Nilihama Nyumba Ya Mume Wangu Nikiwa Na Mimba, Mume Hakunihudumia Hadi Nimezaa, Anataka Nirudi

SWALI

 

 

Assalam aleikum, mimi ni mwanamke wa miaka 28, niliolewa kwa mda wa miezi mitatu na nusu kisha nikatoka kwa mume wangu. Alifukuza kwa ajili nilikataa kuishi na binti yake wa miaka 16. Binti mwenyewe ni wa nje ya ndoa na hakusema yakuwa ana watoto wa nje ya ndoa. Nilipotoka kwake nilikuwa nina mimba mwezi moja. Nimekaa kwetu mpaka nikazaa hivi mtoto yuko mwaka moja. Mume haniulizii wala haniangalii na mtoto pia hajamuona wala kumwangalia kwa masruf. Swali langu ni je mimi ni nimeachika? Na mume kama huyu anamaanisha nini? Kweli mtu kama huyu anaweza kuishi na mimi vizuri? Sababu ataka kunirudisha. Naogopa sana isije nikazaa tena naye kisha akanitupa tena. Nisaidieni kwa mawazo. Nimempeleka kotini kuhusu talaka. Jumanne ni maamuzi kutoka kwa kadhi. Je nirudi kwake? Au atanisumbua?

 

 


 

 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuhama nyumba ya mume wako. Tumesoma swali lako kwa masikitiko makubwa kwa yale yaliyokufikia lakini haya ni maelezo ya upande mmoja kwani hatujapata ulalamishi kutoka kwa upande wa mume. Hata hivyo, tutakupatia nasaha za kijumla kulingana na maelezo yako na tunadhani yatakusaidia.

 

 

Umetaja kuwa mumeo alikuwa na mtoto wa nje ya ndoa naye hakukwambia lakini hili pia ni kosa lako kwani hukuuliza na kama ulifanya hivyo basi hukutueleza. Na kuwa binti huyo alikuwa pamoja naye ni fursa kwako kuweza kumlea ili naye ainukie katika hali nzuri ya Kiislamu. Lakini badala yake ulitoroka nyumbani kwako na hilo ni kosa upande wako kwani zipo njia za kisheria ambazo hukuzitumia. Ilipokuwa hali ni hiyo, ulikuwa ufanye yafuatayo kabla ya kutoka nyumba:

 

 

 

1.     Uzungumze naye kuhusu makosa uliyoyaona.

2.     Ikiwa anaona si kosa basi ulikuwa uitishe kikao baina yako wewe, yeye, wazazi wake na wazazi wako (au wawakilishi wenu). Kikao hiko kingejadili hayo unayoyaona ni makosa, nacho kilikuwa kije na uamuzi wa hilo.

3.     Ikiwa hamkufanikiwa kupata suluhisho ulikuwa uende kwa Qaadhi na ni matumaini yetu kuwa kungepatikana ufumbuzi kuhusu kadhiya hiyo.

 

 

 

Kwa hayo ambayo hukufanya inatakiwa uombe msamaha kwa Allaah Aliyetukuka na kujirekebisha.

 

 

 

Kosa tayari limetendeka kwa upande wako na wazazi wako kukubali kuolewa na mtu ambaye hamkutaka au hamkufanya juhudi ya kumjua kabla ya kuingia katika Nikaah. Lau mngekuwa mmefanya hivyo basi hayo hayangefika kwani mngejua kuwa ana mtoto wa nje ya ndoa na mengineo mengi. Kwa kila hali yaliyopita yashapita na tutazame la kufanywa.

 

 

Hivyo tahadhari ya kwanza ambayo tungetaka kukupa ni kuwa Muislamu hawezi kutumbukia kwenye kosa zaidi ya mara moja ikiwa kweli anaijua dini yake vizuri na kuiheshimu. Tayari umewahiwa mara ya kwanza usijiruhusu kutumiwa na kuwahiwa mara ya pili.

 

 

 

Kurudi kwa mume wako ikiwa amekiri makosa na kuwa na nia ya kujirekebisha ni vyema sana lakini hayo yafanywe kimaandishi. Kwani kwa kurudiana mtaweza kufanya mengi pamoja na kumlea mtoto wenu. Hata hivyo, unatakiwa upate hakikisho hilo kutoka kwake na akuonyeshe kuwa yeye yuko tayari kurudiana nawe, na awe ni mwenye kukulipa gharama zote ulizozitumia katika kulea mimba, kuzaa na kulea mtoto. Ikiwa atakubali kufanya hivyo na kuweza kukubali kuchukua majukumu na kukubaliana katika mambo basi itakuwa vyema kufanya hivyo. 

 

 

 

Kwa mume kutokuangalia sio kuwa umeachika, kuachika ni lazima ima mume atamke kuwa amekuacha au aandike barua ya talaka au uende kushitaki kwa Qaadhi na huko uachishwe. Bila ya kutokea hayo bado wewe unajulikana kuwa ni mke wa mtu. Na kwa kuwa uliondoka mwenyewe nyumbani, mume kisheria si lazima akutazame kwa masurufu yako, wajibu wake ni kumtazama mtoto wake ambaye naye amefanya kosa la kutomtazama.

 

 

 

Kutaka kukurudisha wewe kwake ni jambo zuri lakini inatakiwa muelewane kuanzia mwanzo ili yasikukumbe yaliyokufika. Ikiwa kesi yako tayari iko kotini kwa Qaadhi ni vyema ungojee uamuzi, pia utilie maanani tuliyokueleza. Pia ni muhimu kwako wewe kuswali Swalah ya Istikhaarah kumtaka ushauri Allaah Aliyetukuka kuhusiana na kurudi kwa mumeo.

 

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Alete tawfiki yake na Akupe yaliyo ya kheri kwako katika Dini yako na hatima yake pamoja na maisha yako ya hapa duniani.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share