Nampenda Sana Lakini Kaposa Kwengine Nisome Du'aa Gani Ya Kumsahau?


SWALI:

Assalam aleykum,

Je nifanye nini? nimetokea kumpenda kakangu wa kiislamu kwa ajili ya imani yake ya dini na vitendo vyake vyema kulingana na dini yetu ya kiislamu. Nilimjuza hilo, lakini alisikitika sana na kunijuzi kuwa ameshachumbiwa tangu kwao, yaani ana mchumba. Basi tuliamuwa kuyasahau hayo na kuendelea na maisha. Tatizo ni kuwa nimejaribu kumsahau lakini mashAllaah kila nikimuona na vile anavyojikurubisha na dini, mapenzi yanazidi na hadi nashindwa kuficha, na ninahakika kuwa hilo yualitambua. Sitaki kumuharibia uchumba wake, lakini pia ningependa na mimi pia niolewe na yeye. Najitahidi kumuomba Allaah anisahalishie, ila nashaindwa jinsi ya kuomba dua,yaani nia yangu iwe nini?

 

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Hili ni suala la kawaida ambalo linawatokea watu wengi wanaume kwa wanawake. Huenda mwanamme akamuona msichana ambaye ameridhika naye lakini anapokwenda kuposa akakuta tayari ameposwa. Hivyo hivyo kwa wanawake ambao wanaona kuwa mwanamme fulani ana sifa ambazo anaona wanaweza kuishi pamoja kama wanandoa lakini anapotuma salamu kutaka yule mwanamme aje amuoe anapkuta kuwa tayari ameposa kwengine. Japokuwa kwa mfano hakuna tatizo lau mwanamke ataelewana na mwanamme kuwa yeye hana neno anaweza kuwa mke wa pili wake. Na hilo ni jambo linalowezekana.

 

Huko kuyaamua kuyasahau nyote wawili ni jambo ambalo mumeafikiana lakini ipo fursa ya kuwa pamoja lau utaridhika ndugu yetu huyo aoe kwao na akuoe na wewe ili ile ndoto yako ya kuwa pamoja na kijana mwenye dini kama huyo itimie. Na hata ikiwa una uwezo unaweza kumsaidia katika mambo mengine ya kinyumbani na hilo ni jambo ambalo linakubaliwa ikiwa wewe mwenyewe utaridhia hilo.

 

Ni vigumu kumsahau mara moja hivi mtu ambaye alikuwa moyoni kwa muda mpaka ukadhania kuwa siku moja mutakuwa pamoja kama mume na mke mukiishi katika nyumba moja na kusaidiana katika kujenga maisha yenu ya hapa duniani na Kesho Akhera. Hilo si jambo rahisi lakini baada ya muda litakuwa ni lenye kutoka haswa unapopata mchumba mwengine. Tatizo linatokea kwa kuwa hujapata mwingine ima uliyemuona akakuridhia au aliyekuja kutaka kukuposa nawe ukaridhika na Dini yake pamoja na maadili akiwa kama yule wa kwanza au pengine zaidi yake.

 

Sasa ikiwa unaona kuwa kwako wewe kuolewa na yeye ndio kheri yako basi inabidi uswali rakaa mbili. Katika kufanya hivyo inatakiwa utawadhe vizuri kabisa, kisha usimame kuswali rakaa mbili zisizo faradhi, Swalah ijulikanayo kama ‘Swalaatul Istikhaarah’

Baada ya Swalah umuombe Allaah Aliyetukuka kwa Du’aa ambayo ipo katika vitabu vingi na hata katika kijitabu kidogo kinachoitwa HISWN AL MUSLIM. Katika hiyo Du’aa unaomba ikiwa huyu mwanamme ndiye kheri yangu katika Dini na maisha yangu na hatima yake nisahilishie kumpata na ikiwa ni shari kwangu katika Dini na maisha yangu na hatima yake basi niepushe naye. Hii ni Swalah ya Istikhaarah, kumtaka shauri Aliyetukuka.

Soma viungo hivi upate kujua zaidi kuhusu Swalah ya Istikhaarah na pia Du’aa yake:

Kwa Nini Tuswali Istikhaarah Na Iswaliwe Kwa Ajili Ya Nini?

Muda Wa Swalah ya Istikhaarah

Tunakuombea usahali na wepesi katika amali yako hiyo yote na Allaah Aliyetukuka Akufanyia kila lililo la kheri pamoja na Waislamu wengine, Amiin.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share