Mume Hatoi Haki Kwa Mke Wa Pili Kama Atoavyo Kwa Mke Wa Kwanza

SWALI:

 

Mimi ni Mama wa Watoto 3, niliolewa mke wa pili miaka 21 iliyopita na mume alikuwa ni muadilifu sana lakini tatizo miaka 2 na miezi 6 iliyopita ameasi kwangu hana uadilifu tena yeye na kwa bi mkubwa tu. Wakati mwingine hata mwezi unapita bila ya kuja nyumbani kwangu.

 

Hakija hapo nyumbani anakaa hata saa moja haifiki anaaga hata haki zangu za msingi za Ndoa sizipati na nikimuuliza anakuwa mkali sana hadi inakuwa ugomvi, hataki kuitikia wito anaoitwa ili tusuluhishe tatizo ambalo mie silijui. Ila nasikia anasema ananiona mimi kama mdudu.

 


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutopewa haki zako na mumeo.

Mwanzo ni kukunasihi dada yetu uwe na subira wakati unatafuta suluhisho kwa tatizo lililoibuka baada ya muda mrefu sana wa kuoana. Inatakiwa awali ya yote utizame wakati mzuri wa kuzngumza na mumeo kwani mumeishi miaka mingi mtakuwa mnajuana vizuri sana.

 

Zungumza naye kwa njia ya hekima na busara na upole. Ikiwa atakuwa amefanya zogo au fujo basi itabidi uitishe kikao baina yako, yeye, wawakilishi wa watu wako (kwa mfano wazazi au jamaa zako) na wazazi wake au wawakilishi wake. Twatumai kwa kikao hicho kutapatikana suluhisho la kuridhisha inshaAllaah.

 

Ikiwa kwa kufanya hivyo hakukupatikana suluhisho aina yoyote ile itabidi uende ukashitaki kwa Qaadhi wa mji mnaoishi, Imaam muadilifu wa Msikiti au Shaykh anayejulikana kwa ucha Mungu wake.

 

Twatumai kwa kufuata njia hizo kutapatikana muelekeo na ufumbuzi wa tatizo hilo kwa uwezo wake Allaah.

 

Twakutakia kila la kheri na ufumbuzi mzuri katika tatizo hilo inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share