Bibi Aliyemlea Na Amefariki Anaweza Kumuombea Du'aa Na Kumfanyia Wema? Du’aa Gani Ya Kuwaombea Waliofariki?

SWALI LA KWANZA:

A.aleikum. Napenda kuuliza bibi yangu mzaa mama amefariki ambae ndie mlezi wangu na nampenda kama mama toka nafungua macho namuona yeye, je nikimaliza kusali naweza kumuombea duaa “rabbi arhamhumaa kama rabayani saghira”? Kwani baba yangu pia amefariki lakini mama yangu yuhai. Nataka shauri nifanyeje ili duaa zangu zimfikie? Asanteni.


   

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu du’aa ya kumuombea bibi yako. Tufahamu kuwa du’aa unayoomba inawafikia hata Waislamu wengine ambao huna uhusiano nao wa kidamu kama Anavyosema Aliyetukuka:

Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walioamini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu” (59: 10).

Kwa hiyo yule aliyekulea na akawa na uhusiano nawe wa kidamu du’aa zako za kila wakati na hasa zile nyakati za kukubaliwa kama masiku ya manane, na baina ya Adhaan na Swalah, na kadhalika inakuwa zaidi. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyoyafanya mwenyewe? Na kwamba vitendo vyake vitaonekana?” (53: 39 – 40).

Ibn Kathiyr anasema kwamba hivi ni vitendo alizofanya Muislamu akiwa hai na mtoto ni katika vitendo vyake. Na kwa kuwa bibi alikufanyia wema, na hakuna ihsani iliyo kubwa kama kupatiwa malezi mazuri ya Kiislamu. Hivyo, muombee du’aa hiyo uliyoitaja na nyengine za kumuombea Pepo na mema ya Kesho Akhera.

Pia unaweza ukawa unamtolea sadaka kwa niaba yake au ukapeleka misahafu Msikitini na Madrasa, kwani kusomwa ule msahafu na watoto au yeyote inampatia aliyefariki thawabu kutoka kwa Allaah Aliyetukuka.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share