Anamrusha Roho Katika Harusi, Anataka Ugomvi Naye, Vipi Azuie Shari Zake?

 

SWALI:

 

Kuna mtu anatafuta ugonvi na mimi, sikijui ni nimemkosea, tukiwa maharusini anajaribu kunirusha roho na taarab, na mimi sio mtu wa kugombana. Je nifanye nini? Au kuna dua yoyote ambayo naweza kusoma nikajiepusha nae kwa sababu ni mshari sana.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutafutiwa ugomvi na mtu usiyejua umemkosea nini.

Kulingana na swali lako inaonekana mkosa ni wewe kwani unajipeleka mahali ambapo hufai kuwepo kishari’ah. Tufahamu kuwa sherehe zozote ambazo zinakuwa na muziki au kurusha roho hazifai kuhudhuriwa na Waislamu.

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Allaah pasipokujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha” (Luqmaan (31): 6). Swahaba ‘Abdallaah bin Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliapa mara tatu kwa kuielezea Aayah kuwa maneno ya upuuzi yanamaanisha muziki.

 

Suluhisho kwa tatizo lako ni kuwa ujiepushe kwenda maharusini na kurusha roho na utaepukana na ugomvi wa huyo na mwengineo yeyote na pia utabakia katika taqwa, utalinda heshima yako na utatulia roho yako

 

Tafadhali bonyeza viungo vfutavyo upate maelezo zaidi:

 

Hukmu Ya Muziki Katika Qur-aan Na Sunnah - Ewe Upendaye Nyimbo Na Muziki, Haujafika Wakati Wa Kuogopa Adhabu Kali Za Allaah?

Muziki, Ngoma, Haramu

Tambua Kwamba Muziki Ni Haramu

 

Na Allaah Aliyetukuka Anajua zaidi

 

 

 

Share