Zingatio: Ee Nafsi... Jichunge

 

Zingatio: Ee Nafsi… Jichunge

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

Nafsi na mwili ni vitu viwili tofauti. Wakati wa kukata roho, nafsi hurudi mbinguni ilhali mwili unarudishwa kwenye ardhi. Nafsi ndiyo inayosikia taabu, shida na kuona raha. Mwili ni wenye kupokea tu hizi raha na shida. Katika hali zote, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndio Muweza wa kila kitu. Yeye ndiye Anayekitambua kiumbe Chake ndani na nje.

 

Mwanaadamu siye mwenye kujijua hata kilicho ndani ya mwili wake. Wapi kinaenda chakula anachokitia kinywani na namna gani kitamuathiri mwili wake. Hivi ni vitu ambavyo vimo ndani ya mamlaka ya Muumba wa mbingu na ardhi. Mwanaadamu atabakia kuwa ni mbahatishaji tu.

 

Wanaadamu tunajidai kughafilika kwa pumbazo za dunia hii. Hali ya kuwa Rabb Haghafiliki kwa chochote tunachotenda. Mara nyingi tunapotenda ujinga huwa tunaelewa athari zake. Je kaka mwenye kuburura suruali yake haelewi ya kwamba huwa inachanika chini? Au hakuna madhila yoyote yanayomgusa dada anayetembea na mini skirt? Pamoja na kwamba yote hayo ni madhambi.

 

Kwa hali zote, tukae tuvute fikra zetu vizuri. Kwamba Rabb ni Mwenye kumtambua kiumbe wake kuliko anavyojielewa mwenyewe. Hata hizo kamera zilizoweka kuwachunga wanaadamu bado hazina uwezo wa kuona yaliyomo ndani ya nafsi!

 

Kwa hakika tunatamka kwamba; kila lifanywalo na mwanaadamu litalipwa. Iwapo ni dogo mithili ya mdudu chungu au kubwa mfano wa mbingu na ardhi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tunakuomba utuepushe na ghadhabu Zako zisizofanana na ghadhabu za yeyote!

 

Rabb Hahitaji kuwa na darubini kuona ndani ya nafsi. Jicho linapofumba na kufumbua (linapopowesa) Yeye Ameshalirikodi zamani kabla ya hata kutikisika. Basi ni lipi twajidanganya kwamba litampita kwenye rikodi Zake? Iwapo basi kupwesa kwa jicho ni jambo dogo kulirikodi, iwe ni vigumu Muumba kujua kwamba umezini na nani na mara ngapi? Wapi twakimbilia?!!

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema ndani ya Qur-aan (tafsiri):

 

يَعْلَمُ خَائِنَةَ الْأَعْيُنِ وَمَا تُخْفِي الصُّدُورُ﴿١٩﴾

(Allaah) Anajua khiyana za macho na yale yanayoficha vifua. [Ghaafir: 19]

 

Ndugu wakaa njiani ukisubiri vimwana vipite uvikodolee macho. Basi hukumbuki kwamba Yupo Anayekuangalia na Anajua ule upweso wako wa jicho iwapo ni wa kheri au shari.

 

Basi tujichunge na tupangue mipango ya kumuasi Rabb. Kwani tunapokipanga ndani ya nafsi zetu, Yeye Ameshalitambua hilo kabla ya kulitenda.

 

Na anayeweza miongoni mwetu basi aanze leo kutafuta kipande chake cha ardhi cha kuishi. Ardhi ambayo haitokuwa ni ya Muumbaji. Chakula anachokula kisiwe kinatokana na Rabb. Atafute makaazi yake na mapema kabla ya kutiwa mbaroni siku yake ya kukata roho. Na anayeweza kupenya atoke ndani ya tumbo la mbingu na ardhi, na afanye hivyo!

 

Share