Baba Amefariki Ameacha Wake Wawili, Watoto Saba Wa Matumbo Matatu Mbali Mbali

SWALI:

 

Assallam alaikum sie baba yetu amefariki na amewacha wake wawili na watoto saba wanne tumbo mbali na wawiwi tumbo mbali na mmoja peke yake, wanaume wa 3 na wanawake wane; sasa marehem kabla ya kufariki alisema kwamba akifa ile nyumba mmoja atamuachia mkewe aliezaanaye mtoto mmoja lakini hakukuwa na maandishi jee sheikh tunaomba fatwa juu ya jambo hili marehem kaacha nyumba mbili jee urithi huu utagaiwa vipi ili tusije kudhulumiana


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Asli katika mirathi ni Aayah hizi mbili:

      

"Allaah Anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili za alichokiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alichokiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliyekaribia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyotoka kwa Allaah. Bila ya shaka Allaah ni Mjuzi na Mwenye hikima. Na fungu lenu ni nusu walichoacha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walichoacha, baada ya wasia waliyo sia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlichokiacha, baada ya wasia mliousia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia uliousiwa au kulipa deni, pasio kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Allaah ni Mjuzi na Mpole." An-Nisaa: 11-12.

 

Aayah tulizonazo zimebainisha kuwa wote uliowataja kuwa wako hai baada ya kifo cha mzazi wao ni warithi ila tu mirathi yao inatofautia kulingana na vigawanyo alivyovigawanya Allaah kama Alivyobainisha hapo.

 

Tatizo ni kuwa mzee aliusia akifa ile nyumba mmoja atamuachia mkewe aliezaa naye mtoto mmoja lakini hakukuwa na maandishi.

 

Huu ni usia kama unavyoeleweka katika Uislamu; na asli katika wasia ni Hadiyth ya Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) aliposema:

 

"Mali ilikuwa ni ya mtoto na wasia wa wazazi wawili; Allaah Akafuta Alichopenda na kujaalia fungu la mtoto wa kiume ni kama fungu la watoto wanawake wawili, na Akajaalia fungu la wazazi wawili, kila mmoja wao apate sudusi; na Akajaalia fungu la mke thumni na robo; na fungu la mume nusu na robo" Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Wasia, mlango 'Hakuna wasia kwa mrithi'.

 

Hadiyth hii inabainisha wazi kuwa huyo mke hatakiwi kupewa wasia ulioachwa kwani ni katika warithi wa aliyekufa, hata hivyo kama warithi wote wengine waliobakia wataupitisha basi atapewa, na wasia unatekelezwa baada ya kulipwa madeni ya maiti kama yapo.

 

Na wasia unajuzu kama ni thuluthi ya mali au chini ya thuluthi kama ilivyopokelewa katika Hadiyth ya Ibn Abi Waqqaas (Radhiya Allaahu 'anhu) wakati Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomzuru katika maradhi ya mauti yake, ama katika hali yenu kama ulivyobainisha kuwa marehem kaacha nyumba mbili kama hizo ndio mali yote basi ikiwa baadhi ya warithi wataupitisha na wengine wakakataa kuupitisha; basi wasia huo utatolewa katika fungu la walioupitisha tu, vyenginevyo ni kuwa mali itagaiwa bila ya kuzingatia wasia kwani wote ni warithi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share