwa kwa kudhulumiwa na mimi ni mrithi wake, na Allaah Anasema:

"Na mwenye kuuawa kwa kudhulumiwa, basi Tumempa nguvu mrithi wake huyo, akitaka ataomba kwa Hakimu kuwa amuuwe kama alivyomuuwa mtu wake na akitaka atamsamehe." Bani Israaiyl - 33

 

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye kwa upande wake aliona kuwa kwa vile yeye ndiye aliyechaguliwa kuwa Khalifah wa Waislamu, iliwabidi magavana wote wamtambue kwanza, na kwamba ni yeye tu kama ni Imaam wa Ummah mwenye haki ya kulipiza kisasi hicho, na aliona pia kuwa wakati bado haujafika.

 

Kwa hivyo wote wawili wamejitahidi katika kutoa hukmu zao, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) amesema:

"Anapohukumu hakimu akajitahidi na kusibu, analipwa ujira mara mbili, na anapohukumu akakosea, analipwa ujira mara moja." Al-Bukhaariy

 

 

Utawala wake

Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa Khalifa wa Waislamu muda wa miaka ishirini, na wakati wote huo dola ya Kiislamu ilikuwa yenye nguvu, tulivu, yenye amani, na umoja.

Dola kubwa kubwa zilisalimu amri mbele ya majeshi yake. Utawala wake ulizijumuisha nchi za Makkah na Madina, Misri, Shaam 'Syria' (iliyokuwa kabla ya hapo chini ya utawala wa Byzantine), Iraaq, Khurasaan, Persia na Bara ya Arabu yote ikiwemo Yemen na Morocco na nchi nyingi nyingine

 

Anasema Imaam Ahmad kuwa amehadithiwa na Ruuh kuwa amemsikia Abu Umayyah ‘Amru bin Yahya akisema:

"Nilimsikia babu yangu akisema kuwa siku moja Mu’awiyah alikijaza chombo chake maji akamfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) amtawadhishe. Na alipokuwa akimtawadhisha, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) aliunyanyua uso wake mara moja au mara mbili kumtazama Mu’awiyah, kisha akamuambia:

"Ewe Mu’awiyah, utakapopewa uongozi umuogope Allaah na uwe muadilifu".

Anasema Mu’awiyah:

"Nikatambua kuwa nitapambana na mtihani huo kama alivyoniambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) mpaka nilipokumbana nao". Hadithi hii imepokelewa pia kutoka kwa Ibn Abid-Duniya na Abu Ya’ala. Al Fat-h 121/6

 

 

Imepokelewa pia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alimuombea Mu’awiyah dua nzuri aliposema:

"Allaah mjaalie awe muongofu mwenye kuongoza". At-Tirmidhy mlango wa Manaaqib, Imaam Ahmad mlango wa Musnad Ash-Shamiyn, At-Twabaraaniy na wengi wengine.

 

‘Umar bin Al-Khatw-twaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomteua Mu’awiyah kuwa gavana wa Syria, baadhi ya watu walimuuliza:

"Kwa nini unampa ugavana wakati huyu ni kijana mdogo bado?"

‘Umar akawaambia:

"Nifanye nini ikiwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) mwenyewe amemuombea dua akasema:

"Allaah mjaalie awe muongofu mwenye kuongoza?"

 

 

Anasema Ibn Kathiyr katika Al-Bidaayah wan-Nihaayah:

"Katika utawala wake, Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifanya mashambulizi mara kumi na sita katika nchi za Kirumi na kuziteka nchi nyingi. Alikuwa akipeleka majeshi yake siku za joto mara moja na siku za baridi mara moja, na majeshi yake yaliweza kufika na kuteka mpaka Constantinople (Straits) - Mlango wa bahari ya nchi inayojulikana hivi sasa kwa jina la Uturuki."

 

Huyu ndiye Mu’awiyah ambaye mmoja katika Maulamaa wakubwa wa wakati wake aliyekuwa mwandishi wa ‘Umar bin ‘Abdul-Aziyz aitwae Sulaymaan bin Mahran Al-A’amash, na huyu kutokana na ukweli wake alikuwa akiitwa 'Msahafu', alikuwa akimfadhilisha Mu’awiyah kuliko ‘Umar bin ‘Abdul-Aziyz (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Inajulikana kuwa Maulamaa wengi wamempa ‘Umar bin ‘Abdul-Aziyz heshima ya kuwa Khalifa wa tano muongofu wa Waislamu kutokana na uadilifu wake.

