Mke Mdogo Anadai Talaka Kwa Kutoa Madai Kadhaa Na Kushawishiwa Na Familia Yake Nami Sitaki Kumuacha

 

 SWALI:

 

Assalaam alaykum. amshukuru ALLAH subhana hu wataala na washukuruni pia nyie kwa kutupa faida mbalimbali kupitia jarida hili, nakuombeeni kwa ALLAH awape moyo zaidi na hili, amin.

 

Nina maswali yafuatayo naomba ufafanuzi wake:  Mke wangu mdogo ananidai talaka eti kwasababu tangu nimuoe hajapata mtoto, nami sitaki kumuacha kwasababu sijamfanyia ubaya wowote tangu nimuoe, ila ktk utfiti wangu nimegundua kuwa kuna mwanamme anamshawishi nimwache ili amuoe yeye kwa madai kuwa mimi nina mathna hivyo hafaidi raha ya ndoa nae amekubali.

 

1. Je ikiwa sikumwacha mimi nitakuwa na makosa mbele ya ALLAH?

 

2. je huyo anaemshawishi aachike anahaki kufanya hivyo na kama hana nini hukumu yake kwa ALLAH.

 

3. Mke wangu kwa kunidai talaka kwa sababu hiyo anahaki kufanya hivyo? na kama hana nini hukumu yake?

 

4. Baadhi ya ndugu zake ambao wanamsapoti wanasema endapo sitompa talaka wataenda kwa wenye majukumu ya Kiislamu kudai talaka je wakipewa talaka itaswihi?

 

5. Baadhi ya ndugu zake wananisihi nisimpe talaka kwa kuwa amerubuniwa tu na endapo nikiwasikiliza je ikitokea ndugu kwa ndugu wakifarakana mimi sitokuwa na hatia kisheria? Naomba majibu ikiwezakana na ushahidi wa aya au hadithi.

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kwa maswali yako kuhusiana na talaka.

 

Mwanzo tunataka kukufahamisha kuwa wewe uko katika sawa kutotoa talaka hiyo kwani sababu zinatotakiwa si za kisheria hasa ikiwa wewe unataka kukaa na mkeo hata kama hazai. Na inatakiwa uzungumze naye kwa njia ya kumuelimisha kuwa mas-ala ya mtu kuzaa au kutozaa ni ya Allaah Aliyetukuka kwani Yeye Amesema: “Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Allaah; Anaumba Apendavyo, Anamtunukia Amtakaye watoto wa kike, na Anamtunukia Amtakaye watoto wa kiume. Au Huwachanganya wanaume na wanawake, na Akamfanya Amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza” (42: 49 – 50).

 

Mwenye kumshawishi kufanya hivyo hana haki bali ana dhambi kubwa la kufanya dhulma na Allaah Aliyetukuka Ameharamisha dhulma kwenye nafsi Yake na akaifanya ni haramu baina ya waja (Muslim). Na mwenye kudhulumu atakuwa kwenye viza Kesho Akhera kumaanisha hatopata rahma ya Allaah Aliyetukuka.

 

Mke wako pia hana haki ya kukudai talaka. Yeye ana haki ya kukudai ikiwa una makosa katika utendaji wa Dini yako, humtekelezei mahitaji yake ya msingi na mfano wa mambo kama hayo. Na mwanamke anayedai talaka bila ya sababu yoyote basi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni haramu kwake kupata harufu ya Pepo” (Ahmad, Ibn Maajah na ad-Daarimiy).

 

Usitoe talaka waache ndugu zake waende kushitaki kwa wenye majukumu ya Waislamu. Ikiwa watapitisha talaka, talaka hiyo itakuwa haikupita isipokuwa tu wakikupata na makosa ambayo Qadhi ana haki ya kupitisha talaka hiyo baada ya kusikiliza pande zote mbili.

 

Inatakiwa uungane na ndugu ambao wanamtakia dada yao mema kwa kubakia na mkeo. Ikitokea kuwa ndugu wameteta kwa ajili ya haki wewe hutakuwa na makosa mbele ya Allaah Aliyetukuka. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na saidianeni katika wema na uchaji Mungu wala msisaidiane katika madhambi na uadui. Na mcheni Allaah” (al-Maa’idah [5]: 2).

 

Nasaha ambayo tunaweza kukupa ni kuwa jaribu kumpata shaykh mwenye elimu na mtoa ushauri nasaha azungumze na mkeo na kumnasihi aache jambo hilo la kutaka talaka kwa njia nzuri nay a hekima.

 

Na Insha’Allaah Allaah Aliyetukuka Atakuwa nawe katika kuipata na kuitetea haki yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share