Mke Aliyeomba Aachike (Khul'u) Kabla Ya Kuingiliwa Na Mume -Hukmu Ya Mahari Na Eda

 

 

Mke Aliyeomba Aachike (Khul'u) Kabla Ya Kuingiliwa Na Mume

Hukmu Ya Mahari Na Eda

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Ikiwa mke ndo ametaka kujivua katika ndoa kabla hawajakutana na mumewe, masharti ya kuivunja ndoa hii yakoje, hasa katika suala la haki baina yao juu ya mahari, eda, na gharama za ndoa kwa ujumla?

Baaraka Allaahu fiykum

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

Mke anayejiachisha (khul'u) kabla ya kufanyika tendo la ndoa, anapaswa kurudisha mahari ya mume wake kutokana na dalili ya Hadiyth ifuatayo:

 

عنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {أَنَّ اِمْرَأَةَ ثَابِتِ بْنِ قَيْسٍ أَتَتْ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! ثَابِتُ بْنُ قَيْسٍ مَا أَعِيبُ عَلَيْهِ فِي خُلُقٍ وَلَا دِينٍ، وَلَكِنِّي أَكْرَهُ اَلْكُفْرَ فِي اَلْإِسْلَامِ، قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  " أَتَرُدِّينَ عَلَيْهِ حَدِيقَتَهُ؟ "، قَالَتْ: نَعَمْ. قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  " اِقْبَلِ اَلْحَدِيقَةَ، وَطَلِّقْهَا تَطْلِيقَةً} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ . وَفِي رِوَايَةٍ لَهُ: {وَأَمَرَهُ بِطَلَاقِهَا}

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa) amesema kuwa: “Mke wa Thaabit bin Qays  alimuendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Thaabit bin Qays simtii kasoro katika tabia wala Dini lakini nachukia kukufuru nikiwa Muislamu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Utamrudishia shamba lake?” Akasema: Ndio. Rasuli wa Allaah akasema: (kumwambia Thaabit): “Kubali shamba lako na umuache talaka moja.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

Katika Riwaayah yake nyingine imesema: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamrisha ampe talaka.”

 

Kadhaalika, hatokaa eda kwa mujibu wa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا ﴿٤٩﴾

Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu. Basi wapeni kitoka nyumba na waacheni huru, kwa mwachano mzuri. [Al-Ahzaab: 49]

 

Lakini ingelikuwa amemuingilia basi ingelibidi mke akae eda mwezi mmoja kutokana na dalili ifuatayo:

 

 أَنَّ اِمْرَأَةَ ثَابِتِ بْنِ قَيْسٍ اِخْتَلَعَتْ مِنْهُ، فَجَعَلَ اَلنَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  عِدَّتَهَا حَيْضَةً

“Mke wa Thaabit bin Qays alipewa talaka (ya khul'u) kwa kurudisha shamba, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamuru Eda yake iwe ni kipindi kimoja cha hedhi.” [Abuu Daawuwd na At-Tirmidhiy na ni Hadiyth  Hasan]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share