Mashairi: Siku Ya Mama? (Mother's Day)

 

 'Abdullaah Bin 'Ifaan (Rahimahu Allaah) 

 

Alhidaaya.com

 

 

Mijini na vijijini, salamu zangu natuma,
Ameshafika shetani, ameanza kunguruma,
Jina lake kwa yakini, MOTHER'S DAY imevuma,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Mama sio siku moja, anakumbukwa daima,

Tuishi nae pamoja, kwa mapenzi na heshima,

Tutimize zake haja, tena bila kulalama,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Ona leo makafiri, hawaogopi lawama,

MOTHER'S DAY wanakiri, ni siku ya ta’adhima,

Ni upuuzi wa dhahiri, sisi tusifuate nyuma,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Miezi tisa tumboni, kakubeba kwa huruma,

Daima yupo mbioni, anakwenda kujipima,

Raha katu haioni, hutapika ana homa,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

Wakati ukishafika, baba anafanya hima,

Hospitali kumpeleka, azae kwa usalama,

Mambo pilikapilika, anaombewa uzima,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Sasa ukishazaliwa, mama huanza huduma,

Akunyonyeshe maziwa, daima hukutazama,

Usiku, mchana kutwa, usingizi kumnyima,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Yupo anahangaika, mwana anamuandama,

Anabaki kuteseka, huoni akiroroma,

Kila kitu anaweka, vitu vyote vya lazima,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Mama tena kisha mama, mara ya tatu ni mama,

Kwa wazazi fanya wema, hivyo Mola Amesema, (Al-Israa: 23)

Radhi zote za Rahima, zipo pamoja na mama,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Dini yetu safi sana, ni dini yenye hekima,

Sharia utaiona, ipo wazi ukisoma,

Radhi Zake Maulana, usikose kuzichuma,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Radhi za mama kukosa, hapo ndugu utakwama,

Na pepo hutaigusa, na moto utakuchoma,

Utakumbwa na mikasa, na mengi yatakuuma,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

Mwisho hapa nimefika, na shairi kaditama,

Namuomba Mtukuka, tupate Zake rehema,

Zisije kutuponyoka, tukazikosa neema,

Anakumbukwa daima, Mama sio siku moja.

 

 

 

 

Share