 

 

Kufariki kwake

Imepokelewa kuwa katika maradhi yake ya mwisho Mu'awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alihutubia watu akasema:

"Hakika mimi ni mavuno yaliyokwishavunwa. Na utawala wangu umekuwa mrefu sana mpaka nimekuchosheni, na mimi pia nimekuchokeni. Na wala hatokuja baada yangu akawa bora kuliko mimi, kama vile waliokuja kabla yangu walikuwa bora kuliko mimi. Mola wangu hivi sasa napenda kukutana na Wewe, na Wewe nakuomba upende kukutana na mimi."

 

Alipokuwa akikata roho, Mu'awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:

"Nilikuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) katika jabali la Safa'a, nikamuona akikata nywele. Nilikusanya baadhi ya nywele zake, kwa hivyo nitakapokufa chukueni nywele hizi na muzitie mdomoni na puani mwangu." Al-Bidaayah wan-Nihaayah na Siyar a’alaam an-Nubalaa

 

Alifariki dunia mjini Damascus akiwa na umri wa miaka sabini na nane, katika mwezi wa Rajab mwaka wa sitini baada ya Hijra, na aliusia akafiniwe kwa nguo aliyopewa zawadi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam).

 

 

 

Hitimisho

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anapoleta Mitume, huwatayarishia katika umati wao watu watakaosimama nao na kuwasaidia, na hawa ni Swahibu zao, au Maswahaba wao. Na Allaah Subhanahu wa Taaala Amemkirimu Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) kwa kumtayarishia Swahaba wake, kisha akawasifia katika kitabu chake kitukufu kuwa ni Ummah bora kupita Ummah zote.

 

Allaah Anasema:

"Nyinyi ndio Ummah bora kuliko Ummah zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni) – mnaamrisha yaliyo mema na mnakataza yaliyo maovu."

Aali ‘ Imraan – 110

 

Kisha Akawasifia tena na tena katika aya mbalimbali ndani ya Qur-aan tukufu Aliposema:

"Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao waliotoa baadae na wakapigana. Na wote hao Allaah Amewaahidia wema." Al-Hadiyd -10

 

Wema aliowaahidia ni Pepo. Na Allaah Amewapa Swahaba hao bishara njema kuwa Atawaepusha pia na Moto Aliposema:

"Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na hayo.  Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale zinayoyatamani nafsi zao.

Hicho Kitisho Kikubwa hakitowahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa!" Al-Anbiyaa 101-103

 

Na hii haina maana kuwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wamekingwa na kufanya makosa 'Maasuwmiyn' au 'hawakosei'. Bali wao ni viumbe wanaokosea kama viumbe wengine. Tunachokatazwa ni kuwatuhumu Maswahaba hawa waliotukuzwa na Allaah au kuwadhalilisha kwa chuki tu. Kwa sababu hawa ndio walioibeba Qur-aan hii tukufu wakaifikisha kwetu, na kuieneza sehemu zote za ulimwengu. Bila ya juhudi zao na kujitolea kwao mhanga kwa hali na mali kwa ajili ya kulieneza neno la Allaah, dini isingetufikia, na tungelibaki mpaka leo tukisujudia moto na masanamu.

 

Katika Maswahaba hao watukufu ni Mu'awiyah bin Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhuma). Hata kama tutahitilafiana tukasema kuwa alisilimu baada ya ufunguzi wa Makkah, Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Amekwishambashiria Pepo Swahaba huyu (Radhiya Allaahu ‘anhu) Aliposema:

"Na wote hao Allaah Amewaahidia wema."

Na wema kama tulivyotangulia kusema kuwa maana yake ni Pepo.

 

Imeelezwa na Ibnul ‘Arabiy Al-Maalikiy katika kitabu cha 'Al-‘Awaasim' kuwa:

Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoingia Baghdad alikuta juu ya milango ya misikiti imeandikwa:

"Bora wa watu baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) ni Abubakar kisha ‘Umar kisha ‘Uthmaan kisha ‘Aliy kisha Mu’awiyah mjomba wa Waislamu wote."

