Damu Ya Hedhi Inayoendelea Kwa Muda Mrefu

SWALI:

asalam alaikum warahma tullahi wabarakatum, mie nina suala  linanitatiza , ukweli mimi nimejaribu kuweka luppu  na madaktari wamenambia inachukua muda wa miezi 3 nitakuwa nableeding na kweli mpaka leo karibu miezi 2 na nusu naendelea kubleeding sasa suala langu hili, kuna watu wamenambia naweza kufunga na kusali nijisafishe  tu haya ni maradhi sio hedhi, na kuna wengine wananambia kuwa siwezi kusali  lkn kufunga naweza sasa nimeshindwa kufahamu lkn mimi nafunga kutoka sijajua ukweli wenyewe,  na pia najiuliza  nafsi yangu  kuwa nafunga bila ya kusali, nakuombeni munisaidie   kwa suala hili linanitatiza sana .inshallah nategemea mtanijibu kwa ufasaha  kwa uwezo wake allah (a.w) inshallah nategemea jibu lenu haraka


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

 

Shukrani kwa Allah kwa kutupatia fursa hii kubwa.

Kwa hakika hii yako ni damu ambayo si ya kawaida na huwa ni ugonjwa kwa hivyo kisheria huitwa Istihadhwa. Na hukumu yake ni kuwa iwapo mwanamke alikuwa kabla ya kuwa na damu hiyo ya ugonjwa, ni mzoefu, na anazijua siku zake za ada yake katika kila mwezi. Katika siku hizo hatafunga wala hataswali. Baada ya kumalizika siku hizo ataoga na ataswali na atafunga na ataingiliwa ikiwa ameolewa.

 

Na akiwa amesahau muda wake au idadi ya siku zake, basi akiweza kupambanua damu, ikawa inatoka mara nyeusi, mara nyekundu, akiona rangi ya kawaida haipo tena na inatoka rangi nyengine ataoga na kutekeleza ‘Ibadah zake zote. Ghalibu ada inakuwa kwa siku 6 au 7 kishaa ataoga na kuswali pamoja na kufunga.

 

Na mwenye damu ya ugonjwa katika siku za kuwa katika hali hiyo atatawadha baada ya kuoga na ataweka kitambara au nguo au padi katika sehemu yake ya siri na ataswali ijapokuwa damu inamiminika kwa nguvu. Ataunganisha Swalah ya Adhuhuri na Alasiri kwa kuichelewesha Adhuhuri na kuiswali mapema Alasiri na hivyo hivyo Magharibi na Ishaa kwa kuichelewesha Magharibi. Na hii ndio njia aliyoipenda Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ahmad].

 

Hivyo, wakati mwanamke anapokuwa ana shida ya kutokwa na damu nyingi anatakiwa aswali na afunge kama kawaida.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share