Muislamu Kufuga Rasta

 

Muislamu Kufuga Rasta

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

 

Asalaam Alaykum,

 

Mimi niliulizwa swali kuwa - Je inaruhusiwa kisharia kwa mwanamke au mwanaume kuwa na rasta ya nyele zake za asili? Sasa kwasababu huwa napata nakala za Alhidaaya nikaona nilipitishe hili swali kwenu kwasababu ninatumaini jibu litakuwa zuri na la uhakika. Waasalaam,

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kuweka rasta ni katika kuwaiga makafiri na si katika mila zetu za Kiislam. Uislamu unachunga nadhafa na usafi na pia mienendo yote kama  tulivyofundishwa na Nabiy wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na yeye ndiye aliyetukataza tusijifananishe au kuwaiga wasiokuwa Waislam.

Kuhusu kujifananisha na makafiri Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((...وَمَنْ تَشَبَّهَ بِقَوْمٍ فَهُوَ مِنْهُمْ))

"Atakayejifananisha na watu, basi yeye ni miongoni mwao". [Abu Daawuud na Ahmad].

 

 

Isitoshe hali hii inakhalifu Fitwrah (Maumbile ya asli ya mwanaadam ambayo ni Uislam).

 

 

Hivyo, kuweka rasta ni jambo lisilo la Kiislam na halifai, na swali la kuwauliza wafanyao hivyo, wanafanya kwa malengo yepi? Kwa mafunzo ya nani? Kwa faida gani? Ikiwa pia kavutiwa kwa kuwaona hao ambao sehemu ya dini yao ni kuvuta bangi, basi hakika atakuwa mtu huyo hajitambui na hajui malengo yake hapa duniani na kwa sababu malengo ya wmanaadam hapa ulimwenguni ni kumuabudu Allaah na hakupatikani hilo isipokuwa mtu kuwa Muislam na kufuata mafunzo yake yote bila kuacha mengine.

 

 

Tunamuomba Allaah Awaongoze Waislam na Awaruzuku mapenzi ya kuipenda dini yao na kuifuata na kuacha kufuata mila na tamaduni zisizo za Kiislam.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share