Makundi 72 Yatakayoingia Motoni

SWALI:

assalam aleikum.amma baad namshukuru Allaah kuniwezesha tena kuandika sula hili ambalo natumai litakuwa bayana kwako kwa uwezo wake Allaah. Naomba uanitajie makundi 73 ambayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)(s.a.w) kayabashiria kuwa yataingia motoni ila moja tu na unifafanulie vizuri tofauti zao? Ahsante wajazakAllaahu kheir. 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako hilo kuhusu makundi yaliyotajwa kwa idadi katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa yataingia Motoni. Ieleweke kuwa hapa si mahala pake pa kuweza kuyaeleza makundi hayo kufanya utafiti huo itabidi tusiwe ni wenye kujibu maswali wala kufanya kazi wala shughuli nyengine isipokuwa hiyo. Hivyo ni juu ya mwanafunzi kwenda katika vitabu vingi vilivyoelezea hayo.

Kwa kifupi tu kwa kukupa mwangaza kidogo, utayajua yale makundi yaliyo potofu kwa kuona na kujua itikadi zao. Mfano mzuri leo utaona wanaodai kuna mtume baada ya Mtume wa haki na wa mwisho Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), utawaona pia wale wanaowakufurisha Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) na kuwatukana wake za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pia utawaona wengine wanaokufurisha Waislam na kuwatoa katika Dini kwa sababu wanaamini kuonekana Allaah Qiyaamah, na wanakufurisha Waislamu kwa sababu ya kufanya baadhi ya maasi, na pia utawaona wengine wanakataa Hadiyth za Mtume na kudai kuwa wao wanafuata Qur-aan pekee, na pia utawakuta wengine wanakwenda kuwaomba watu waliokufa makaburini ili wawasaidie haja zao, na wengi wengine wasio na idadi.

Tutalijua kundi lililookoka na ambalo halipo katika hayo makundi 72, kwa kuitazama ile Hadiyth ya bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:  

((Wamegawanyika Mayahudi katika mapote 71, wakagawanyika Wakristo katika mapote 72 na Ummah wangu utagawanyika mapote 73. Yote hayo yataingia motoni ila moja tu)) Maswahaba waliuliza: Ni lipi hilo, ewe Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa Allaah! Akasema: ((Ni lile nililokuwemo mimi na Swahaba zangu)) [Ahmad, Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy na Ad-Daarimiy].

Kundi hilo litakuwa ni lenye kufuata maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Makhalifa waongofu (Radhiya Allaahu ‘anhum) na Maswahaba wengine (Radhiya Allaahu ‘anhum) na wema wote waliotangulia (Salafus-Swaalih). Muislam atakayejikita na kuwa imara katika hayo basi atakuwa katika njia nyoofu. Dalili ni nyingi katika Qur-aan na Sunnah. Miongoni mwayo ni kauli ya Aliyetukuka:

((Na anayemtii Allaah na Mtume Wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa)) [33: 71].  

Pia Amesema Aliyetukuka:

((Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu. Na Allaah ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu)) [3: 31].

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye anatueleza yafutayo katika khutbah yake ya Hijjatul Wadaa: ((Hakika nimewaachia kitu ambacho hamtapotea baada yangu lau mtashikana nacho, Kitabu cha Allaah)) [Muslim].

Sehemu nyengine kasema: ((Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

Na katika masimulizi ya Abu Najiih al- 'Irbaadh bin Saariyah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Alituwaidhia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yaliyozifanya nyoyo kuingia hofu na macho yakatokwa na machozi. Tukamwambia: "Ewe Mtume wa Allaah! Yaonyesha kama haya ni mawaidha ya kuaga, basi tuusie". Akasema: ((Nawausia kumcha Allaah, Kwani hakika atakayeishi katika nyinyi ataona khitilafu nyingi, basi jilazimisheni kufuata Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa walioongoka, yashikeni kwa magego mambo yao)) [Abu Daawuwd, Ahmad, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na Ad-Daarimiy].

Mambo muhimu ambayo tunayapata katika dondoo za hapo juu ni kuwa, kuwepo kwetu katika kundi litakaloongoka ni kufuata mwendo aliokuwa nao Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na kushikamana nao kivitendo barabara.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atufanye ni wenye kuyashikilia hayo vilivyo ili tuwe ni wenye kuingia katika Rehma Yake na kuwa ni kundi lililosalimika na moto, kundi lililonusurika na ni kundi liliokoka. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atusahilishie hatua zetu katika kuelekea katika mwendo wa sawa na wa haki.

Na Allaah Anajua zaidi  

 

Share