Nimemkimbia Mume Wangu Kwa Sababu Ya Kunipiga.

SWALI:

 

Asalam aleikum,

 

Leo ni mwezi moja na nusu tangu nimkimbie mume wangu. Nilimkimbia kwa sababu alinipiga. Nimezaa naye mtoto na nilimchukuwa mtoto na mimi. Tangu niondoke, mume wangu haja jaribu kunitafuta wala kumuulizia mtoto wake. Hiyo wiki niliokimbia, wazee wa nyumbani walijaribu kusuluhisha lakini hakuna jibu kutoka kwake. Nilikuwa nataka kujua, kwa sheria ya kislamu mke anafaa kusubiri mwezi ngapi ndio aweze kuomba talaka?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupigwa na mume. Hakika ni kwua dada yetu hukutueleza sababu ya wewe kupigwa na mumeo. Je, ulifanya makosa, ulianza uchokozi au ni vipi? Kwa hali zote mume hafai kumpiga mkewe kipigo cha kumuumiza ila anaruhusiwa kumpiga kipigo kizichotia alama lau atakengeuka maagizo ya Dini baada ya kumnasihi kuhusu hilo na akakataa kurudi katika njia ya sawa.

 

 

Dada yetu umefanya makosa kukimbia katika nyumba ya mumeo. Ilihitajika wewe ufuate njia za kisheria ili kutatua tatizo lako na mumeo. Kukimbia kwako kunaleta bughudha zaidi mbali na kuwa amekupiga. Njia ambazo unafaa uzichukue sasa ni kama zifuatazo:

 

  1. Baada ya hilo tukio ilikuwa ni wajibu wako kuketi na mumeo na kumueleza hisia zako kwa lililotokea ambalo si sawa. Ikiwa anaona alilofanya ni sawa kabisa, basi ungepanda daraja nyingine ya kuelekeza tatizo hilo lako.

 

 

  1. Ni wewe baada ya kufanywa hivyo kuwaelezea wazazi wako kuhusu jambo hilo. Wazazi wako walikuwa waje kwako pamoja na kwuaita wazazi wa mume ili mlizungumzie suala hilo kinaganaga kwa njia ya kutafuta suluhisho. Ikiwa familia zimekuja kwa ikhlaasw na kutafuta ufumbuzi basi kutapatikana suluhisho bila ya wasiwasi.

 

 

  1. Ikiwa hakukutikana suluhisho aina yoyote ile ilikuwa wakati huo ni wajibu wako kwenda kwa Qadhi ili kulalamikia tatizo hilo. Na bila shaka kwa kufuata mfumo huo kungepatikana ufumbuzi wa haraka wa kudumu.

 

Mke anafaa kusubiri kwa muda anaoona kuwa aweze. Pindi anapoona kuwa ameshindwa kuvumilia na mume hamtizami kwa lolote anatakiwa kwenda kuipeleka kesi yake kwa Qadhi ili zijulikane mbivu na mbichi, ima kurudiana kwa wema au kuachana kwa wema.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awaletee suluhisho la kudumu baina yako na mumeo.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share