Anaishi Nje Ya Nchi, Wakwe Zake Wanamzuia Mtoto Wake Asiende Kwa Wazazi Wake

SWALI:

Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabaratu.

Mimi niko na mtoto wakiume yuko na miaka sita,mimi niko safari na mumewangu lakini mtoto tumemuwacha kwa watu wa mume wangu,shida ni kwamba watu wake hawataki mtoto aende kwetu,nikumwambia mume wangu asema yeye hayaingilii watu wakwao wafanye vile wanavyotaka,mamake na babake wakiamuwa huyo mtoto pia asiende kwetu kabisa basi ndio hivyo kwani yeye ataka radhi za wazee wake,je hiyo ni sawa?na mwenye kuamuwa yote haya ni dadake mkubwa ndiye anayetaka kutupangia sisi mambo anavyotaka yeye sio waume zetu,je ni sawa?atakalo sema yeye ndilo litakalo fuatwa,mimi huuliza je nimeolewa na mume au na family nzima?kwasababu ni mambo yakushangaza,kila mtu ataka kukucontrol wewe mke mmoja.

Waiting for reaply

Shukran

 

SWALI JINGINE:

 Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatu.

ningependa munitatulie tatizo hili.mimi niko safari na niko na mtoto wangu mwenye miaka sita ambaye hatukusafiri nayeye tumemuacha na nyanyake mzaa baba,lakini hataki kukaa huko ataka kwenda kwetu lakini babake na watu wake hawataki aende akakae kwetu,hivi anamwezi na siku kadhaa hajakwenda kwetu akisema ataka kwenda kwetu aambiwa angojee mpaka school zifungwe na school zikifungwa yeye yuwasafiri kuja huku kutuangalia kwa sababu ya viza isiharibike,school niliyomtia ni karibu na nyumbani kwetu pia ametolewa bila ya mimi na babake kujuulishwa,dadangu akienda school kumjulia aambiwa haendi school,nikamwambiya babake ajulie ndipo alipoambiwa ametolewa na kutiwa school nyingine ili asipate nafasi ya kwenda kwetu. na kila akienda kwetu huambiwa hakuna kulala huko na hutishiwa atachapwa,hivi mimi nimeamuwa nirudi nikakae na mwanangu.Je nifanyeje?


 

JIBU:

Sifa zote njema zamstahikia Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Rehma na amani zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako.

Mtoto ni wenu nyote na wazazi wa baba wana haki kama walivyo na haki hiyo hiyo wazee wa mama; hivyo basi kumzuia mtoto wakati wowote ule kwenda kwa mama yake au baba yake au kumzuia kwenda kwa wazee wa mama yake au wazee wa baba yake ni moja kati ya yenye kueleweka kama ni kuvunja udugu, na hilo ni katika madhambi makubwa; kwani mtoto au mtu yeyote kuwatembelea jamaa zake wawe wa upande wowote ule ni katika jambo la wajibu na huko ndio kuunga na kuimarisha udugu/ujamaa. Na kumkataza au kumzuilia huyo mtoto kutekeleza jambo hilo ni lililo wajibu ni haramu, Allaah Anasema:

Mcheni Allaah mnayemtaka msaada kwa kila mnachokihitajia, na kwa jina Lake ndio mnaombana nyinyi kwa nyinyi katika mambo yenu. Pia tahadharini na kuacha kuwasaidia jamaa zenu, wa karibu na wa mbali –kuukata udugu-…” An-Nisaa: 1.

 

Hivyo wewe na huyo mumeo munahitaji muelewe haya na mujaribu kadiri ya uwezo wenu bila ya kuvutana wala kugombana kuwaelewesha wengine ili wasiingie katika makosa kwa kukataza jambo lilioamrishwa na Uislamu; na huko ndio kutafuta radhi za wazee wenu kwani mutakuwa mumewasaidia kuachana na yaliyokatazwa na Uislamu na kuwapelekea kutekeleza yaliyohimizwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyothibiti katika Hadiyth aliyoulizwa Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam kuhusu kitu kitachomuingiza mtu peponi, alijibu kwa kusema:

“Haingii peponi mwenye kukata udugu” Imepokelewa na Al-Bukhaariy. Kitabu cha Aadabu, mlango dhambi za asiyeunga udugu.

Ama maamuzi yako ya kwenda kuishi na mwanao, hayo ni maamuzi ya busara, na ni jambo linalohitajika haswa wazazi kuishi na mwana wao kwani kunaimarisha mapenzi, kujenge mahusiano ya karibu, malezi kuwa mepesi na kufuatilia nyendo zake kwa karibu. Na haipendezi kukaa mbali na mtoto wenu kwa sababu tu ya maslahi ya kidunia, bila dharura zozote zile za msingi.

Bonyeza kiungo kiufatacho upate manufaa zaidi:

 

Kukata Undugu

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share