Mume Anapenda Sana Muziki Anafaa Kuomba Talaka?

 

SWALI:

asalam alaikum warahmatullahi wabarakat

 

swali langu enyi maamiri wa kiislam mimi nina mume wangu anapenda sana muziki upo ndani ya moyo wake nimejaribu kusema nae kwa wema nimeshindwa akiingia ndani ya gari ni mziki barabara yote wanamshangaa na mimi ni mtu najulikana na watu wa jamii yangu ni mtu ninapingana na mila za kiyahudi na kinaswara ee amiri wa waislam mimi nataka kudai talaka yangu je ntakuwa nipo sawa kisheria sintojali watoto wataishije wala sijali ntaishi wapi kwani anapowasha muziki mimi roho yangu inaungua na yeye anafanya makusudi hata nikipanda ndani ya gari anafungulia hata hasemi mke wangu hapendi ngoja nizime na mimi nilikuwa mpenzi wa muziki ila nimeacha sababu ya kujua hasara ya muziki nipeni jibu nitoke ndani ya nyumba ntamsema wapi mtu jahili huyu nimemchukia sababu ya alah hata watoto wake wanajua dini wanamshangaa baba gani anatutia aibu mbele ya maustadh wetu sina wazazi mimi wala yeye hana wazazi ntampeleka wapi na jamii yake ni watu wa ajabu ajabu

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu mume wako kupenda muziki.

 

Tunakupa pongezi kwa kuacha muziki na kupata imani ya hali ya juu kuchukia uovu huu. Hakika inapasa umshukuru sana Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala kwa kukutoa katika uovu huo. Kwa sababu muziki katika Usilamu imeharamishwa na dalili ni kutokana na dalili zifuatazo:

 

 

 

 ((Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha)) [Luqmaan: 6]

 

Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kuhusu Aayah hii "Naapa kwa Allaah hii inamaanisha ni kuimba" [At-Twabariy 20:127]

 
Na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) pia amesema kuhusu Aayah: ((Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi)) "Ni nyimbo na maneno ya yanayofanana (ya upuuzi)" [Isnaad Sahiyh kutoka kwa Shaykh Al-Albaaniy]

 

Hivyo mume wako anapaswa kufahamishwa uovu huo. Na atambue kwamba   kuna hatari kubwa mno kwa Muislamu kupenda muzikii kwani huenda akashindwa kutamka neno la tawhiyd (laa ilaaha illa-Allaah) inapofika wakati wa kuaga dunia, Allaah Ampe umri mrefu na Amhidi kabla ya hayo. Na hasa anapokuwa garini ni hatari kubwa kwani huenda akapata ajali ikawa ni ahadi yake ya kufariki na akashindwa kumdhukuru Mola wake. Hali kama hii imeshawatokea watu kadhaa ambao walipofikwa na sakaratil-mawt walishindwa kutamka neno la tawhiyd na badala yake wakitamka nyimbo walizokuwa wakizisikiliza wakati wa mauti kuwafikia.

 

 

Hata hivyo, itambulike kuwa wanaadamu kwa hakika wana maumbile tofauti, wapo wale ambao wanakuwa rahisi kubadilika wakiijua kheri na haki, wapo walio wakaidi, wapo wenye kusitasita na kadhalika.

 

 

Kwa hiyo, mara nyingine inabidi ufanye kazi za ziada katika kurekebisha munkar nyumbani au katika jamii. Kama ulivyotuelezea kuwa wewe pia ulikuwa shabiki wa muziki lakini sasa umeacha na unakerwa sana kumuona wapili wako katika ndoa akiwa bado yumo katika uharamu wa kutekeleza hilo. Usimkatie tamaa naye pia atabadilika, kwani Muislamu hakati tamaa na rehma ya Allaah Aliyetukuka.

 

 

‘Alaa kulli haal, zipo njia ambazo unaweza kuzitumia katika kumrekebisha mumeo. Na ujue katika kufanya hilo unapata thawabu kwani mwanzo Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe” (at-Tahriym 66: 6).

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

Allaah Akukiwezesha ukawa sababu ya kumuongoa mtu mmoja ni bora kwako kuliko ngamia wekundu” (al-Buklhaariy).

 

Utakapofanya juhudi utapatiwa tawfiki na Allaah Aliyetukuka Inshaa-Allaah ya kurekebisha kosa. Tekeleza yafuatayo upate natija nzuri:

 

 

1.     Zungumza na mumeo kwa hekima, wema na mawaidha mazuri, kwani Allaah Aliyetukuka Anasema: Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora” (an-Nahl 16: 125). Tumia maneno ya busara na pia tafuta wakati munaasib wa kumpa nasaha, kwa mfano pale unapomuona ametulia nyumbani na anafuraha nawewe.

 

2.     Lingania katika njia ya Allaah Aliyetukuka kwa ujuzi na elimu iliyo bayana. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Allaah kwa upeo (elimu) - mimi na wanaonifuata” (Yuusuf 12: 108).

 

 

3.     Usifanye haraka kutaka kuona mabadiliko, kwani ilimchukua ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) miaka mitano, Abu Sufyaan na Ikrimah bin Abi Jahl (Radhiya Allaahu ‘anhuma) miaka ishirini kuingia katika Uislamu.

 

 

4.     Muombe sana Allaah Aliyetukuka du‘aa Amrekebishe mumeo. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuomba sana Allaah Aliyetukuka juu ya mama yake aliyekuwa mushrik na hata akatakabaliwa na Allaah na mama yake akasilimu.

 

 

5.     Tumia mbinu zote za kumvutia katika mas-ala ya Dini na kuacha muziki kama kumhimiza kwenda Msikitin kwa ajili ya Swalaah au darsa, kwenda pamoja sehemu za kheri. Kuwatumia marafiki zake walio wema wazungumze naye na kumshajiisha. Mchapishie makala zifuatazo na muombe azisome huenda zikamfungua macho na moyo wake atambue dhambi zake.  

 

Hukmu Ya Muziki Katika Qur-aan Na Sunnah - Ewe Upendaye Nyimbo Na Muziki, Haujafika Wakati Wa Kuogopa Adhabu Kali Za Allaah?

Muziki, Ngoma, Haramu

Tambua Kwamba Muziki Ni Haramu

Muziki

 

 

Juu ya hivyo, ukitazama utaona kuwa mume wako pengine ana tatizo hilo moja la muziki lakini wengine wamekuwa na matatizo makubwa na mengi kuliko hayo.  Kwa hiyo kuomba talaka kwa sababu ya mume kupenda muziki si jambo la busara kwani huenda Allaah (Subhaanah wa Ta’ala) Akamhidi akaacha muziki. Nawe utakuwa umeachika bure na utawaharimisha watoto na baba yao. Madamu tu anaswali basi huenda Swalah zake zikamuepusha na maovu mengineyo kama hayo.  Hivyo tunakushauri kuwa vuta subira na uzidi kumomba Mola wako Akusaidie katika jambo hili.

Tunakuombea tawfiyq katika kumuongoza mumeo na Allaah Atakulipa Inshaa-Allaah kwa iymaan yako na juhudi zako za kumtakia kheri mumeo. Na pia tunamuomba Allaah Subhaanah wa Ta’ala Akuthibitishie iymaan yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share