Maulidi: Kutumia Aayah Nyingi Kuthibitisha Uzushi Wa Maulidi Japo Hayajatajwa Katika Qur-aan

 

Mawlid: Kutumia Aayah Nyingi Kuthibitisha Uzushi

Wa Mawlid Japo Hayajatajwa Katika Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Alekum

Ndugu masheikh naomba kuuliza swali, hivi inaruhusiwa kuitumia Qur-aan utakavo kujibia maswali japo ikiwa matendo au mada haiusiani na sababu za kushuka kwa hiyo aya.  Na kama hairuhusiwi mbona mchezo huu unaendelea na hakuna anayekataza, mbona tunakifanya kitabu chetu kama kinyonga.mfano; utona mtu anakataza maulid halafu anakwenda kutoa aya zisopungua 20, jee ikiwa hayo mauled ya Nabiy s.a.w hajayazungumza, hayakuwepo, vipi tena Quraan inaingia na aya ziloshuka kwa sababu nyengine? Na kuanza kuchambua, jee hivi haya sio makosa? Au inafaa kuzigeuza aya kwa matamanio yetu na kwa kupamba ridhaa za akili zetu.

Shukran

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Qur-aan imeshushwa ili iwe ni uongofu kwa wacha wa Allaah, hivyo basi iko wazi na haina wa kumuonea hayaa wala vibaya wakati inapotaka kuweka sawa na kusahihisha jambo au kukemea tena kwa mtu yeyote yule awe Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au mwenginewe kama amekosea humkosoa na kama ametenda haki humpa haki yake; kwani ni Kitabu kilichonyooka sawa, ili kitoe onyo kali na kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri.

 

Qur-aan ilipoteremshwa wakati mwengine palikuwa na sababu ambayo huitwa Sababun-Nuzuul (Sababu ya Kuteremka Aayah au Surah fulani). Wakati mwengine ambao ndio mwingi hapakuwa na sababu; hata hivyo kinachopasa kueleweka ni kuwa Sababun-Nuzuul huwa ni msingi madhubuti wa kuelewa tafsiri ya hiyo Aayah au Suwrah, si vinginevyo; na wenye elimu ya Qur-aan na yenye kufungamana nayo; The Science of Qur-aan, wanasema hivi kuhusiana na sababu za kushushwa kwa Aayah:

 

"Mazingatio ni katika ujumla wa hiyo lafdhi ya Aayah na sio katika sababu maalumu iliyoteremshiwa Aayah kwa ajili yake."

 

Hii ina maana kuwa hata kama Aayah fulani ilishuka kwa sababu maalumu haina maana kuwa haina hukumu au haiwezi kutumiwa katika tukio jingine lenye kuonekana kuwa linakwenda sambamba na makusudio ya hiyo Aayah, kwani mazingatio huwa katika ujumla wa maneno ya Aayah na sio katika sababu; kwa mfano kauli Yake Aliyetukuka:

 

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾

Basi Naapa kwa Rabb wakohawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu. [An-Nisaa: 65].

 

Aayah hii hata kama itakuwa na sababu ya kushushwa kwake, sababu yake haitakuwa zingatio, bali itakuwa ni yenye kusaidia kuelewa kusudio la hii Aayah na kazi yake itakuwa imekwisha; sasa kama kuna asiyeelewa au asiyeweka sababu ya kushushwa kwake katika tafsiri yake vipi ataweza msomaji kufaidika na lafdhi ya Aayah? Kwa hivyo, hapo ndipo palipokusudiwa kuwa zingatio ni katika lafdhi ya Aayah na sio katika ukhususi wa sababu ya kushushwa kwake; na katika Aayah yetu hapo zingatio liko wazi nalo ni kuwa kinachotakiwa kipatikane kwa Waumini kufikia kuwa Waumini wa kweli na wenye imani itakiwayo imani ya kweli. Si kusema tu nampenda Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au namsifu Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au vinginevyo; bali kuwa Muunimi wa kweli na hichi ndio hasa kinachotakiwa na ndio zingatio la Aayah ni kumfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  kuwa ndie muamuzi katika yale yote wanayokhitalifiana hao wenye kudai kuwa ni Waumini. Vinginevyo imani yao si kamili.

 

Si hilo pekee, bali tunatakiwa tupige hatua ya pili baada ya kumfanya kuwa yeye Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakimu muamuzi tunatakiwa pia turidhike na uamuzi/humuku yake kwa kuufuata na kushikamana nayo kwa moyo mkunjufu na msafi bila ya kuona uzito katika nyoyo juu ya hukumu alizotoa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na cha mwisho chenye kuthibitisha ukamilifu wa imani ya Muumini wa kweli na asiye wa kweli ni unyenyekevu kabisa katika aliyoyapitisha Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hivyo basi ndugu yetu, hakuna katika Uislamu (kauli yako) "kuruhusiwa kuitumia Qur-aan utakavo" kinachoruhusiwa na ndio kinachofanywa na wenye kujibu masuali yako na ya wenzako ni kujibia maswali japo ikiwa matendo au mada haihusiani na sababu za kushuka kwa hiyo Aayah lakini kuna hali yenye kufanana na kwa kuwa zingatio la hiyo Aayah ndio linalotakiwa kueleweka na kufikishwa kwa wahusika.

