Twalhah Bin 'Ubaydillaah (رضي الله عنه)

Talha Bin 'UbaydiLLaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

 

Na Muhammad Faraj Saalim As-Saiy

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema;

 

 

مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّـهَ عَلَيْهِ ۖ فَمِنْهُم مَّن قَضَىٰ نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن يَنتَظِرُ ۖ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِيلًا  

 

"Miongoni mwa Waumini, (wapo) wanaume wamesadikisha yale waliyomuahidi Allaah; basi miongoni mwao aliyetimiza nadhiri yake (aliyekufa shahidi), na miongoni mwao anayengojea (siku yao kufika); na hawakubadilisha (ahadi yao) mabadiliko yoyote".   [Suuratu Al-Ahzaab 23.]

 

 

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliisoma aya hii akiwa amewakabili Maswahaba wake (Radhwiya Allaahu 'anhum), kisha akamuashiria Talha (Radhwiya Allaahu 'anhu) huku akisema;
"Anayetaka kufurahi huku akimuangalia mtu anayetembea juu ya ardhi akiwa keshaitimiza ahadi yake (anayetaka kumtizama aliyekufa shahidi aliye bado yuhai) basi amtizame Talha".

 

Hii ni bishara njema aliyopewa Talha (Radhwiya Allaahu 'anhu) baada ya kukatika sehemu ya mkono wake katika vita vya Uhud, bishara ambayo kila Muislaam anatamani ahusishwe nayo.

 

 

Talha (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisikia habari za dini hii mpya na juu ya Rasuli Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa safarini kwa ajili ya biashara katika nchi ya Sham wakati alipoonana na mmoja katika wachaji Allaah wakubwa wa nchi hiyo.
Kuhani huyo wa kinaswara alimwambia Talha;
"Ule wakati wa kuja kwa Rasuli mpya atakayetokea katika ardhi takatifu umekwishawadia. Nakutahadharisha usije ukakupita msafara huo wa kheri na rehma na utakatifu bila kujiunga nao".

 

Baada ya mwezi, Talha (Radhwiya Allaahu 'anhu) alirudi Makkah, na haukupita muda mrefu akaanza kusikia juu ya habari za yule aliyekuwa akijulikana kwa jina la Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Mkweli na Mwaminifu na juu ya wahyi anaoupata kutoka mbinguni na juu ya ujumbe alokuja nao.

 

Suali la mwanzo alouliza Talha mara baada ya kupata habari hizo, ni juu ya rafiki mpenzi wa utotoni wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aitwae Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu). Alipojulishwa kuwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) naye yuko pamoja na Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akasema;
"WaLLahi wawili hawa hawawezi kuungana katika jambo la upotovu abadan. Huyu Muhammad ambaye umri wake umefikia miaka arubaini, na sisi tunamjuwa vizuri kuwa tokea utotoni mwake hakupata hata siku moja kusema uongo, aseme uongo leo baada ya kufikia umri huu? Tena juu ya Allaah? Ama jambo hilo haliwezekani kabisa'.
Talha (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) na huko hakuchukua muda mrefu wakaondoka wote wawili mpaka nyumbani kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kusilimu, na kwa ajili hiyo akawa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika Dini hii tukufu.

 

Katika vita vya Uhud, wakati jeshi la Waislam liliporudi nyuma baada ya Makureshi kufanikiwa kuwazungukia na kupashika mahala walipokuwa wamekaa watupaji mishale, Talha alimouna Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mbali akiwa amezungukwa na maadui huku akipigana na damu ikimtiririka usoni pake. Bila ya kufikiri, Talha aliruka kama simba na kupakimbilia mahali hapo huku akiwaruka makafiri waliokuwa wakija kutoka huku na kule. Alipita mbele yao huku panga na mikuki ikitupwa ovyo kutoka upande wa makafiri, mpaka akaweza kumfikia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumsaidia.
Talha alimfikia Rasuli  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akawa anapigana kwa nguvu zake zote na kwa ujasiri mkubwa kwa ajili ya kumkinga.

 

 

Alikuwa akipigana kwa mkono wake wa kulia huku mkono wake wa kushoto ukifanya kazi ya kumsukuma nyuma Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumweka mbali na hatari ya maadui waliokuwa wakijaribu kila njia kumfikia, na wakati huo uso wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ulikuwa umejaa damu.

Anasema Bibi 'Aaysha (Radhwiya Allaahu 'anhaa);
"Abu Bakr akitajiwa tu vita vya Uhud, alikuwa akisema;
"Siku ile yote ilikuwa ya Talha. 

 

 

Nilikuwa wa mwanzo kumfikia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mimi na Abu 'Ubaydah, na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

"Mtizameni ndugu yenu", tukamtizama, tukamuona amejaa alama za panga na mikuki zisizopungua sabini na tukaviona vidole vyake vikiwa vimekatika".
Huyu ndiye Talha ambaye Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kusema juu yake na juu ya Az-Zubair; "Talha na Az-Zubair majirani zangu Peponi".

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share