Mwanamke Ana Haki Kuomba Talaka Ikiwa Haridhiki Na Mumewe?

 

Mwanamke Ana Haki Kuomba Talaka Ikiwa Haridhiki Na Mumewe?

 

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

 SWALI:

 

Assalaamu Alaykum. Swali langu ni kwamba mwanamke anaye muomba talaka mumewe kwa sababu haridhiki na mumewe kitandani, je mume huyo ana haki ya kutoa talaka kwa mkewe. Wameishi miaka kumi pamoja na wana watoto wawili bado wadogo chini ya umri wa miaka kumi.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mwanzo kabisa tungependa kukuuliza kuhusu mahusiano yako na mumeo hapo awali baada ya kuoana? Je, alikuwa sawa kitandani? Hili tatizo ilianza lini?

 

Ikiwa mlipoana mlikuwa sawa na tatizo hilo lilianza karibu basi huenda akaweza kusaidika kwani zipo dawa kwa ugonjwa huo. Huo ni ugonjwa na itabidi kabla ya kuchukua hatua ya kutaka akuache basi zungumza na mumeo kwa njia nzuri kuhusu hilo. Kwa kuzungumza hivyo ndio mnaweza kupata ufumbuzi mzuri kwenu nyote. Wapo madaktari na matabibu ambao wanaweza kuwasaidia katika hilo. Ikiwa atakubali basi itakuwa kheri nasi twawaombea mafanikio mema.

 

Ikiwa atakataa basi itabidi uende kwa Qaadhi umuelezee kuhusu shida yako hiyo, na lau sehemu hakuna Qaadhi basi utakwenda kwa Shaykh aliyekuoza au Shaykh mwengine muaminifu na muadilifu ili asikilize kesi yenu. Mume kutoweza kumtimizia mkewe starehe ya kitandani ni sababu ya mke kuomba talaka. Mara nyingi mume hatotaka kutoa talaka itabidi wewe kutodhurika ukashtaki kwa Qaadhi ili upate haki yako.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awasuluhishie tatizo lenu hilo na Awapatie tawfiki.

 

Tunapata kujua kuwa hilo lawezekana kisheria na mke atapaswa amrejeshee mumewe mahari yake, kama tunavyoona katika  kisa cha mke wa Thaabit bin Qays aliyekwenda kushtaki kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya mumewe, pamoja na kuwa mumewe hakuwa na tatizo la dini wala tabia bali yeye hakumpenda na akawa anakhofia kutotekeleza wajibu wake kama mke. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  aliwatenganisha lakini kwa kumtaka mke airejeshe shamba aliyokuwa amepewa na mumewe kama ni mahari. Hadiyth ni kama ifuatavyo:

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa)  amehadithia kwamba: Mke wa Thaabit bin Qays alimfuata Rasuli  wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema: Ee Rasuli wa Allaah,  Thaabit bin Qays simlaumu katika tabia wala Dini, lakini mimi nakhofia ukafiri katika Uislamu (kutokutekeleza haki zake). Basi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)   akasema: “Utamrejeshea shamba lake?” Akasema: Ndio. Akasema kumwambia Qays: “Kubali shamba na umtaliki.” [Al-Bukhaariy (5273)].

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share