Zingatio: Neema Za Allaah Hazihesabiki

 

Zingatio:  Neema Za Allaah Hazihesabiki

 

Naaswir Haamid 

 

Alhidaaya.com

 

 

Rabb wetu Mtukufu Amemuumba mwanaadamu katika umbo bora lisilomithilika na kiumbe chochote. Naye ameumbwa kwa kutumia udongo uliopulizwa roho itokayo kwa Rabb Mtukufu.

 

Akamjaalia mwanaadamu ni mwenye kupata shida, mitihani, mtenda dhambi na mwenye kupata maradhi. Hakusita hapo Rabb wetu Mtukufu, bali Akajaalia mlango wa pili wa kutokea kwenye mashaka ya dunia; Akajaalia kuwepo starehe, utulivu, toba na afya. Basi ni kwa neema zipi mwanaadamu anaweza kumlipa Rabb wake!?

 

Tutambue kwamba hii roho tuliyokuwa nayo yatosha kuwa ni sababu ya kushukuru neema za Rabb Mtukufu kwa vitendo na kauli. Tusisahau wapi tulipotoka na wapi tunaelekea, hatukuwa chochote miaka 100 iliyopita. Basi ni nani kati yetu alikuwa na uhakika kwamba atadhihiri duniani kwa jina na umbo lake kabla ya kuzaliwa? Kuwa na adabu kwa kumcha Rabb wako!

 

Muislamu yupo juu ya mgongo wa ardhi akiruzukiwa kila chenye manufaa na yeye, ni mwenye kula akapata njia ya kutolea uchafu, na siku uchafu unaposhindwa kutoka ndani ya tumbo ndio unaelewa umuhimu wa neema ya kuyeyusha chakula kwenye mwili. Ameumba kila kitu kwenye kiwango maalumu, kwani tumbo likiyeyusha kupita kiwango, mwanaadamu ataugua maradhi ya tumbo la kumuendesha. Hivyo, kumbuka na yazingatie maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٨﴾

Na mkihesabu neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika Allaah bila shaka ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [An-Nahl: 18]

 

Basi elewa ndugu yangu, kwamba sisi si chochote si lolote zaidi ya tone la manii lililoengwa engwa hadi likafikia miezi tisa likaweza kutoka kwa sura ya mwanaadamu. Ndani ya tumbo, Rabb wetu Mlezi Alitulinda na wala hatukuhitaji askari, jeshi, polisi, ultimate security au mwengineye. Ukatoka kwa ukenya wa kilio cha juu ukiomba msaada kwa mama yako. Ukafikia baleghe ukaweza kuoa/kuolewa na sasa kwa Qadar ya Rabb unaweza nawe kupata mtoto. Aliyekuwa mbabe kati yetu azihesabu neema ngapi zimepita baina ya kuzaliwa kwake hadi hivi sasa, kisha aangalie ni kwa kiwango gani ataweza kuzishukuru neema hizo. SubhaanaLlaah! Yuko umbali gani mwanaadamu kwa kuzitilia maanani neema za Rabb wake?

 

Ugeuze uso wako, uangalie mbingu ilivyotanda na ardhi ilivyotandikwa, kisha useme kwamba Rabb wako amekutupa. Rizki zako Akazimimina kutoka mbinguni na Akazichimbua kutoka ardhini. Ni kipi basi katika chakula chako kitokacho nje ya mfumo huu? Basi kwa Kiburi Chake Rabb Mlezi Anastahiki kuyaambia makundi ya wanaadamu na majini:

 

يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ إِنِ اسْتَطَعْتُمْ أَن تَنفُذُوا مِنْ أَقْطَارِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ فَانفُذُوا ۚ لَا تَنفُذُونَ إِلَّا بِسُلْطَانٍ ﴿٣٣﴾

Enyi jamii ya majini na watu! Mkiweza kupenya kwenye zoni za mbingu na ardhi, basi penyeni. Hamtoweza kupenya isipokuwa kwa mamlaka (ya Allaah). [Ar-Rahmaan: 33]

 

Tumcheni Rabb wetu kwa kila kitu, kwa dogo na kubwa, kwa tunayoyajua na tusiyoyajua. Tutende mema kabla ya kutufika yale yasiyoweza kuhimili miili yetu. Wahenga wanatuambia: "Kijua ndi hichi usipouanika utaula mbichi."

 

Share