Kwa Nini Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatumia Neno ‘Sisi’, Au ‘Tuta...’ Na Hali Yeye Hana Mshirika?

 

Kwa Nini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatumia Neno 'Sisi',

Au 'Tuta....' Na Hali Yeye Hana Mshirika?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam aleykum.

 

Mimi Nina Swali Kuhusu Mada Hii Mpya Ya Madhara Ya Chumo Laharam. Kama Ilivyoandikwa Kama “enyi Mlioamini Msiliane Mali Zenu Kwa Batili.  Isipokua Iwe Biashara Ya Kuridhiana Baina Yenu. Wala Msijiue (wala Msiue Wenzenu) Hakika Allaah Ni Mwenye Kukuhurumieni. Na Atakae Fanya Hayo Kwa Uadui Na Dhulma Basi Huyo ''tuta Muingiza Motoni''. 
 
Swali Langu Ni Hivi, Inakuaje Linatumika Neno ''tuta'' Kwa Wingi Wakati Allaah Ni Mmoja? Na Sio Mada Hii Pekee Inayosema Hivyo. Hata Ninaposoma Tafsir Za Kuran Huwa Nikikutana Na Neno Hilo Au Neno ''tuli'' Je Inamaanisha Vip?
 
Nitashukuru Mkiweza Kunielimisha Hapo. Allaah Awajaalie Kheri Ya Hapa Duniani Na Kesho Akhera Kwa Kazi Njema Mnayoifanya. Shukran
 

 

 JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ni kweli maneno hayo yanatumiwa na Allaah Aliyetukuka ndani ya Qur-aan yanayomaanisha wingi. Sasa wengi kati yetu tunakuwa na utata mkubwa, vipi Allaah Aliyetukuka hana mshirika lakini Anatumia wingi katika kauli Zake?

 

Hakika ni kuwa hakuna utata wowote katika hilo kwani ni tabia ya utumizi wa lugha nyingi ikiwemo Kiarabu, Kiingereza na hata Kiswahili. Wingi huu katika Lugha ya Kiarabu unaitwa Jam’u Litta’dhwiym (wingi wa utukufu na ukubwa). Wingi umegawanyika sehemu mbili – wingi kama wingi na wingi wa utukufu. Wingi unaotumika katika Qur-aan kwa Allaah Aliyetukuka ni huu wingi wa utukufu na ukubwa.

 

Katika lugha ya Kiingereza inaitwa The Majestic We. Mara nyingi wakubwa na watukufu kama Raisi, Mfalme, Malkia, Waziri mkuu anapoandika barua au anapohutubia watu husema sisi ilhali makusudio ni yeye peke yake. Sasa hawa sisi ni kina nani na ilhali ni yeye peke yake? Bila shaka ndiyo hayo hayo matumizi ya kutumia wingu wa utukufu.

 

Na katika Kiswahili, pia utamkuta mzee anasema akimwambia mtoto wa mtu mwengine, sisi tumekulea ilhali yeye hakumlea wala hakushirikiana na wazazi wa mtoto katika hilo. Huo ni wingi wa ule ukubwa wake wa umri.

 

Na ndivyo katika Qur-aan, Allaah Anatumia wingi huo wa utukufu Naye hakuna anayemfikia hata kumkaribia katika ukubwa na utukufu Wake.

 

Na Mara nyingine katika Qur-aan Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hutaja hivyo pale kitendo kinapohusiana na Malaika wanapotumwa kufanya jambo. Mfano Anapotuma Malaika kuangamiza mji Anataja kwa wingi kwa maana Yeye Subhaanahu wa Ta’aala Ndiye Aliyetuma Malaika kufanya kitendo hicho kama ilivyo katika mifano ifuatayo:     

 

فَكَذَّبُوهُ فَأَهْلَكْنَاهُمْ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣٩﴾

Wakamkadhibisha; basi Tuliwaangamiza. Hakika katika hayo pana Aayah (ishara, zingatio n.k.), lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. [Ash-Shu’araa: 139]

 

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي أَيَّامٍ نَّحِسَاتٍ لِّنُذِيقَهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَخْزَىٰ ۖ وَهُمْ لَا يُنصَرُونَ﴿١٦﴾

 Basi Tukawapelekea upepo wa dhoruba na mngurumo katika siku za mikosi ili Tuwaonjeshe adhabu ya hizaya katika uhai wa dunia; na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni ya hizaya zaidi, nao hawatonusuriwa. [Fus-Swilat: 16]

 

Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Ameupiga vita ushirikina katika njia zake zote na Akafunga milango yote ambayo itampelekea kuja karibu na ushirikina huo. Ushirikina unaharibu ‘amali na unamuingiza sahibu wake Motoni. Hivyo, Akasema:

 

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ ﴿١﴾

Sema: Yeye ni Allaah Mmoja Pekee. [Al-Ikhlaasw: 1]

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share