Mume Amemrudia Baada Ya Talaka Ya Pili Lakini Hana Raha Naye Tena, Je, Anaweza Kuomba Talaka?

Mume Amemrudia Baada Ya Talaka Ya Pili   Lakini Hana Raha Naye Tena,

Je, Anaweza Kuomba Talaka?

 

 

SWALI:

 

asalam aleykum warahmatuh llahi wabarakatuh.

 

mume wangu kaniacha sasa ni talaka ya pili. ilipofika wiki mbili akarudi kuniregelea mimi nikawa sitaki. akaniambia mimi sikuja kwa ubaya nimekuja kwa uzuri. nikawa sitaki akanirahi, kwa imani yangu na pia ni babayo watoto wangu nikakubali. nimeketi nae siku tatu roho yangu ikawa haitaki tena kuishi nae. sasa naweza kuomba talaka nipewe? naomba msaada kwenu.

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho 

 

 

 

Kulingana na swali lako umetuelezea  kuhusu talaka bila kututajia sababu ya mumeo kutoa talaka. Hata hivyo, inaonyesha kuwa maisha yenu mbali ya kuwa mumezaa watoto hayako kama yanavyotakiwa kuwa. Wanandoa wanatakiwa waishi katika hali iliyo njema ya kuelewana na kufahamiana kwa kiasi kikubwa. Na hata kukiwa na tatizo basi wakae chini ili watatue matatizo hayo kama wanandoa.

 

 

Kwa wakati huu tunaomba mwanzo uondoe wazo lako kutaka kuachwa kwani si niyyah nzuri. Ikwia mumeo amekuja na kukuelezea ya kwamba tuache yaliyopita na tuganje yajao inatakiwa uchukue hilo kwa nia safi na moyo mkunjufu. Na lau atakuwa si mkweli basi yatahidhihirika hayo kwa wakati mfupi na hamtaweza kuishi pamoja. Na ujue kuwa hiyo nafasi ya pekee ambayo mumeo anayo, kwani akikupatia tu talaka hatoweza kukurudia tena mpaka uolewe na mume mwengine kisha akuache. Ondoa kinyongo katika moyo wako kuhusu mumeo ili mpate kuendelea vizuri katika unyumba wenu.

 

Hata hivyo, ikiwa kweli wasikia kinyongo inatakiwa uchukue hatua zifuatazo:

 

1.  Jaribu kukaa na mumeo mzungumze kwa uwazi kama wanandoa lakini bila ya kumpigia makelele bali utumie Lugha nzuri na ya upole. Inatakiwa uwe wazi kwa yale unayoyahisi. Na umpe nafasi naye aweze kujieleza kwa nini naye anafanya anayoyafanya kwa kutoa talaka ovyo bila kutafakari.

 

 

 

2.  Ikiwa kikao chenu kimekwenda vyema itakuwa ni vyema na lau hamtaelewana basi itabidi uwashirikishe wazazi wako na wake ili mpate suluhisho kwa kinyongo unachosikia. Ikiwa kweli mnataka maslahi basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala)   Atawapatia ufumbuzi wa haraka kwa matatizo mliyo nayo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا ﴿٣٥﴾

 Na mkikhofu mafarikiano baina yao wawili, basi pelekeni mwamuzi kutoka watu wa mume na mwamuzi kutoka watu mke. Wakitaka sulhu Allaah Atawawafikisha baina yao.  Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 35]

 

 

 

3. Ikiwa hamkufanikiwa kwa hilo, itabidi uende kwa Qadhi au ikiwa hayupo hapo unapoishi umtafute Shaykh aliyewaozesha au Shaykh mwengine mwenye elimu, mwenye taqwa na uadilifu ili aweze kuwasikiliza katika hayo.

 

 

4. Pia usisahau kuswali Swalaah ya Istikhaarah.

 

 

Kwa kufanya hayo bila shaka utapata ufumbuzi kwa shida uliyo nayo.

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share