Anapitwa Na Swalaah Ya Magharibi Kila Siku

SWALI:

 

A/Alaykum

Natumai hamjambo na mnaendelea vizuri na kazi zenu za kila siku Nashkuru kwa kutuwekea website hii ambayo inatuelimisha mambo mengi sana inshaallah M/Mungu atakujaalieni kila kheri Duniani na kesho Akhera Swali langu hivi?

 

Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu Daresalaam, muda wetu wa kuingia darasani ni saa 10 kamili jioni mpaka saa 2:00 usiku, kwa hiyo sala ya saa 10 na magharibi inanipita jee naweza kuzilipa kwa sala ya insha zote hizo?

Naomba nijibiwe


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu kulipa Swalah. Hili ni swali ambalo linakaririwa sana kila wakati lakini jibu lake ni sahali sana. Hakika isiyopingika ni kuwa wengi wetu bado hatujakomaa kiimani na tuna udhaifu mkubwa kwa kushindwa hata kutimiza wajibu wa Allaah Aliyetukuka.

Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu” (4: 103).

 

Hivyo jibu ni kuwa haiwezekani kabisa kuwa kila siku wewe unalipa Swalah za Alasiri na Magharibi.

Licha wewe unasoma sehemu ambayo Waislamu ni wengi, wengine wanaosomea Chuo cha kikafiri katika nchi ya makafiri kusiko hata na kutambulika haki za Kiislam kama huko ulipo, na walikuwa wanaingia kuanzia saa tatu hadi Magharibi lakini hawakuwa wakikosa Swalah hizo kwa wakati wake.

 

Muhimu ni wewe kujipanga na kutoka kwa ajili ya Swalah pindi inapofika. Na kwa kuwa upo Dar es Salaam huenda ikawa Swalah ambayo utatoka darasani ni moja tu, Magharibi. Swalah ya Alasiri huwa inaingia mapema kwa maeneo ya pwani huenda ikawa inaingia kabla ya saa kumi. Unachotakiwa kufanya ni kupata nyakati za Swalah kwa eneo la Dar kwa mwaka mzima. Ukawa unatazama wakati wa kuingia Swalah, na ikiwa inaingia kabla ya saa kumi swali Swalah ya Alasiri kisha nenda darasani.

 

Na inapofika wakati wa Magharibi toka darasani pata mahali nje ya darasa na uswali Swalah yako kisha urudi darasani. Hutakosa mengi yaliyozungumzwa na mwalimu huyo katika somo hilo.

 

Ama ukiwa umebanwa sana unaweza baadhi ya siku ukaunganisha Magharibi na ‘Ishaa katika wakati wa ‘Ishaa ukiziswali zote kamili; yaani Magharibi rakaa tatu na ‘Ishaa rakaa nne.

 

Ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

 

Vipi Kukidhi Swalah Kama Shida Kuswali Kazini?

 

Hapati Kuswali Kwa Wakati, Kila Siku Anakidhi Swalah

 

Tunakuombea tawfiki ya kuweza kutekeleza ‘Ibaadah hiyo kwa wakati wake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share