Mu'awiyah hakufanya chuki wala hakuchukua hatua yoyote ya kulifuta jina la ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyetangulizwa kabla yake kwa ubora.

 

 

Na alipoulizwa ‘Abdullaah bin Mubaarak:

"Yupi bora Mu’awiyah bin Abi Sufyaan au ‘Umar bin ‘Abdul-‘Aziyz?"

Alisema:

"Wallahi lile vumbi lililokuwa likiingia puani mwa Mu’awiyah akiwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) ni bora kuliko ‘Umar mara elfu. Mu’awiyah aliswali nyuma ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam), na Mtume alipokuwa akisema:

"Samia Allaah liman hamidah', Mu’awiyah alikuwa akisema; 'Rabbanaa walaka l hamd', unataka nini tena zaidi ya hayo?" Wafayatul a’ayan - Ibni Khalqaan (3/33) na kitabu cha Ash- Shari’ah Al-Aajiri (0/2466) Al-Bidaya wan-Nihaayah 13/8

 

Imepokelewa kuwa mtu mmoja alimuuliza Al-Muafiy bin Amran:

"Ewe Aba Mas’uud, Iko wapi daraja ya Mu’awiyah mbele ya ‘Umar bin ‘Abdul-‘Aziyz?"

 

Anasema Al-Jaraah Al-Mausaliy msimulizi wa hadithi hii:

"Alikasirika sana Al Muafiy akasema:

"Huwezi kumfananisha Swahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na mtu yeyote yule. Na Mu’awiyah si Swahaba tu, bali alikuwa pia mwandishi wake, Shemeji yake na mwaminifu wake katika Wahyi wa Allaah Mtukufu."

 

Anasema Muhyid-Diyn al-Khatwiyb:

"Niliulizwa na mmoja kati ya vijana wa Kiislamu nini rai yangu juu ya Mu’awiyah, nikamuambia:

"Mimi nani hata unaniuliza juu ya Mu’awiyah, huyu ni mtukufu katika watukufu wa Ummah huu, Swahaba wake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na katika wabora, yeye ni taa miongoni mwa taa zinazomulika njia, isipokuwa taa hii ilikuja wakati taa nne ziking'ara duniani, kwa hivyo nuru yake ikashindwa nguvu na taa hizo.”

 

Tumsikilize Sayiduna ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema nini juu ya Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika kitabu cha Nahjul-Balaaghah:

"Natamani Wallahi lau kama Mu’awiyah atakubali nibadilishane naye kama inavyobadilishwa Dinari kwa Dirham. Achukue watu wangu kumi, na badala yake anipe mmoja tu katika watu wake" (224/39)

 

Alipoulizwa Hasan Al-Basry (Radhiya Allaahu ‘anhu) juu ya ‘Aliy na Mu’awiyah alisema:

"Huyu amehusiana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na yule amehusiana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam). Huyu katika waliotangulia na yule si katika waliotangulia, na sisi sote tumeingizwa katika mtihani."

 

Na katika riwaya nyingine akasema:

"Sikuridhika na Mu’awiyah katika mambo mawili tu:

Alipoingia vitani na ‘Aliy, na alipomteua mwanawe kuwa Khalifah baada yake."

 

Katika Siyrah yake Mu'awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) tumeona namna gani alivyopata sifa mbali mbali kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam), kutoka kwa Swahaba watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum), kutoka kwa watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam), na pia tumeona namna gani anavyoingia katika sifa mbali mbali za watu wema walioahidiwa Pepo zilizotajwa ndani ya Qurani tukufu.

 

Allaah Anasema:

Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.” Al-Hashr: 10

 

Tunamuomba Allaah Asiingize undani ndani ya nyoyo zetu kwa wenzetu waliotangulia, Atufufue pamoja na wale aliowaahidi Pepo chini ya bendera na Mtume wake mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam), tunywe pamoja katika hodhi lake kinywaji ambacho baada yake hatutokuwa na kiu tena. Aamiyn

 

 

Share