Amefuturisha Watu Amezuliwa Kuwa Amesababisha Maasi; Afanyeje Na Ndugu Hawasemi Naye?

 

SWALI:
 
Asalam aleykum ndugu waislam, Allah Awasamehe dhambi zenu na awape kila lenye heri nanyi hapa na kesho Akhera.  Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu hapa ng'ambo,  kawaida yangu hujitahidi kufuturisha waislam hapa hasa wanaume  (hawajui kupika)tukishirikiana na dadazangu wachache. walikuja wanafunzi wageni kutoka nyumbani ramadhani iliyopita nao tukawakaribisha.  Baada ya Ramadhan, wageni wote 17 waliacha kuongea namimi,  wakisema wameripotiwa nyumbani kuwa wanafanya mambo ya usherati na wanadhani ni mimi kwani uhusiano wangu na anaewasponsor ni mkubwa.wasichana kadhaa seniors pia wametoa malalamiko kuwa niliwasemea kwao eti wanawanaume huku na wanaenda club nakadhalika. sijawahi fanya mambo kama hayo,ila hakuna anaeniamini HIVI WENGI HAWAONGEI NAMI,  haijawahi tokea maishani mwangu na sijawahi pata ugomvi na mtu yoyote. ramadhani hii kijaaliwa ntafuturu pekeangu,haifai kutozungumza na ndugu wakiislam kupita mda wa siku tatu lakini sina namna yakujisaidia nifanyeje?

 


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Asli ni kuwa amali uliyoifanya kujitahidi kufuturisha waislam ni njema lakini inamushkali ndani yake, kwa kuwa kama inavyojionyesha katika suala lako ni kuwa wewe ni mwanamke na kawaida ya sharia ya kiislamu ni kuwa mwanamke haruhusiwi kuchanganyika na wanaume isipokuwa wawe mahaarimu wake na hao wanaume japo kuwa umeweka sababu kuwa hawajui kupika sharia haitambuwi sababu hiyo, kwanini usiwashauri kuoa au kujifunza kupika na kadhalika?

 

 

Hata kama unashirikiana na wanawake wenzako pia nyote kama hakuna miongoni mwenu   mahaarimu wenu basi mtakuwa mnafanya amali njema na Insha-Allaah mtalipwa lakini pia mtakuwa mnaasi kwa kuchanganyika na wasio kuwa mahaarimu wenu. Mfano kama aliye kwenda Hijjah bila ya mahram, maulamaa wanasema kuwa Hijja yake huwa sahihi lakini pia huwa ameasi kwa kutokuwa na mahram.

Ama mtu kuaacha kuongea na wewe, unachotakiwa ni kuwa wewe uwe wa mwanzo katika kumsalimia na kuzungumza nae hata kama hajibu wewe kila ukimuona msalimie maamkizi ya Kiislamu ‘Assalamu ’alaykum’ na huku ukitabasamu na usiwache mpaka salamu itapoleta muujiza yake iliyopewa na Mola wake. Ila la kuangalia ni kuwa mwanamke hatakiwi awe anasalimia wanaume na kuanza kuzungumza nao bila ya kuwepo dharura au mahram wake.

 

 

 

Asli katika watu kusema jambo ukasikia au kukuzulia bila ya ushahidi ni kufuata kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):  

 

 

 

“Enyi mlioamini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo yatenda”. [Al-Hujuraat: 6]  

 

 

Hivyo basi wewe unatakiwa yasikushughulishe yale wanayoyaripoti watu, iwe nyumbani au kwengineko, ila tu elewa kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni Raqiyb; na kama wao wanafanya mambo ya uasherati na kuwa wana wanaume huku na wanaenda club na kadhalika, unachotakiwa si kuwasemea. Ikiwa umefanya hivyo au hujafanya sio muhimu, bali kuwapa mawaidha kwa kuwapendekezea na kuwaamrisha mema na kuwakataza mabaya na kuwaelekeza ubaya wa kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hasa katika kuwafuturisha japo ni aasi ilikuwa ni fursa ya kuwaidhiana na kukumbusha na kushajiishana kutekeleza mema na kukatazana mabaya.

 

 

Pia kuhusu dhana ya jambo ni kwamba hili pia tumeonywa tusiwe ni wenye dhana mbaya: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anayependa kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu” [Al-Hujuraat: 12]

 

 

 

Ukiweza kuwafutarisha waislamu wanawake wenzako Waislamu  fanya kwani ni katika jambo la kheri na jiepushe  kuchanganyika na wanaume ambao sio mahaarimu zako na hii ndio chanzo cha fitina yote ulikuwa ukiwafutarisha wasiostahiki kukaa na wewe bila ya kuwepo mahaarim  zako.

 

 

 

Mwisho ni kuwa watu hugombana na kusahau ugomvi na kusameheana na Ramadhaan ni wakati muwafaka wa kuwasamehe wewe na kuwatkia kila lenye kheri na manufaa, kwani nyote ni ndugu katika Uislam na mnachotakiwa ni kupatanishana na kusuluhishana sio vyenginevyo kama inavyothibitisha Qur-aan:  

 

 

“Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Allaah ili mrehemewe”  [Al-Hujuraat:12]

 

 

 

Pia tumeonywa na Mtume (Swalla-Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) kutokuzungumza na ndugu Wakiislam kupita mda wa siku ni kuwa amali zake hazipokelewi.

 

 

 

Imetoka kwa Abu Ayyuub Al-Answariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alisema: Kasema Mtume (Swalla-Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam)   ((Haimpasi Muislamu amhame ndugu yake zaidi ya siku tatu hata wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu. Na aliye mbora wao ni yule anayeanza kutoa salaam)) [Al-Bukhaariy na Muslim na katika Riwayaah ya Abu Daawuud ((Atakayemhama (mwenzake) zaidi ya siku tatu akafariki basi ataingia  motoni))

 

 

Pia,

 

 

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba kasema Mtume Swalla-Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam)  ((Amali njema (vitendo vyema) huoneshwa kila Jumatatu na Alkhamiys, kisha Allaah Humghufuria kila mtu asiyemshiriki kitu Allaah, isipokuwa mtu aliyekuwa baina yake na baina ya ndugu yake uhasama, Husema: Waacheni hawa wawili mpaka wapatane)) [Muslim]

Hivyo basi ni muhimu kwako kutekeleza hayo na kuwa na subra na maudhi yanayokufika.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share