 

Pia hakuna miongoni mwa wenye kumuamini Allaah na Siku ya mwisho ki kweli kweli wenye (kauli yako) "kukifanya kitabu chetu kama kinyonga" kwani wao wanaelewa kuwa Qur-aan haijaletwa kwa kukidhi matashi yao au kuwafikiana na mitazamo yao bali wanaelewa fika kuwa kishikamana na Qur-aan na Sunnah za Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Sunnah za Makhalifa waongofu wa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio kusudio la Uislamu wote; hivyo kila chenye kuwa na harufu ya kukosekana mambo hayo huwa ni tatizo kwa umma wa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndio hujaribu kwa kadiri ya uwezo wao kutoa Aayah nyingi kadiri wawezavyo kuweza kwa tawfiki yake Rabb kufikisha ujumbe huku wakielewa kuwa wao si wenye kuwatawala wala si wenye uwezo wa kuwalazimisha kitu, bali kinachoweza kuwageuza na kurudi kwa Rabb wao ni Qur-aan ambayo wao wanaogopa maonyo yake. Hivyo basi kutoa hizo Aayah ni kutaka kuwakumbusha tu kama ilivyoshauri Qur-aan kwa kusema:

 

نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ ۖ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِجَبَّارٍ ۖ فَذَكِّرْ بِالْقُرْآنِ مَن يَخَافُ ..﴿٤٥﴾

...Wala wewe si mwenye kuwalazimisha kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur-aan anayekhofu onyo Langu. [Qaaf: 45]

 

Ujumbe wa Qur-aan unabeba dhana nyingi zenye kusudio na lengo moja tu, nalo ni kuamrisha Aliyoamrisha Allaah na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au kukataza Aliyoyakataza Allaah na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo basi kauli yako: "mfano; utona mtu anakataza maulid halafu anakwenda kutoa aayah zisopungua 20." Kama unaelewa sababu za kushushwa kwa hizo Aayah zisopungua 20 zilizotolewa basi una hazina kubwa na kama huelewi basi elewa kuwa lililowapelekea kutoa Aayah hizo ni kile tulichokueleza kuwa zingatio ni katika ujumla wa lafdhi na sio katika ukhususi wa sababu iliyopelekea kushushwa.  Hivyo basi (kauli yako) "ikiwa hayo maulid ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hajayazungumza, hayakuwepo", kilichokuwepo au kilichozungumzwa na ndio hasa wanachotaka kukisisitiza hao watu na kutaka kiendelee kuwepo kwa kila mwenye kudai kuwa anampenda Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kishikamana na Qur-aan na Sunnah za Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Sunnah za Makhalifa waongofu wa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Makusudio yako wazi katika namna ya kumpenda, nako ni kumfuata katika kila kitu katika maisha yetu ya kila siku vinginevyo huwa hatumpendi kwani ameletwa awe riwaza na kigezo chetu.

 

Ndugu yetu katika Uislamu, ushauri wetu ni kuishi na hizo Aayah na kuziangalia kwa utulivu je lafdhi zake zinakwenda sambamba na anachozungumzia huyo mzungumzaji au vinginevyo?  Kama zinakwenda sambamba, basi elewa kuwa alikuwa analenga zingatio la hizo Aayah na si jengine; na kama utaona hazina uhusiano wowote basi vyema umuainishie hiyo Aayah au hizo Aayah na kuthibitisha kuwa hakuna uhusiano wowote ule baina ya Aayah na kinachotaka kuthibitishwa. 

 

Ukishindwa kuthibitisha, basi irejee nafsi yako na akili yako na uelewe kuwa kumpenda  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) si kumsifu, bali kushikamana na mafundisho yake sahihi, hata kama watu wachache tu wanashikamana nayo; na kuachana na yasiyokuwa mafundisho yake sahihi, hata kama yatakuwa yanapendwa na watu wengi; kwani hukumu za Uislamu hazithibiti kwa kisingizio tu kuwa watu wengi wanafanya kitu hicho, hivyo kinakubalika katika dini; bali hukumu na vitendo vyote vya Uislamu huthibiti kwa kuwepo dalili yenye kutokana na mihimili iliyotangulia nayo ni Qur-aan na Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Sunnah za Makhalifa waongofu wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share