Maulidi: Wanafunzi Wa Madrasa Wanachangishwa Pesa Kwa Ajili Ya Maulidi Mwalimu Hataki Kupokea Nasaha

 

Wanafunzi Chuoni Wanachangishwa Pesa Kwa Ajili Ya Mawlid Kuvalishwa Sare.

Mwalimu Hataki Kupokea Nasaha Ya Mzazi Kuhusu Mawlid

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Watoto wangu watatu wanawake wamekuja na vitambaa vya sare wamepewa na mwalimu wao wa kuraan kama ni sare ya maulid pia wametakiwa kutoa mchango wa pesa kwa ajili ya kununuliwa vyakula baada kusomwa hayo maulidi. Tulijaribu kumfahamisha huyu mwalimu kupitia wanafunzi wake lakini yeye alisema ni bidaa baadhi ya milango katika maulid sheikh tunaomba kupitia mtandao huu wa al hidaya utupe maoni yako ili kufikishia mwalimu huyu ambaye kwa kweli yuko katika mstari wa mbele katika kusomesha watoto quraan.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Mara nyingi watu hasa walio wasomi wanakosa kufuata rai na nasaha tu kwa kuwa labda hazikutolewa kwa njia nzuri au anaona kuwa hakuna anayeweza kumpatia yeye nasaha kama mwalimu au Shaykh.

 

 

Hapa kosa lililofanywa ni kwa wazazi kuwatuma watoto waende wampe nasaha mwalimu wao. Katika hali ya kawaida mtoto ambaye ni mdogo au hata akiwa ni mkubwa kidogo anaweza kushindwa kutumia njia muafaka kabisa katika kutoa nasaha. Ima anaweza kutoa nasaha sivyo, au akashindwa kufikisha ujumbe au mwalimu akakataa kumsikiliza kuhusu hilo. Ilikuwa ni vyema na busara zaidi kama nyinyi wazazi ndio mngekwenda ili kuzungumza na mwalimu huyo kwa njia ya upole, busara na utaribu ulio mzuri ili kumfahamisha kuhusu hilo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuhimiza sana kuhusu utumiaji wa njia muafaka, upole na busara katika Da‘wah.

 

 

Wakati wa kuzungumza naye inatakiwa mumueleweshe mwalimu kuwa Mawlid si katika Dini na kumpatia dalili zake kutoka katika Qur-aan na Sunnah kama zilivyotajwa baadhi yake katika makala ifuatayo:

 

Sababu 35 Muislam Asisherehekee Maulidi

 

 

Na badala ya watoto kutumia wakati mwingi kujitayarisha na sherehe hizo wanafunzi wangekuwa wanafaidika na kuhifadhi Qur-aan zaidi na masomo mwengine ya Kiislamu ambayo yatawasaidia watoto katika maisha yao ya hapa duniani na Aakhirah.

 

 

Pia mjue nyie wazazi mnatakiwa mjishughulishe moja kwa moja katika maendeleo ya Madrasah pamoja na kumpatia ushauri mzuri mwalimu kuhusu mambo tofauti ili watoto wapate kufaidika. Yapo mambo mema na ya faida zaidi yanayoweza kufanya kwa pesa zilizokusanywa badala ya kuwanunulia watoto sare na kutoa mchango wa chakula. Je, umuhimu wa Mawlid ni chakula au Waislamu kufunzwa kwa njia nzuri zaidi jinsi ya kufuata maagizo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Tufahamu kuwa huko kusema ni baadhi ya milango ndio haifai ni kujitia katika mashaka na taabu kwani tutakuwa tunapoteza wakati mwingi ima wa kutunga Mawlid yetu au kuchambua yale yaliyoandikwa na kisha kutoa. Kwa nini tupate shida yote hiyo ni afadhali kwa kiasi kikubwa kuyaacha kabisa.

 

 

Twawatakia tawfiki katika kuzungumza na mwalimu wa watoto wenu kuhusu hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share