Kupiga Makofi Katika Mihadhara, Kongamano Na Sherehe

 

Kupiga Makofi Katika Mihadhara, Kongamano Na Sherehe

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Nini hukumu ya kupiga makofi wanaume wanapokuwa wanapongeza mtu au kushangilia jambo kama tunavoona ktk mihadhara, makongomano, semina, mijadala na midahalo ya dini? Hili limekuwa jambo la kawaida hata ktk TV za Kiislamu tunazoona.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:  

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ

Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. [Al-Anfaal: 35]. 

قال الرسول صلى الله عليه وسلم: (مَنْ نَابَهُ شَيْءٌ فِي صَلَاتِهِ فَلْيُسَبِّحْ فَإِنَّهُ إِذَا سَبَّحَ الْتُفِتَ،، و إِنَّمَا التَّصْفِيقُ لِلنِّسَاءِ). رواه البخاري (684) ومسلم (421)

"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayetanabahi kitu katika Swalah yake, alete tasbiyh [Aseme Subhaana-Allaah] kwani anapoitamka, humvutia mtu atanabahi, na hakika kupiga makofi ni kwa ajili ya wanawake))." [Al-Bukhaariy (684), Muslim (421),]

 

Imeulizwa kuhusu tafsiyr ya:  

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ

Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. [Al-Anfaal: 35]

 

 

Imaam ‘Abdul-’Aziyz bin Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:

 

Hiyo ni Swalaah ya watu wa jaahiliyyah yaani makafiri wa ki-Quraysh na waliyokuwa wakifanya ya miruzi na kupiga makofi. Ikawa ada yao kupiga makofi kwa mikono na kupigia miruzi wakaharamishwa Waislamu vitendo kama vyao. Kwa hiyo haimpasi Muislamu apige miruzi au makofi katika ‘ibaadah zao wala katika Masjidul-Haraam wala katika vitendo vyake vinginevyo, bali kupiga makofi ni kwa ajili ya wanawake. Ama mwanamme aseme anapotanabahisha jambo; alete tasbiyh katika Swalaah: Subhaana-Allaah! Subhaana-Allaah!  Wala asitumie miruzi, bali atamke maneno yanaohitajika bila ya miruzi.

 

 

Swali:

 

Nini Hukmu Ya Watu Kupiga Makofi Katika Sherehe, Matukio Na Mihadharah Na Makongamano?

 

Kupiga makofi ni katika vitendo vya ujaahiliyyah na hukmu ya chini kabisa ni jambo ka kuchukiza na lililo dhahiri kabisa katika dalili ni kuharamishwa kwake kwa sababu Waislamu wamekatazwa kuigiza makafiri, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika kuwaelezea makafiri wa Makkah:  

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ

Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. [Al-Anfaal: 35].

 

 

Wanavyuoni wamesema: ‘Al-Mukaa’ ni Miruzi na ‘At-Taswdiyah’ ni kupiga makofi. Na Sunnah kwa Muumini ni kwamba anapoona au kusikia jambo linalompendeza au linalomchukiza aseme: “Subhaana-Allaah” au aseme:  “Allaahu Akbar” kama ilivyothibiti kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth nyingi. Na imeruhusiwa wanawake kupiga makofi hasa wanapotanabahisa kitu katika Swalaah au wanapokuwa na wanaume pale Imaam anaposahau kitu katika Swalaah basi inaruhusiwa atanabahishe kwa kupiga kofi. Ama wanaume anapokosea Imaam, wao wanatakiwa walete tasbiyh kama ilivyotibiti katika Sunnah kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na kwa hayo, inatambulikana kwamba wanaume kupiga makofi ni katika kuigiza makafiri na kuwaiga wanawake; na yote hayo yamekatazwa.

 

 

Na Allaah Ndiye Mwenye kuleta Tawfiyq.

 

 

Kwa faida, Ash-Shawakaan amesema katika ‘Niyl Al-Awtwaar’: (kuhusu kauli ya Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Hakika kupiga makofi ni kwa ajili ya wanawake."

 

Inamaanisha kwamba imekatazwa kwa wanaume kabisa kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayejishabihisha na watu basi yeye ni miongoni mwao)).

 

Na Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika: ‘Al-Iqtidhwaa’ (1/83):

 

Hadiyth hii, inaonyesha na kuthibitisha kuwa, hali ya chini kabisa ni kuharamishwa kushabihiana nao japokuwa dhahiri yake ni hukmu kuwa ni kufru kushabihiana nao kama katika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):  

وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ ۗ

Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao.[Al-Maaidah: 51].

 

Na akasema pia kuhusu Hadiyth hii katika ‘Al-Iqtidhwaa’ (1/81):

 

"Sababu ya kuharamishwa huku ni kushabihiana (kujifananisha) nao."

 

 

Na Fatwa ya ‘Allaamah Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah) chini, inatilia nguvu yaliyotanguliwa kuelezwa:

 

 

Swali:

 

Fadhwilat Shaykh, Allaah Akuhifadhini: Nafanya kazi ya udaktari na nnapohudhuria vikao au makongamano ya udaktari, wanaume husimama kumpigia makofi mtoa mada. Ninapowaambia kwamba hakika kupiga makofi haifai kwenu bali ni kwa wanawake tu, husema: Hukmu hiyo imekusudiwa katika Swalaah pekee. Je, maneno haya ni sahihi?

 

 

Akajibu ‘Allaamah Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah):

 

Hapana! Si sahihi. Wanaume hawatakiwi kupiga makofi katika Swalaah wala kwengineko. Kupiga makofi ni kwa ajili ya wanawake na si kwa wanaume katika Swalaah au kwengineko. Hivyo ni kwa upande mmoja. Ama kwa upande mwengine, ni kwamba kuna kujifananisha na makafiri. Hiyo ni ada ya makafiri hatukuwa tukiijua wala Waislamu hawakuwa wakiijua (wakifanya) au hapakuwepo wanaume kupiga makofi isipokuwa ilipotujia mila na desturi za kikafiri katika sherehe zao na katika mikusanyiko yao. Na kupiga makofi pia ni katika mambo ya kijaahiliyyah: 

 وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ

Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. [Al-Anfaal: 35]

 

 

Wanavyuoni wamesema: ‘Al-Mukaa’ ni Miruzi na ‘At-Taswdiyah’ ni kupiga makofi. Kwa hiyo kupiga makofi ni katika kitendo cha kafiri. Na sasa (siku hizi) Subhaana-Allaah Wanapiga makofi na kupiga miruzi katika sherehe kama kitendo cha jaahiliyyah.” 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share