Nilizini Kwa Sababu Wazazi Walikataa Tuoane Sasa Tumeoana Najuta Kuzini

SWALI:

Bismillah rahman rahim, naomba mnisaidie kwa kunijibu swali hili linalonipa dhiki moyoni mwangu; mie katika kukua kwangu nilipendana na mchumba wangu ambae wazee wake walikataa asinioe. Na sisi hatukuweza kuachana kwa sababu tulipendana sana, bahati mbaya tukazini na nikapata mimba. Wazee wangu walipojua aliwatamkia kunioa. Akafukuzwa na wazee wake siku ya harusi yetu na wao ndio waliotufanya tuzini. Najuta maishani mwangu. Nimeolewa nikiwa na mimba.

je hii ndoa na mtoto niliyemzaa na watoto nilozaa baadae na kila tendo la ndoa nnalofanya na mume wangu tangu aliponioa mpaka hii leo ni halali? Nifanye nini au niombe msamaha vipi ili Allaah (swt) anihalalishie yote hayo pamoja na wanangu?

Najuta kila siku naomba msamaha kwenye msala mpaka nalia na inshAllaah mwaka huu nakwenda kuhiji Allaah (swt) akitupa khatua, nitajitahid kuomba msamaha sana inshAllaah.

(YAARAB TUSAMEHE MADHAMBI YETU YOTE UTUHALALISHIE WATOTO WETU WOTE NA NDOA ZETU AAMIYN).


 JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa baada ya zinaa. Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Ametukataza sio tu kuzini bali hata kukaribia zinaa (17: 32).  Na ajabu sana kumsikia dada yetu kuwa kuzini ilikuwa bahati mbaya. Hiyo haikuwa bahati mbaya kwani nyote mkiwa Waislamu mnajua kuwa zinaa ni dhambi kubwa na hata kama hamjui hilo lakini mtakuwa mnafahamu kuwa ni kinyume na maadili, ada na desturi ya sehemu nyingi. Mlikuwa na nia ya kufanya hivyo na mkakamilisha nia yenu hiyo kwa kufanya kimatendo.

Yaonyesha kuwa huyo mchumba wako amekosa kuifahamu Dini yake ya Kiislamu na hivyo kuona njia ya pekee ya kukupata wewe ni kukutia mimba. Tufahamu kuwa mume katika kuoa hahitaji kupata idhini ya wazazi wake tofauti na mwanamke. Na ni ajabu kuwa hata baada ya kufanya dhambi mkaendelea kukaa pamoja na kuzidisha kufanya madhambi hayo ya uzinzi. Ajabu ni kuwa wazee wako wamekubali ambao ndio sharti kwa kusihi ndoa yenu lakini hamkuweza kuitumia hiyo kwa maslahi yenu.

Naona dada yetu umekosea kabisa kwa kudai kuwa wazazi wa mume wako ndio waliowafanya kuzini kuondoa kosa kutoka kwako. Nyinyi wote wawili tayari mmebaleghe na hivyo madhambi mnaandikiwa nyinyi na sio wazazi wenu. Kwa hiyo, msitafute visingizio bali mnatakiwa murudi kwa Mola wenu Mlezi. Lau mgetaka nasaha kuanzia wazazi wake walipokataa hamgeingia katika dhambi hilo lakini kukosa kuuliza kwenu kwa walio na elimu ndio mmefikia hapo.

Hakika katika sheria ya Kiislamu mlikuwa hamfai kuoana ukiwa na mimba mpaka uzae. Lakini hilo lishapita kitu ambacho mnatakiwa kufahamu ni kuwa huyo mtoto wenu wa kwanza si mtoto wa halali wa mume wako. Ufahamu kuwa hafai kuchukua jina la mumeo na pia hao wawili hawawezi kurithiana, yaani mtoto na baba yake wa kidamu. Bila shaka baada ya kuoana Kiislamu na kupatikana masharti ya ndoa kila tendo la ndoa mlilokuwa mkifanya litakuwa ni halali na kupata thawabu kwa hilo. Hakika ni kuwa wanao wengine baada ya ndoa halali watakuwa ni wana wenu halali ama yule wa kwanza atakuwa ni mwanao pekee. Mengine yoyote utaweza kuyasawazisha ila hilo la mtoto wa kwanza.

Ama yale ambayo unaweza kupata msamaha kutoka kwa Allaah Aliyetukuka ni ile zinaa mliyofanya kabla ya kuoana. Toba inakubaliwa na Allaah Aliyetukuka baada ya kufuata masharti yafuatayo:

1.     Kujuta kwa uliyofanya.

2.     Kuweka azma ya kutorudia kosa hilo tena.

3.     Kutorudia tena kosa na dhambi hilo.

Na inaonekana kulingana na swali lako masharti haya umeyatimiza lakini hata hivyo fanya bidii zaidi kufanya mambo yaliyo mema na kuleta istighfaar kwa wingi na kuwasaidia wengine.

Unaweza kusoma zaidi kuhusu masuala hayo kwenye viungo vifuatavyo:

Ndoa Ya Wazinifu

 

Ndoa Baada Ya Kutubu Zinaa

 

Watoto Baada Ya Ndoa Ya Uzinifu

 

Wazinifu Waliotubu Wanaweza Kufunga Ndoa Na Waliotakasika

 

Ndoa Ya Waliofanya Zinaa

 

Waliofanya Zinaa Wanaweza Kuoana?

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akusamehe na Akupe hima ya kufanya amali njema kwa wingi.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share