Anaweza Kuolewa Iikiwa Talaka Ya Kwanza Ni Moja Na Ya Pili Ni Talaka Mbili?

SWALI:

Assalamaleikum,

SWALI LA KWANZA:

Tafadhalini naomba munipe majibu ya suali langu lifuatalo:

Mtoto wangu ameachika kwa muda wa miaka miwili tu tokea alipoolewa.

- Talaka ya kwanza alipewa kwa maandishi, tulikutana tukasawazisha akarejewa

- Mara ya pili aliachwa tena kipindi kifupi baada ya kurejewa  kwa maelezo   yalioandikwa) kwamba ameachwa talaka mbili.

Amekaa mpaka akajifungua na kumaliza eda. Muume anaomba kumuoa tena mtaliki wake. Mimi nilifaham kwamba, kwa talaka ya kwanza ukijumlisha na talaka mbili za mara ya pili inatimiza talaka tatu alizo kusudia. Nimesikia kwamba masheikh wanasema kwamba aweza kumuoa tena. Naomba nijuilishwe ni kweli kwamba anaweza kumuoa tena kama jibu ni ndio jee zitabakia talaka ngapi? Naomba munisaidie ili nitoe uamuzi, natanguliza shukran

SWALI LA PILI:

Assalam aleikum:

Suali langu ni kwamba, mtoto wangu aliachika kwa (talaka moja) mara ya kwanza miaka miwili tu baada ya kuolewa.  Akarejeewa, tena baada ya muda mfupi aliachwa tena, mara hii aliachwa kwa maandishi yanayo someka; "Fulani bint fulani, nimekuacha talaka mbili"

Tumekaa mpaka kipindi cha eda (baada mke kujifungua) kimemalizika, muume amekuja na ombi lakutaka kumuoa tena mtaliki wake, na masheikh wanasema anaweza kumuoa ila sisi familia tunavyo fikiria ni kwamba kwa talaka ya kwanza jumlisha na mbili pamoja zimetimia talaka tatu hivo nibudi mtoto aolewe na mtu mwengine  akiachika ndio na mtaliki wake wa kwanza ataweza kumuowa tena.

 

Tunaomba kujua jee  1. Ni kweli kwamba mtoto wetu anaweza kuolewa hivi hivi?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu talaka na kurejewa kwa binti na mumewe. Inaonyesha kuwa maswali haya ni mawili lakini yanafafana kikamilifu. Hivyo jibu letu litakuwa ni moja tu. Mwanzo tunataka kumuelewesha ndugu yetu muuliza swali kuwa talaka hata zikitolewa ngapi, mfano mbili kama katika swali lako au elfu moja kwa kikao kimoja talaka hiyo inahesabiwa ni moja. Hatuna haja ya kwenda kwa kina katika suala hilo kwani tayari katika swali la talaka tulilieleza kwa mapana na marefu. Unaweza kwenda kwenye tovuti ya alhidaaya kuona hilo. Hata hivyo inafaa tufahamu kufanya hivyo ni uzushi na mwenye kufanya ni lazima atubie na arudi kwa Allaah Aliyetukuka kuomba msamaha na kutorudia tena kosa hilo.

Kwa hiyo, inabidi mumpe nasaha mume wa binti yenu asiwe ni mwenye kurudia kosa hilo tena kwa yoyote. Na pia ni vyema mumtanabahishe kuwa akitoa sasa talaka baada ya kumrudia atakuwa hawezi tena kumrudia mkewe huyo hata akitaka namna gani mpaka aolewe na mume mwingine, wafanye tendo la ndoa, aachwe ndio aweze kumrudia na hiyo ni bahati nasibu. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Talaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlicho wapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Allaah” (2: 229).

Na tena,

Na kama amempa talaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Allaah” (2: 230).

Kwa muhtasari ni kuwa hao wawili wanaweza kurudiana kisheria bila pingamizi lolote.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share