Zingatio: Ahadi Isiyotimizika

 

Zingatio: Ahadi Isiyotimizika

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Mwanaadamu ni mwenye kuhitajia hata vitu vyenye hatari ndani ya maisha yake na vyenye kuleta matatizo chungu nzima. Kwa mfano maradhi ni lazima yawepo kwa mwanaadamu, kwani pamoja na kuwa ni mitihani Aliyowekewa na Muumba, vilevile ni jambo la kumsaidia kumfutia madhambi yake madogo madogo, na pia kutokana nayo atavumbua dawa. Kuna dalili za vifo ambazo tunaamini zinachangia kwa namna moja au nyengine, mfano ajali. Hivyo, atajikinga na ajali ili kuokoa maisha yake.

 

Na namna hiyo, Muislamu pia anahitaji ushiriki wa washirikina kwa namna ambayo wao wanatuhitajia sisi pia. Kaa ufikirie yareti dunia ingelikuwa yote ni yenye Waislamu wenye imani madhubuti, wapi tungelitoa da’wah? Hata haya maandishi unayosoma sasa yasingekuwepo. Bila ya shaka kusingekuwa na ushindani wala harakati zenye manufaa.

 

Ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akatuumbia mitihani ya kila namna. Kutokana nayo tujiepushe na tujifunze tusiteleze kwayo. Ndani ya mitihani hii ndimo kunapatikana haja ya Muislamu kuwa karibu na Rabb Mlezi. Na hakuna mtihani mkubwa alioumbiwa mwanaadamu zaidi ya Shaytwaanur Rajiym.

 

Kiumbe Shaytwaan kila mmoja anaye ndani ya nafsi yake. Wapo Waislamu wanaoathirika naye mno kiumbe hichi kupita mpaka. Hufanywa kuwa ni pumba kwa kupelekeshwa kwenye maovu makubwa makubwa. Utashangaa mno kumkutia Muislamu ni mwenye kulewa, kuzini au kuiba jicho kupe kupe bila ya woga kabisa! Huyo ameathirika kutokana na laghai za Shaytwaan.

 

Urafiki baina ya Shaytwaan na mwanaadamu hudumu kutokana na kiwango cha madhambi anachotenda Muislamu. Pale tu atakaporudi kwa Rabb wake kidhati kabisa, ataikuta himaya (ulinzi) wa Rabb Mlezi ukiwa upo tayari kumpokea kwa furaha na hamu ya hali ya juu.

 

Ni urafiki baina ya Muislamu na Rabb wake ndio huzaa matunda na humpatia utetezi bora kabisa mbele ya Siku ya Hisabu. Urafiki mwengine wowote huzaa uadui tu. Na ni hasara iliyoje kwa mwanaadamu kufuata mkumbo bila ya kuangalia khatima yake. Wale vibaraka vya wakubwa na wanafiki wa kugeuza Aayah za Rabb kwa manufaa yao binafsi watakiona cha mtema kuni Siku Hiyo: 

وَبَرَزُوا لِلَّـهِ جَمِيعًا فَقَالَ الضُّعَفَاءُ لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا كُنَّا لَكُمْ تَبَعًا فَهَلْ أَنتُم مُّغْنُونَ عَنَّا مِنْ عَذَابِ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ ۚ قَالُوا لَوْ هَدَانَا اللَّـهُ لَهَدَيْنَاكُمْ ۖ سَوَاءٌ عَلَيْنَا أَجَزِعْنَا أَمْ صَبَرْنَا مَا لَنَا مِن مَّحِيصٍ ﴿٢١﴾

Na watahudhuria wote mbele ya Allaah, wanyonge watawaambia wale waliotakabari: Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu (tukikutiini). Basi je, nyinyi mtaweza kutuondolea chochote katika adhabu ya Allaah? Watasema: Kama Allaah Angetuhidi, bila shaka tungelikuongozeni. Ni sawasawa kwetu; tukipapatika au tukisubiri, hatuna mahali pa kukimbilia. [Ibraahiym: 21]

 

Kwa wale waliomfanya Shaytwaan kuwa ni rafiki wa dhati ndani ya nafsi zao. Wakaacha kufuata amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hadi kutenda maasiyah ya kila namna, hawatamkuta Shaytwaan kuwa ni mtetezi wao kama alivyowarubuni duniani kwa ahadi kemkem. Bali watamruka na hata akihitaji kumpatia msaada wowote, atashindwa tu: 

وَقَالَ الشَّيْطَانُ لَمَّا قُضِيَ الْأَمْرُ إِنَّ اللَّـهَ وَعَدَكُمْ وَعْدَ الْحَقِّ وَوَعَدتُّكُمْ فَأَخْلَفْتُكُمْ ۖ وَمَا كَانَ لِيَ عَلَيْكُم مِّن سُلْطَانٍ إِلَّا أَن دَعَوْتُكُمْ فَاسْتَجَبْتُمْ لِي ۖ فَلَا تَلُومُونِي وَلُومُوا أَنفُسَكُم ۖ مَّا أَنَا بِمُصْرِخِكُمْ وَمَا أَنتُم بِمُصْرِخِيَّ ۖ إِنِّي كَفَرْتُ بِمَا أَشْرَكْتُمُونِ مِن قَبْلُ ۗ إِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na shaytwaan atasema itakapokidhiwa jambo: Hakika Allaah Alikuahidini ahadi ya haki (na Ameitimiza); nami nilikuahidini kisha nikakukhalifuni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu isipokuwa nilikuiteni mkaniitikia. Basi msinilaumu, bali laumuni nafsi zenu. Mimi siwezi kukusaidieni kukuokeeni wala nyinyi hamuwezi kunisaidia kuniokoa. Hakika mimi nilikanusha yale mliyonishirikisha zamani. Hakika madhalimu watapa adhabu iumizayo. [Ibraahiym: 22]

 

Hiyo ndio hali ya walioathirika na vitimbi vya Shaytwaan watakavyokuwa Siku ya Hisabu. Shaytwaan si rafiki wa kuwa naye hata kidogo! Hawezi kutupatia ahadi yoyote ya kutusaidia Siku ya Hisabu. Yeye mwenyewe atakuwa mashakani. Tujiepushe naye kwa kila hali. Tuwe macho na vitimbi vyake na tuwe tayari kupigana naye kwa kujiweka karibu na himaya ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Himaya ambayo itapatikana tu kwa kutomshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) pamoja na kutenda matendo mema.

 

Share