Mke Kaambiwa Akitoa Mguu Wake Nje Ni Talaka Na Mke Amefanya Hivyo Je Ameachika? Vipi Arudi Katika Ndoa?

SWALI:

 

Asalam alaikum kwa waislam wote wanaohusika na mtandao huu. Bismilah rahman arrahim napendelea kuuliza swali hili kwa faida ya waislam wote inshallah. Kuhusu sisi wanawake tulio ndani ya ndoa.jirani yangu aligombana na mume wake na baada ya ugomvi yule mwanamke aliamua kutaka kuondoka ndani ya nyumba alishindwa kuvumilia tena matatizo madogo madogo. Mume akamwambia ukitoa mguu wako nje ya nyumba hii basi utakua si mke wangu kuanzia utakapotoa mguu nje ya mlango huu. Basi yule mwanamke hakuelewa chochote kwa wakati ule aliutoa mguu wake nje ya mlango wa nyumba baada ya masaa machache yule mwanamke alirejea mule ndani. Sasa je mwanamke yule atakua ameshaachika au bado atakua anaendelea ndoa kutokana na alirudi ndani ya nyumba? Na kama hayuko ndani ya ndoa basi afanye nini ili arudi ndani ya ndoa?

 

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa iliyowekewa sharti au masharti.

Kabla hatujaingia katika swali hili ni vyema tukumbushane machache kuhusu maisha yetu ya kindoa. Matatizo katika ndoa baina ya mume na mke ni kawaida mbali na kuwa inatakiwa kwetu tufanye juhudi ya kutatua matatizo hayo mdogo madogo bila ya ugomvi. Matatizo hayo madogo yanatokea kwa wanandoa kwa kutojua majukumu yao na jinsi ya kuvumiliana na kutatua shida hizo kwa namna moja au nyingine.

 

Wanaume nao wana jukumu zaidi la kuwaelewa wake zao na maumbile yao hivyo kutoweka mambo ambayo yatakuja kutia doa katika ndoa. Na wanawake pia wasiwe ni wenye kuchukua hatua za haraka kisha kuja kujuta baadaye na kushindwa labda kurudiana na mume au ndoa hiyo kuingia katika matatizo zaidi. Hiyo ni talaka iliyowekewa masharti na mume, hivyo mke akifanya kama alivyofanya kutoka nje ya nyumba talaka huwa imepita hapo hapo. Hivyo, mke ameachika talaka moja. Kule kurudi kwake nyumbani kwa mke si kurudiwa na mume bali inatakiwa mume akubali hilo la kumrudia. Ikiwa mume hatomwambia lolote baada ya kurudi na pengine kujimai naye, hiyo ni ishara tosha ya kuwa mke amerudiwa lakini talaka moja itakuwa tayari imepita.

 

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

 

Mume Kasema Nikifanya Jambo Nimeachika, Nami Nimefanya Na Kumdanganya Kuwa Sikufanya, Nini Hukmu Yake?

 

Nimemdanganya Mume Wangu, Je, Nimeachika? Na Je, Inanipasa Nikae Eda?

 

Talaka Kwa Kuasi Amri Ya Mume

 

Akienda Kazini ndio talaka Yake – Mume Hamhudumii yeye wala watoto wake Afanyeje?

 

 

Mume Kaahidi Kutoa Talaka (Tatu) Ikiwa Mke Alifanya Zinaa Kabla Au Baada Ya Kumuoa Naye Mke Amefanya Zinaa Lakini Ameficha

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share