Mdogo Wetu Amejiozesha Bila Ya Radhi Za Mama, Tuuze Simu Tulomnunulia Ili Tutoe Pesa Katika Sadaka?

SWALI:

ASSALAM ALEYKUM WARAHMATULLAHI WA BARAKATU.

SWALI LANGU NI HILI: NINA MDOGO WANGU WA MWISHO WA KIKE AMETAKA KUOLEWA NA MWANAMME MMOJA NASI NDUGU WOTE HATUTAKI AOLEWE NA HUYO BWANA KWANI SISI HATUMJUI TABIA ZAKE, MPAKA HUYO BWANA AKAFIKIA KUANZA KUMNUNULIA NGUO NA SIMU ILI AWE ANAWASILIANA NAE MIMI NILIVOGUNDUA ANA SIMU NIKAMTUMA DADA ANGU MKUBWA AKAZIME SIMU ALIVOENDA NAE SIMU NJE DADA ANGU MKUBWA AKASEMA NIMEIBIWA, YOTE HAYO TULIKA ATUTAKI AWE NA MAWASILIANO NA HUYO BWANA, HIO SIMU AKANIPA MIMI MPAKA SASA NINAYO.

BAADA YA MWEZI MMOJA TUKASIKIA WAMESHAOANA KISIRI KWA KWELI TUMECHUKIA SANA MDOGO WETU ALIVOFANYA MPAKA AMEFIKIA KUMLIZA MAMA YETU MZAZI, NDIO TUKACHUKUA JUKUMU LA KUMFUKUZA PALE NYUMBANI KWETU NA MPAKA SASA YUKO KWA HUYO MME WAKE.

SASA NAULIZA KUHUSU ILE SIMU NILIE NAYO NIIFANYEJE? JE TUUZE NA HIZO PESA TUGAWE KWA WATOTO YATIMA AU TUTOE SADAKA KWA WATU MASIKINI?

NATUMAI MAJIBU MEMA TOKA KWENU.

SHUKRAN JAZIRA. MAASALAM!


 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mdogo wenu na aliyoyafanya. Tatizo hili ambalo mmelitaja katika swali lenu linarudi katika malezi. Yaonyesha kuwa malezi hayakuwa mazuri au mdogo wenu alikuwa anadekezwa kwa jinsi akachukua sheria mkononi mwake bila kujali hatima yake.

Pia hamkutumia njia za kisheria ya kuweza kutatua tatizo hilo la mdogo wenu. Ikiwa mwanamme Muislamu amekuja kuposa nanyi hamumjui ilikuwa ni wajibu wenu wa kumuulizia kwa wanaomjua hadi mfike hatima yake. Kwa kutofanya hivyo ndio maafa yamekuwa makubwa dhidi yenu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwausia wazazi kwa kuwaambia: “Akikujieni yule ambaye mmeridhia Dini na maadili yake mwozesheni, mkitofanya hivyo kutakuwa na fitina katika ardhi na ufisadi mkubwa” (at-Tirmidhiy).

Tabia hujulikana kwa njia nyingi zinazojulikana na wazee lakini mliacha kufanya hivyo badala yake mkatumia nguvu ambazo hazikufaulu. Mara nyingi kukosa kuzungumza na wasichana wetu kwa njia iliyo njema ndio hupatikana matatizo haya.

Kisha ilikuwa si juu yenu kuchukua kwa udanganyifu kisichokuwa chenu. Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wamekataza kabisa udanganyifu kwa kiasi ambacho Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kutudanganya si katika sisi” (Muslim).

Baada ya hapo mkafanya kosa jingine la kumfukuza mdogo wenu hivyo kumpatia nguvu zaidi kuyaendea maasiya. Hakuna ndoa katika Uislamu bila ya walii sasa mumemtumbukiza na kumuacha mdogo wenu katika maasiya ambayo yatamuathiri kwa muda mrefu katika maisha yake. Sasa kinachotakiwa nyinyi kufanya ni kujaribu kumtoa katika maasiya hayo ya uzinzi na pengine kuwafungisha ndoa kihalali ili asizidi kupata madhambi.

Na kwa kuwa hiyo simu mlioichukua si mali yenu inabidi mumrudishie mwenyewe kwani hamuwezi kuiuza na kufanya hivyo mtapata madhambi hata kama pesa mtakazopata mtazitoa sadaka. Sadaka inatolewa kwa mali safi, yake mtu binafsi na sio ya mtu mwengine.

Twataraji hayo majibu yetu yameeleweka. Tunamuomba Allaah Awape ilhamu ya kuweza kutatua tatizo hilo la mdogo wenu na muweze kumtoa katika aliyo nayo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share