Mashairi: Allaah Hana Mshirika

Allaah Hana Mshirika

'Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)
 

Alhidaaya.com

 

 (1)  Salaam zangu natuma, ziwafike Afrika,
        Allaah Awape hekima, mzidi kuneemeka,
        naomba Zake rehema, zivuke zote mipaka,
        Allaah Hana mshirika, Hana mwana wala mama.

 (2)  Hana mwana wala mama, Allaah Hana mshirika,
        Hana mke Amesema, Hana baba wala kaka,
        Tokea zama za zama, pekee Ametajika,
        Allaah Hana mshirika, Hana mwana wala mama.

 (3)  Kaunda ardhi na mbingu, peke Yake Msifika,
        Kawaumba binadamu, iblisi na malaika,
        Tupate kumuabudu, ibada Anavyotaka,
        Allaah Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (4)  Kutoka kwenye mchanga, binadamu kaumbika,
       atarudia mchanga, mauti yakimfika,
       atoke kwenye mchanga, wakati wa kufufuka,
       Allaah Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (5) Kamuumba iblisi, kwenye moto unawaka,
       na hapo atajilisi, motoni atachomeka,
       adui wetu halisi, lazima kumuepuka,
       Allaah Hana Mshirika, Hana mwana wala mama.

 (6) Malaika kwenye nuru, Amewaumba Rabuka,
       maisha hawakufuru, ibada wameishika,
       Allaah Anavyoamuru, upesi wanaridhika,
       Allaah Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (7)  Riziki ipo mbinguni, huko ndiko inatoka,
       ipo Mwake mikononi, tena imeshagawika,
       tuwe tuna shukurani, bila ya kulalamika,
       Allaah Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (8)  Yupo macho Maulana, hukuti Akizeeka,
        kila kitu Anaona, yote yanayotendeka,
        hakuna ya kufichana, Kwake vinaeleweka
        Allaah Hana Mshirika, Hana mwana wala mama

 (9)  Yupo karibu na sisi, dua Kwake zinafika,
        ili zifike upesi, tuzidi Kumkumbuka,
        tuache yote maasi, tuyaache kwa haraka,
        Allaah Hana Mshirika, Hana mwana wala mama.

(10)  Allaah Atupe uzima, hapa mwisho kuandika,
        Atupe nguvu na hima, radhi Zake tunataka,
        Atupe nzuri hatima, dhambi zipate futika,

Allaah Hana Mshirika, Hana mwana wala mama.
 

 

Share