Jamaa'atu At-Tabliygh Na Muasisi Wake Aliyekuwa Mtu Wa Bid’ah

 

Jamaa'atu At-Tabliygh Na Muasisi Wake Aliyekuwa Mtu Wa Bid’ah

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalaamu alaikum.

Kuna hili kundi la tabligh, wenyewe wanasema lengo lao ni kuifufua suna ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) hivo wanakuwa wakitoka ama siku tatu, arobaine au miezi minne, etc... wanasema kufanya hivyo ni mtu kujiweka mbali na mazingira ya nyumbani ili kufanya fikra ya dini wakiwa huru kabisa manake hizo siku zote huwa wamekaa misikitini, na hawatoki ila wakienda haja au kufanya jaula au sokoni kuhemea, na wanadai hicho kipindi chote huwa wametoka fii sabiilillahi; lakini sasa kuna masheikh hawakubaliani na hayo wayafanyao Tabligh wakisema ni uzushi kwa vile hata na mu'asisi wa tabligh Muhammed Zakaria alikuwa mtu wa bid'a. Naomba mniweke sawa kutokana na hili kundi la Tabligh na itikadi yao kama ni sahihi au la. Jazakallahul khair.

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Harakati hizi za Tabliygh zilianzia huko India na zilianzishwa na Muhammad Ilyaas bin Muhammad Ismaa‘iyl Hanafiy Deobandi Chisti Kaandhalawiy, na si kama ulivyoandika kuwa muasisi wake ni Muhammad Zakariya. Hapo juu katika jina la muasisi zipo lakabu ambazo ingefaa tuziweke sawa, nazo ni:

 

1.     Hanafiy – kuonyesha kuwa alikuwa mfuasi wa dhehebu la Imaam Abu Haniyfah.

 

2.     Deobandi – kuonyesha kuwa alipitia katika Madrasah ambayo inapatikana India katika mji unaoitwa Deoband.

 

3.     Chisti – kumnasibisha na ile twariyqah (njia ya usufi) ambayo alikuwa anaifuata.

 

4.     Kaandhalawiy – kumnasibisha na mji aliozaliwa/aliotoka.

 

Yapo makosa ambayo yanafanyika kwa makundi kadhaa kama tulivyotangulia kueleza na Muislamu anatakiwa anapokuwa na makosa ajirekebishe na kujiondoa katika kosa na kujiweka katika hali ya usafi na mbali na utata. 

 

 

Miongoni mwa makosa kwa hao Tabliygh ni huku kuweka siku maalumu za kutoka kama siku kila wiki, siku tatu kila mwezi, siku arobaini kila mwaka na miezi minne kwa umri.

 

Na katika kutoka huko huwa wanawaambia wafuasi wao kuwa watoke siku hizo kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka. Je, siku nyingine zilizobaki Waislamu watoke kwa ajili ya nani? Shaytwaan!

 

Bali usawa ni kuwa Muislamu anatakiwa ayatoe maisha yake yote kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka. Ndio Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾

Sema: Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.  Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza. [Al-An‘aam: 162 – 163]

 

Muislamu mzuri ni yule anayekabiliana na mazingira ya nyumbani ili kuyarekebisha si yule mwenye kuyakimbia. Na ndio Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuelekeza kwa kutwambia:

 

"Mche Allaah popote ulipo, na unapofanya baya lifuatishe na zuri. Na hilo zuri litafuta baya. Na tangamana na watu kwa tabia njema" [Ahmad, at-Tirmidhiy na ad-Daarimiy].

 

Fikra inatakiwa ifanywe katika kijiji, kitongoji, au eneo mtu anayoishi, kwani mwanzo amri imekuja ya kuwahofisha watu wa nyumbani kabla ya kutoka nje. Na Muislamu kukaa Msikitini peke yake amekatazwa kwani Uislamu ni mfumo kamili wa maisha, hivyo ni msahafu na upanga, ni 'Ibaadah na Jihaad, ni kazi na mapumziko. Hivyo, Muislamu anatakiwa afanye kazi ili ailishe familia yake kwa pato la halali na hivyo afanye ‘Ibaadah nyingine kama Swalah, Swawm, Hajj, Jihaad na mengineyo. Inatakiwa tufahamu kuwa mara nyingi neno ‘Fiy SabiyliLlaah’, linapotumika katika Qur-aan huwa linamaanisha Jihaad, kwa kuipigania Dini ya Allaah Aliyetukuka kwa kutumia silaha. Hata tukifaradhisha kuwa inamaanisha ulinganizi (Da‘wah), je maana yake ni kutoka tu kwa muda mdogo wa maisha au ni vipi? Maana yake halisi ni kinyume na hayo wanayosema.

