Anapomaliza Hedhi Anaweza Kufanya Wudhuu Kisha Afanye Jimai Na Mumewe Kabla Ya Ghuslu?

 

Mwanamke Anapomaliza Hedhi Anaweza Kufanya Wudhuu Pekee

Kisha Ajimai Na Mumewe Kabla Ya Ghuslu?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 SWALI:

 

Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

 

Baada ya salam naomba ufafanuzi wa swali langu hili.

 

Ninavyoelewa nikuwa mwanamke anapokuwa katika hedhi haruhusiwi kukutana na mumewe kimwili mpaka atwahirike (akoge kwa ajili ya kuongdosha hadath kubwa ya hedhi). Hivi karibuni nimesoma kitabu fulani cha dini kinachohusu maswala ya ndoa kikaeleza kuwa mume anaweza kumuingilia mkewe pindi tu damu ya hedhi itakapomalizika si lazima mwanamke akoge josho kubwa bali anaweza kujisafisha vizuri sehemu iliyokuwa inatoka damu,au anaweza kutia udhu au anaweza kukoga kabisa, likipatikana lolote kati ya haya matatu ni halali kwa mke kukutana na mumewe kimwili. Jee hii ndio sahihi? naomba ufafanuzi juu ya hili.

 

WabiLlaahi tawfiq 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

Rai za ‘Ulamaa kuhusu kumuingilia mwanamke anapomaliza hedhi kabla ya kufanya ghuslu zimepatikana nazo ni kama zifuatazo:

 

Rai ya kwanza ni kwamba hadi mwanamke amalize hedhi na afanye ghuslu (aoge josho). Hii kutokana na kauli ya Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 

 وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾ 

Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara; basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike. Watakapotwaharika basi waendeeni kupitia pale Alipokuamrisheni Allaah.”  Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha  [Al-Baqarah: 222] 

 

Rai ya pili ni kwamba mwanamke anapomaliza hedhi mumewe anaweza kumuuingilia pindi yakifanyika matatu yafuatayo; Atakapokuwa ametwaharika kutokana na damu ya hedhi yote na kutoka kwake kumesimama kabisa, hapo anaruhusiwa kurudia kitendo cha jimai baada ya kuosha sehemu inayotoka damu, akafanya wudhuu au akakoga josho kamili (Ghuslu). Vyovyote kati ya haya matatu atakavyofanya itaruhusiwa kwao kurudia kitendo cha jimai kutokana na kauli ya Allaah:   

 

   ۚ فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا ۚ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ﴿١٠٨﴾

Humo mna watu wanaopenda kujitwaharisha. Na Allaah Anapenda wanaojitwaharisha.  [At-Tawbah 9:108]

 

Lakini rai ilyo na nguvu kabisa ni rai ya kwanza kwamba mwanamke ajitwaharishe kwa maana afanye ghuslu (aoge josho) ndipo mumewe aweze kurudia kitendo cha jimai.

Kwa maelezo zaidi ingia katika kiungo kiufatacho:

 

Je, Inafaa Kujimai Na Mke Baada Hedhi Lakini Kabla Ya Ghuslu?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share