Mashairi: Uwahabi

 

Uwahabi

 

                 ‘Abdallah Bin Eifan

                    (Jeddah, Saudi Arabia)

 

 

 

Salaamu zangu natuma, zifike kwa ikhwani,

Uwahabi umevuma, kila pembe duniani,

Wengi wameusakama, bila ya kutamakani,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Lazima tuuelewe, Uwahabi ndio nini,

Lazima tufafanuwe, na tutoke mashakani,

Tujitahidi wenyewe, tusome tuulizeni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Uwahabi si dhehebu, au nguzo kwenye dini,

Kwa hivyo usiwe bubu, uliza wanazuoni,

Wabishao tuwajibu, kwa dalili vitabuni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Mashia walovumisha, kwa nia mbaya rohoni,

Na dini yetu kuitwisha, jina hili lilo geni,

Wapate kubabaisha, kuingiza yao dini,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Uwahabi neno hili, halipo lichunguzeni,

Huwachezea akili, wasosoma masikini,

Ona kwa mwenye akili, Mshia hupiga chini,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Huchukia Maswahaba, vipenzi vya Rahmani,

Wale walo na nasaba, na Mtume wa imani,

Abubakar ndio baba, wa mama wa Waumini,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Mashia wanamsema, kwa chuki na ukhaini,

Wenyewe Shia tazama, wanavyofanya mwilini,

Hujipiga kwa vyuma, kama vile majnuni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Wameifanya sababu, ya kuwatukana Sunni,

Nia yao kuharibu, aqida yetu moyoni,

Wanatunga na vitabu, uongo tupu someni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Wanawadanganya watu, kwa pesa kila makani,

Khasa wasio na kitu, wale watu masikini,

Huwanunulia vitu, kama vile maskani,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

        

Pia walitupoteza, Masufi misikitini,

Mengi waliyaongeza, ni mapya katika dini,

Kaja Shekhe kaongoza, mema kawaonyesheni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Masufi wanatutaka, tuwabusu mikononi,

Eti wao ni baraka, wanajua ya mbinguni,

Majahili kwa hakika, washirikina yakini,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Wanajifanya wajuzi, Masufi angalieni,

Watufanyia hirizi, eti kinga ardhini,

Mambo yao ya upuuzi, wanaeneza nchini,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

          Abdul Wahabi ni jina, la Shekhe wa Arabuni,

Amefuatilia sunna, na dini ya Rahmani,

Ametuongoza sana, katutoa ujingani,

Maana ya Uwahabi, wengi hawaelewi.

 

 

 

Katuonyesha ukweli, na kututoa kizani,

Tulikua majahili, kama watu wa zamani,

Katuchezea akili, adui wetu shetani,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Katufundisha mazuri, Shekhe mengi kabaini,

Kama vile makaburi, kuomba walo shimoni,

Jambo hilo sio zuri, Kumshiriki Manani,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Macho ametufumbua, njia ya haki fuateni,

Mengi hatukuyajua, tulikuwa hatarini,

Shekhe katuzindua, amesema amkeni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Bida'ah kapinga sana, kayatia maanani,

Sheikh huyo akanena, mambo hayo yaacheni,

Ghadhabu za Maulana, zitawafika mwishoni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Kama vile Maulidi, katika dini ni geni,

Hujikusanya makundi, na kusoma hadharani,

Sheikh huyo alinadi, hili kosa tazameni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Na pia kusoma khitma, kwa kusoma Qur-aani,

Sheikh nae alisema, hayafiki kaburini,

Ukweli aliosema, tumeona vitabuni,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

  

Dini imekamilika, nyongeza faida gani,

Hadithi zilotajika, sahihi ndio someni,

Tupate kuelimika, tusome na Qur-aani,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Hawa wameshapotea, na haki hawaioni,

Kila nchi hutembea, wana pesa mfukoni,

Siasa huingilia, hujifanya wahisani,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Sumu yao kali sana, wajanja hawa jamani,

Si usiku si mchana, utawakuta njiani,

Lengo lao ni vijana, kuwateka akilini,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

Nimesema vya kutosha, ndugu zangu kwaherini,

Shekhe ametuonyesha, ukweli umebaini,

Mabaya kayasafisha, Mungu Amweke peponi,

Maana ya Uwahabi, wengi hawauelewi.

 

 

 

 

 

Share