Zingatio: Ulimi Ndio Chanzo

 

Zingatio: Ulimi Ndio Chanzo

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Kawaida ya daktari ni kutibu wagonjwa wakati fundi wa computer ni kutengeneza computer. Iwapo mmoja wao atavamia nyanja ya mwenziwe hatoweza kuona ndani na ghafla anaweza kuharibu kila kitu.

 

Chukulia mfano wa fundi aliyeingia ndani ya chumba cha operation, au daktari aliyefungua computer; wote hawatojua kinachoendelea. Hivyo kila mmoja ana nyanja yake maalum na yampasa aitumie kwa maadili mazuri na kuiheshimu.

 

Ndivyo ilivyo kwa mwanaadamu juu ya viungo vyake vya mwili. Kila kiungo kina kazi yake maalum na yamlazimu kuvitumia kwa uadilifu. Aangalie Muislam namna ulimi unavyofanya kazi. Ni kiungo kisichohitaji kupatiwa petroli au dizeli ili kipate kufanya kazi wala si kiungo kinachotaka malipo ya alfu za dola kila mwezi. Kiungo ambacho maskini amepatiwa na tajiri hali kadhalika.

 

Basi na atupe jicho lakeMuislam kwa kiungo hicho ambacho ni chenye sifa ya kipekee. Sifa ambayo mwanaadamu anapoikosa hutafutiwa jina jengine na kupachikwa nalo: 'bubu'. Basi elewa ya kwamba una masuala mengi ya kujibu mbele ya Muumba juu ya neema hii kubwa uliyopatiwa.

 

Ulimi ndio utangulizi na muhtasari wa kila ovu. Zinaa inaanzia hapo na biashara za haramu zatangulizwa hapo. Unapokosa kudhibitiwa ulimi, ndio hutokezea mifarakano baina ya watu; rangi nyeupe ikafanywa nyeusi, dari likageuzwa sakafu na Muumini akavurumishiwa ukafiri. Hiyo yote ni kazi ya ulimi tu! Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَتَصِفُ أَلْسِنَتُهُمُ الْكَذِبَ

"… na ndimi zao zinaeleza uongo …" [An-Nahl: 62].

 

Tuyakumbuke maneno ya Imaam An-Nawawy aliposema:

 

"Mjuwe kuwa mtu hapaswi kuzungumza isipokuwa lile lenye manufaa...Badala ya kujilazimisha kuzungumza yenye faida, Waislam wa leo tumekuwa ni wepesi wa kusema uongo. Na hakuna msaada anaopatiwa Muislam kusema uongo kama simu za mkononi (mobile).

 

'Nipo karibu nakuja'subiri dakika tano tu' 'nipo hapa mtaa wa….' Ukitanabahi ni muda wa saa umepita nduguyo bado hajafika. Huo muda unaoahidiwa mara nyengine wavuka masafa ya kutoka Marekani kwenda Afrika Kusini, tena bila ya hata kuambiwa 'cancelled'. Maana utamsubiri hadi itaingia jioni, uende zako na kesho yake asitokee. Afadhali ya ndege utaandikiwa 'cancelled'.

 

Waislam tunalichukulia jambo hili ni la masikhara mno na dhihaka ya hali ya juu. Kila sekunde na kila neno linawekwa ndani ya kitabu ambacho tutapatiwa Siku ya Hisabu. Je umewahi kufikiria hilo? Siku ambayo utapatiwa kitabu kilichojaa maongezi ya simu yaliyokuwa ya uongo mtupu! Kumbuka ya kwamba Allaah Analipa kila kheri au shari ifanywayo duniani:

 

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾

Siku zitakaposhuhudia dhidi yao ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [An-Nuwr: 24].

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Uchafu wa ndimi zao wasababisha watupwe Motoni kifudifudi…"

 

Ni lazima kwa Waislam, iwapo wanataka usalama mbele ya Muumba, waudhibiti ulimi. Kwani huo ndio msingi wa tabia njema.

 

Ulimi ndio chanzo, wengi Waislam wamefarikiana.

Ndimi zimejaa uozo, hadi ndugu kukhasimiana.

Simu zinaleta mzozo, uongo humo umejazana.

Uchunge ulimi wako, Allaah Akupatie hifadhi.

 

Badili yako mawazo, kumkumbuka wako Rabana.

Mukhofu Mwenye uwezo, Akinena kun fayakuuna.

Wewe sie mwanzo, utakufa shaka hapana.

Uchunge ulimi wako, Allaah Akupatie hifadhi.

 

Ulimi waleta maangamizo, duniani zahma zimejazana.

Yakamate yale mafunzo, aliyotuachia Nabiy al-amiyna.

Hakufanya uongo gumzo, uzushi hakupatapo kunena.

Uchunge ulimi wako, Allaah Akupatie hifadhi.

 

 

Share