Zingatio: Elewa Maana Ya Maandishi Kwenye Kivazi

 

Zingatio: Elewa Maana Ya Maandishi Kwenye Kivazi

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Miongoni mwa tofauti kubwa ya Uislamu na imani nyengine ni kuweka muongozo wa kila kitu katika dira la Kiislamu lililo kamili na lenye kwenda pamoja na maumbile ya mwanaadamu.

 

 

Hutakuta jambo ambalo ni la msingi, Uislamu ukawa umeacha kutoa tamko lake. Uchumi, siasa, jamii; vyote vinaangukia ndani ya mwenendo mzima wa Uislamu. Ni kusema kwamba, Uislamu upo kamili usiotaka kujifunza katika mambo yasiyo maana kutoka kwenye imani nyenginezo!

 

 

Baadhi ya mambo ambayo Waislamu wamegubikwa nayo sana katika jinamizi la ujinga ni kivazi. Wengi hawaelewi kivazi anachotakiwa kukivaa Muislamu. Inafika wakati Muislamu anataka fatwa (jibu) ya kivazi cha kidani kwa mwanamme?? Ni suala ambalo linamuacha mdomo wazi Muislamu anayeelewa mafundisho ya Uislamu kwamba ni haramu kuchanganya kivazi baina ya mwanamme na mwanamke.

 

 

Tuingie katika mada yetu ambayo ni maandishi kwenye kivazi cha Muislamu. Ni sikitiko na pigo kubwa kwa jamii ya Kiislamu kutotilia mkazo kile kinachovaliwa katika mwili wa Muislamu. Fulana za aina wa aina zinavaliwa tu bila ya kufuata msingi wa Uislamu. Alimuradi fulana imependeza mbele ya macho yake na ikawa inaenda na wakati, basi hilo ndio chaguo lake.

 

 

Basi tambuwa kwamba CARLSBERG ni pombe na kila mwenye kuitangaza anatakiwa kujitayarishia jibu mbele ya Hisabu. Pia elewa kwamba NIKE ni mungu wa kike wa Kigiriki na kila mwenye kuvaa anaridhia kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Fahamu pia kwamba JESUS ni yule wanayemuitakidi Manaswara kwamba ni mtoto wa Allaah na kila mwenye kuvaa kinachotokana nacho anaenda sambamba na Unaswara. Kubali kwamba SOS linasimama kwa maana ya Sword Of the Spirit (Upanga Wa Roho) [Ephesians/Waefeso, 6:17]. Na kila kinachowafikiana na BIBLIA, kwa mfano maandiko yake kwenye fulana basi yawajibika kuepukwa.

 

 

Wapo baadhi ya ndugu zetu wanafikia kuvaa fulana za matusi na inakuwa ni karaha mbele ya kadamnasi za watu. Yawezekana haelewi maana yake, lakini dhimma bado inabaki na kwanini asiulize kabla ya kuivaa?!

 

 

Halikadhalika wapo baadhi ya Waislamu wanaopoteza fedha zao kwa kununua kivazi cha timu fulani. Mwenendo mzima wa maisha yake unakuwa umejaa maandiko ya timu hiyo, kuanzia taulo, vitambaa vya gari, fulana, suruali na hata nguo za ndani! Ukoloni huu unaenezwa pia kwa kuwavalisha watoto wasiotambuwa hata kutamka 'mama' nembo ama jina la timu anayoishabikia.

 

 

Iwapo Waislamu hawaelewei - Nembo za timu za mpira: Timu za Taifa za Uingereza na zile za Scandinavia zote jezi zao zina Msalaba, LIVERPOOL ina alama ya msalaba na isitoshe matangazo ya pombe, dragon na picha ya moto, MANCHESTER ina picha ya dragon, ARSENAL ina alama ya bomu lenye duara la tundu sita, na isitoshe wana baadhi ya hisa na Mayahudi, CHELSEA ina picha ya dragon na duara la ua lenye tundu sita. Basi tambua kwamba picha ya dragon, moto, msalaba, duara na mfano wa hayo ni miongoni mwa alama za Umasoni!

 

 

Kinamama nao wanatengenezewa Hijaab zenye nembo za mashirika ya Mayahudi - CK (Calvin Klein) - na wao wanajiona wamevaa brand na wanakwenda na wakati!

 

 

Ni jukumu la kila Muislamu kuachana na vivazi vya kijahili na pia kumuamrisha mwenziwe kuachana na kivazi kinachoenda kinyume na Uislamu, na kwetu sisi hilo tumelifikisha.

 

 

Rabb wetu! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kutuongoza, na Utupe rehema itokayo Kwako; hakika Wewe ndiwe Mpaji mkuu.

 

Share