Tafsiyr Ya Aayah: Na Tukajaalia Kutokana Na Maji Kila Kilicho Hai

 

Tafsiyr Ya Aayah: Na Tukajaalia Kutokana Na Maji Kila Kilicho Hai

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Nnaomba maelezo na mafundisho kutoka katika aya "Tukajaalia kutokana na maji kila kitu kilicho hai.”

Maombi samahani sikuweza kuziandika aya hizo kwa lugha ya kiarabu.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

..وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ ۖ أَفَلَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٠﴾

"Tukajaalia kutokana na maji kila kitu kilicho hai. Je, basi hawaamini?  [Al-Anbiyaa: 30]

 

Mara nyingi hushindwa kuielewa Aayah hii tunapochukulia kwa ule ufahamu wetu kuwa hasa sisi binadamu tumeumbwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)kwa udongo kama inavyosema Aayah:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾

Kwa yakini Tumemuumba insani kutokana na mchujo safi wa udongo. [Al-Muuminuwn: 12]

 

Na ifahamike huku kuumbwa kwa binadamu wa kwanza ilikuwa ni mchanganyiko wa udongo na maji, na ama baada ya hapo mwanadamu huyo anatokana na maji yenye kuchupwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema: " Kisha Tukamjaalia kuwa tone la manii katika kalio makini." [Al-Muuminuwn: 13]. Inafahamika kuwa manii ni maji.

 

Ama tukirudi katika Aayah hii maana yake ni kuwa kila kitu kimeumbwa kutokana na maji. Haya ni kama alivyosema Ibn Kathiyr katika tafsiri yake: "Imaam Ahmad amepokea kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliyesema: 'Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah, ninapokuona ninafurahi na kuridhika, niambie kuhusu kila kitu'. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kila kitu kimeumbwa na maji".

 

Kwa hiyo viumbe vyote vimeumbwa kwa maji na vitu vingine na baada ya hapo kitu muhimu katika uumbaji ni maji yanayotoka kwa mwanaume na kuingia kwa mwanamke.

 

Elezo la pili ni kuwa maji ni muhimu sana katika maisha ya viumbe kwa jinsi ya kwamba ukosefu wa maji kunamfanya yule kiumbe asiweze kuishi hapa duniani. Mwanadamu mwenyewe ambaye ni kiumbe bora thuluthi mbili ya mwili wake ni maji. Na sayari nyingine hakuna uhai kwa ajili ya ukosefu huu wa maji yaliyo muhimu katika amali za mwanadamu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share