Ana Ukimwi Je, Anaweza Kuoa?

SWALI:

 

Assalaam alaykum

 

Nina virusi vya Ukimwi je Sina haki za kisheria kuoa kwa mujibu wa dini? Na kwa kuwa bado nipo fit kiafya na nahitaji kufanya jimai kwa halal Nashauriwa kufanya nini?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuoa kwa mwenye ukimwi. Mwanzo ni maelezo kwa ndugu yetu ya nasaha kabla ya kuingilia swali lenyewe. Na nasaha hiyo itamsaidia kila mmoja wetu kwa njia ambayo ni nzuri sana.

 

Tunataka kukuuliza swali moja ambalo utalijibu mwenyewe bila kurudi kwetu. Swali lenyewe ni je, uliupataje ukimwi huo? Ikiwa umeupata kwa njia ya matibabu kama kutiwa damu au kudungwa sindano itakuwa hulaumiwi kwani hukutaka iwe hivyo.

 

Hata hivyo, ikiwa umeupata ukimwi kwa njia ya uzinzi (zinaa) basi inahitaji urudi kwa Mola wako Mlezi kwa kutubia toba ya kikweli na ya sawa sawa. Uhakika ni kuwa uzinzi ni katika madhambi makubwa katika Dini yetu ya Kiislamu. Inatakiwa ufuate masharti yote ya toba ukiwa katika hiyo unayoiita ya afya kabla hujaaga dunia. Miongoni mwa masharti ya toba ni:

 

1.     Kujuta kwa kufanya kosa hilo.

2.     Kuazimia kutorudia tena kosa hilo.

3.     Kuacha kosa hilo.

4.     Kufanya mema mengi.

 

Tukija katika swali lako ni kuwa tunafahamu kuwa ukimwi ni ugonjwa unaoambukiza kutoka kwa mtu hadi mwingine hasa kwa jimai na njia nyingine. Unapooa ni lazima ufanye jimai na mkeo kwa njia ya halali, njia ambayo upo uwezekano mkubwa sana wa kumuambukiza mkeo, hivyo naye kupata ugonjwa huo. Kumpatia ukimwi mkeo ni dhulma, dhulma ambayo imekatazwa katika Uislamu.

 

Kitu ambacho unaweza kufanya ni ima unapokwenda kuposa useme ukweli kwa wazazi na mwanamke unayetaka kumuoa kuwa wewe una ukimwi. Ikiwa msichana atakubali kuolewa katika hali hiyo itakuwa ni sawa kisheria japokuwa haifai mtu kujiangamiza kwa mikono yake. Aidha pia unaweza kumuoa mwanamke ambaye pia ana ukimwi kama wewe lakini pia baada ya kumueleza hali yako. Kumficha mposa wako kuhusu hali yako ni kosa jingine na dhulma kubwa zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share