Mtu Asiyeswali Na Anayekanusha Uwajibu Wa Swalaah Kuitwa Kafiri

 Mtu Asiyeswali Na Anayekanusha Uwajibu Wa Swalaah Kuitwa Kafiri

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 

In Shaa Allah Allaah awajalie kila la kheri. Ninataka kuuliza kuhusu hukumu ya mtu aliacha swalah. Katika mawaidha yaliotolewa na Sheikh Naasir Bachu ameeleza kuwa mtu aliacha swalah ni kafiri na hukumu yake kuuwawa. Swali langu ni Kama makafiri ambao hawakuamini Uislam hawapasi kuuwawa, vipi muislam aleye iacha swala auwawe.

 

Tashukuru sana kama mtanifafanulia zaidi. In Shaa Allaah, Allaah atuongeze katika haki. Amini 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kulingana na suali lako, makafiri ambao hawakuamini Uislamu hawapasi kuuawa, vipi Muislamu aliyeacha Swalaah auawe?

 

Ni kwa sababu kafiri halazimishwi kuingia katika Uislamu kama alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٥٦﴾

Hapana kulazimisha katika Dini, kwani imekwishabainika kati ya uongofu na upotofu. Basi atakayemkanusha twaghuti na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah: 256]

 

Lakini mtu akishasilimu au akiwa ni Muislamu harusiwi tena kutoka.  Dini si kitu cha mchezo, mtu kuingia na kutoka atakavyo. Mwenye kutoka katika Uislamu huitwa “murtad” na hukmu yake ni kuuliwa. Kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

  ‏((‏من بدل دينه فاقتلوه))

Mwenye kubadilisha Dini yake (ya Kiislamu) muueni.”  [Al-Bukhaariy (6922), Abu Dawuwd (4329), At-Tirmidhiy (1483)]

 

Ama kuhusu mtu asiyeswali (Taarikus-Swalaa), ‘Ulamaa wame wagawanya vikundi viwili:

 

i-Mwenye kuacha kwa kukanusha uwajibikaji wa Swalaah; huyu ni kafiri kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote.

 

 

ii-Mwenye kuacha kwa uvivu au kwa kupuuza pamoja na kuwa anaamini kuwa Swalaah ni nguzo miongoni mwa nguzo tano za Kiislamu, na kuwa ni wajibu kwake kuswali.

 

Huwa yeye ni kafiri. Wamethibitisha kauli yao hii kwa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

((بين الرجل وبين الشرك والكفر ترك الصلاة)) مسلم

“Baina ya mtu na ukafiri na shirki, ni kuiacha Swalaah.” [Muslim]  

 

Na pia akasema:

 

 ((‏إن العهد الذي بيننا وبينهم الصلاة فمن تركها فقد كفر)) أحمد

“Ahadi ambayo iko baina yetu na baina yao (makafiri) ni Swalaah, na mwenye kuiacha basi amekufuru. [Ahmad]  

 

 

Kuwa ni ‘aasw (mwenye kuasi) au faasiq (fasiki). Kwa kuwa mara anaswali na mara anaacha, anaswali kwa wakati anaotaka yeye, kwa kuchelewa kuswali bila ya sababu za ki-Shariy’ah, na kadhalika. Kikundi hiki wamethibitisha maneno yao kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾ الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾

Basi Ole kwa wanaoswali  Ambao wanapuuza Swalaah zao. [Al-Maa’uwn: 4 – 5]

 

Hivyo, akiwa mtu yu katika kundi hili atakuwa bado hajatoka katika Uislamu na anaporudi kutekeleza ibada huwa hana haja ya kutoa shahada nyengine.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share