Mume Amenikasirikia Kupanda Gari La Mtu Hataki Nirudi Nyumbani Anataka Talaka, Je Ni Haki?

SWALI:

 

Asalaam alaykum

 

Mume wangu kanikuta nikiwa ndani a gari la mtu binafsi na ikiwa hilo gari ndilo linalotumika kutupeleka mida ya usiku kituoni ili kutuepusha na vibaka wa usiku, namuita mume wangu nimtambulishe yule ni nani lakini hakutaka na kunitolea matusi na maneno makali, nikapaki gari pembeni ili nimfate kwenda kumuita akakataa na kupanda ndani ya gari na kuondoka, na kunambia nisirudi nyumbani ataniua, na anatafuta mashehe tuachane je hii ni haki na kwa nini adhani hivo?

 

Wabillah toufiq


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kukutwa na mumeo ukiwa ndani ya gari. Hakika haya ni matatizo yanayopatikana katika jamii yetu duniani.

 

Kwanza dada yetu lazima ufahamu kuwa hairuhusiwi mwanamke kupanda gari la mwanaume asiyekuwa Maharimu wako. Vilevile faragha yoyote ili baina ya mwanamke na mwanaume hairuhusiwi kabisa katika dini. Soma makala hapa chini kwa maelezo ya kutosha kuhusu ubaya wa jambo hilo:

 

Ikhtilaatw (Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake)

 

Na hilo ndilo linaloweza kuwa limemuudhi sana mumeo na kufanya maamuzi makali kama hayo. Huenda pia maamuzi yake hayo mazito na makali, yamesababishwa na kutokuwa na kuaminiana baina yenu.

 

Katika hali ya dharura unaweza kuruhusiwa kubebwa kwenye gari la dereva ambaye si Maharimu wako, kama vile gari la kazini n.k.

 

Na katika hali kama hiyo ulipaswa uwe ushamjulisha mumeo jambo hilo ili awe anajua kinachoendelea. Na kutojulishana kuanzia mwanzo kuhusu shughuli zako na kazi ya kila mmoja kati yenu ktaweza kusababisha matatizo kama yaliyokutokea.

 

Ikiwa ulimueleza kuwa katika kazi unayofanya usiku inabidi upelekwe kituoni na gari ya kazini dereva akiwa ni mwanamme naye akakubali baada ya kumwambia ukweli basi atakuwa ana makosa mumeo kufanya aliyofanya. Ama ikiwa hukumfahamisha hilo, wewe utakuwa na makosa mbali na kuwa mumeo pia naye atakuwa na makosa yake.

 

Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana mtu kutokasirika haraka. Na pale alipojiwa na mtu akitaka nasaha alimwambia asikasirike. Hivyo pia akatupatia (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) dawa kwa mtu anapokasirika abadilishe mkao wake, akiwa amesimama akae, akiwa amekaa ajinyooshe, au aende akachukie wudhuu au abadilishe mazingira yake kwa kutoa nyumbani na kadhalika.

 

Ama kukutisha kuwa atakuua pia si katika maadili ya Kiislamu, hivyo inakupasa wewe uwapigie watu wa nyumbani kwako na kwao kuhusu tukio hilo ili mpate kusuluhisha suala hilo kwa njia nzuri zaidi. Ikiwa hukufanikiwa katika hilo inabidi uende kwa Qaadhi akiwepo katika maeneo hayo ili umshitakie kuhusu hayo. Wala usilichukulie suala hilo kijuu juu kwani maafa huenda yakawa makubwa.

 

Kwa kuwa umbali nasi hatuna budi kukuelekeza kwa walio karibu nawe ili wapate kusuluhisha tatizo hilo. Sababu ni kuwa sisi tunaweza kukupa nasaha tu wala hatuwezi kutoa uamuzi kwa kuwa tuko mbali nawe na tumesikia kutoka upande wako tu na hatujasikia kutoka kwa mwenzio.

 

Tunakutakia mafanikio mema na kheri katika mazungumzo yakiwepo ya kutafuta suluhisho.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share