Zingatio: Uchaji Allaah Ndio Siri Ya Mafanikio

 

Zingatio: Uchaji Wa Allaah Ndio Siri Ya Mafanikio

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

Nakuusieni pamoja na nafsi yangu katika jambo la kumcha (kujichunga na makatazo Yake na kutii amri Zake) Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika kila jambo. Kwa sababu kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni silaha bora kupita zote mbele ya kitu chochote.

 

Nayo ni njia nyepesi ya kuipata elimu na pia ni mbinu bora yenye nguvu kupita zote katika Jihaad. Tujichunge tusije kufanya maasi, kuliko tunavyomchunga adui yetu, kwa sababu madhambi yetu yana hatari zaidi kupita adui. Kwa hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) huwapa ushindi Waislamu kwa sababu maadui ni watu wenye kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ama sivyo sisi hatuna nguvu za kuwashinda, kwa sababu idadi yao ni kubwa kuliko idadi yetu, na silaha zao ni kali kupita silaha zetu.

 

Kwa hivyo tukiwa sawa nao katika kufanya maasi, basi wao watatushinda kwa nguvu zao, kwa sababu tunapewa ushindi kutokana na fadhila zetu na si kwa nguvu zetu.

 

Na tutambue kwamba katika safari ya maisha yetu kuna Malaika wenye kuhifadhi, wanaojua kila tunalotenda, kwa hivyo tuwaonee hayaa, na tusiwe wenye kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na wala tusiseme kuwa: ‘Kwa vile adui zetu wana shari kupita sisi, kwa hivyo hawataweza kupewa ushindi juu yetu,’ kwani huenda watu wakasalitishiwa (wakapelekewa) na kushindwa na adui aliye mbaya kupita wao kama pale Bani Israaiyl walipomuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akawapelekea Majusi (wanaoabudu moto) wakaingia mijini mwao kila upande, ikawa ahadi iliyoyotimizwa.

 

Tumuombeni Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atusaidie katika nafsi zetu kama tunavyomuomba Atupe ushindi juu ya adui zetu.

 

REJEO: Wasia wa 'Umar bin Khattwaab kwa Sa’ad bin Abi Waqaas pamoja na maaskari wengine (Radhiya Allaahu ‘Anhum).

 

Share