 

Mwanzilishi wa kundi hilo ametumbukia kwenye makosa mengi ukilinganisha mfumo wake na Uislamu wenyewe. Hata hivyo, inaonyesha wafuasi wake wamekataa kubadilisha mfumo huo ili kuliweka kundi hilo katika mfumo mzuri, bali wamemfuata mwanzilishi wao kiupofu. Mambo yenyewe ni kama yafuatayo:

 

1.     Kauli ya kuwa Taqliyd (umbumbumbu/ kufuata bila kuuliza) ni wajibu, kwani masharti ya Ijtihaad ambayo yamewekwa na watangu wema hayapo tena wakati huu. Na hili si sawa kwani Ijtihaad itabaki mpaka siku ya Qiyaamah.

 

2.     Kuitakidi kuwa njia ya Usufi ndio njia ya kuwa na mafungamano na Allaah na kupata utamu wa Imani. Na hiki ndicho kipimo cha kupimia wafuasi wao kushikamana sawa sawa na kundi hilo. Na hakika ni kuwa mafungamano na Allaah Aliyetukuka hayakufungamana na usufi bali ni ‘Ibaadah ambayo anafuata mja kujikurubisha kwa Allaah Aliyetukuka kama Swaalah, Swawm na Hajj, pamoja na mambo yote ya Faradhi na Sunnah.

 

3.     Kutokataza kwao mabaya (Munkar) kwa hali zote, huku wakielezea kuwa wakati huu kwao si muafaka mpaka watu waingie katika kundi lao. Na hii ni kinyume na Qur-aan pamoja na Sunnah, kwani kuamrisha mema na kukataza maovu ni vitu viwili vinafuatana. Tafadhali tazama Qur-aan Al-‘Imraan [3]: 104, 110, 114 na nyinginezo nyingi.

 

4.     Hawaoni haja ya kutoka nje ya zile mbegu sita ambazo amezianzisha mwanzilishi wao Muhammad Ilyaas. Mbegu sita zenyewe ni kama zifuatazo: Shahada, kusimamisha Swalah, Elimu na Dhikr, Kumkirimu kila Muislamu, Ikhlaasw na kutoka Fiy SabiyliLlaah. Na wanaona kuwa kutoka nje ni kutoka nje ya mpango wa kundi. Ilhali sahihi ni kuwa mfumo wa Kiislamu ambao umekamilka unatutaka tuingie kwa moyo wetu wote sio nusu nusu. (Tazama al-Baqarah: 208).

 

5.     Wanawakataza wafuasi wao kupanua elimu zao na kutazama falsafa za jamii wanazoishi ndani yake. Na hili tumelishuhudia kwani hufai kutoka katika yale maelezo ambao Amiri wa kundi amewaelezea bali unatakiwa ufafanue kama ulivyoelezewa bila kuongeza hata ikiwa ni sahihi.

 

 

6.   Wanatenganisha baina ya Siasa na Dini kama kwamba ni vitu vyenye ukinzani ilhali msimamo wa Uislamu ni Dini na Dola.

 

7.     Wanaona kuwa si vyema watu wa kijiji au nchi moja kuwalingania wenziwao bali inavyofaa kwao ni kuwa watu wa kijiji kimoja au mji mmoja au nchi moja wawalingalinie walio katika kijiji kingine au mji mwengine au nchi nyengine. Na huu si msimamo wa Uislamu. Qur-aan inatueleza kuwa Rusuli walitumilizwa kwa watu wao. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiziwa:

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ ﴿٢١٤﴾

Na onya (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) jamaa zako wa karibu.  [Ash-Shu‘araa: 214]

 

8.     Wana msimamo wa uadui kwa Mashaykh na wanachuoni wa Da‘wah ya Kiislamu, mfano wamemzungumza vibaya Mwanachuoni Mujaddid Shaykh Muhammad ‘Abdul-Wahhaab na wengineo. Kwa mfano, Husayn Ahmad al-Hanafiy, mmoja miongoni mwa wakubwa wa kikundi hicho amesema yafuatayo kuhusu Shaykh Muhammad ‘Abdul-Wahhaab: “Jueni kuwa Muhammad bin ‘Abdul-Wahhaab ilidhiri jambo lake mwanzo wa karne ya kumi na tatu huko Najd. Naye alikuwa na Itikadi potofu na nadhariya za batili”.

 

Tunadhani kwa hayo yatakupatia fikra nzuri kuhusu Tabliygh.

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

 

 

Kundi Tabliygh Liko Katika Sheria Ya Kiislam?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share