Nani Masiyhud-Dajjaal? Ni Mtu Au Jini? Ataingia Kila Kona Ya Dunia?

 

Nani Masiyhud-Dajjaal? Ni Mtu Au Jini? Ataingia Kila Kona Ya Dunia?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalamualaikum Warahmatullahi Wa Barakatuh,

 

Ni matarajio yangu kuwa nyote katika Alhidaaya ni wazima wa afya na mko tayari kutupatia mafundisho na ukumbusho juu ya mambo yanayohusu dini yetu ya uislam. Nimewahi kusikia mawaidha kutoka kwa sheikh mmoja juu ya kiumbe anayeitwa  Dajjal  na vituko vyake, na hata tukausiwa na  Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa katika swala zetu tunapaswa kumuomba Allaah atuepushe  na vituko vya huyo dajjal.

 

Swali langu ni kuwa huyu dajjal ni mtu au ni jinni na je huyo dajal atatembea kila kona ya dunia hii?

Wabillah ttaufiyq

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hakika ni kuwa kila Nabiy na Rasuli aliyetumwa hapa ulimwenguni pamoja na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametuonya kuhusu kiumbe huyu ambaye umemuulizia. Hiyo ni kwa mujibu wa kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):  "Ninawatahadharisha naye kama vile Nabiy Nuwh alivyowatahadharisha watu wake" [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na pia,

"Hakuna Nabiy aliyetumwa isipokuwa amewatahadharisha watu wake na mwenye jicho moja mrongo" [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Hebu tutazame baadhi ya sifa ambazo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia kuhusu Dajjaal ili tuwe na taswira nzuri kumhusu. Huu ni ufupisho wa Hadiyth kadhaa ambazo zinapatikana katika Swahiyh al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim). Nazo ni kama zifuatazo:

 

1-Atakuwa na jicho moja tu la upande wa kushoto, na kutokuwa na jicho la kuliani. Jicho lenyewe litakuwa kama zabibu inayoelea.

 

2-Kati ya macho yake pameandikwa neno "kafiri".

 

3-Atakapotokeza atakuwa na maji na moto. Kinachoonekana ni moto basi hayo ndio maji baridi ama kile watu watakachokiona ni maji baridi basi huo ni moto unaounguza.

 

4-Hatoweza kuingia miji miwili mitukufu, nayo ni Makkah na Madiynah.

 

5-Atapatiwa muujiza wa kuweza kumuhuisha aliyekufa.

 

6-Atashindwa kumuua mwenye Imani thabiti.

 

7-Hatokuwa na kizazi.

 

8-Wafuasi wake watakuwa ni Mayahudi.

 

9-Atauliwa na Nabiy 'Iysaa ('Alayhis Salaam) katika lango la mji wa al-Lud (Palestina).

 

 

Ama mtu huyu kuweza kuzunguka ulimwengu mzima hakuna ajabu kwani uwezo huo atapewa na Allaah ('Azza wa Jalla)   naye atakuwa ni mtihani mkubwa kwa watakaokuwa hai wakati huo.

 

Qur-aan inatueleza kuwa Dhul-Qarnayn naye alipatiwa na Allaah ('Azza wa Jalla)  uwezo wa kutembea sehemu nyingi kama Anavyotuambia Allaah ('Azza wa Jalla)    Tafadhali rejea Suwrah Al-Kahf: 83 – 99.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share