Muziki Inayowekwa Katika Nashiyd Na Qaswiydah Inafaa? Anavutiwa Nazo Sana

 

Muziki Inayowekwa Katika Nashiyd Na Qaswiydah Inafaa? Anavutiwa Nazo Sana

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Asalam Aleikum.

 

Nimesome makala moja inaeleza kuwa muziki ni haramu. Nauliza hivi ile muziki inayotiwa kwenye kasida pia ni haramu? Kama hi hivyo niache mara moja maana mimi ni mpenzi sana wa kusikiliza kasida zote zinazosomwa hivi hivi na zile zenye muziki na zenye muziki ndiyo zinanivutia zaidi

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Muziki na utumiaji wa ala za muziki ni haramu katika Dini yetu hii, Uislamu. Zifuatazo ni dalili kuhusu hilo:

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kutakuwa watu katika Ummah wangu watakao halalisha uzinzi, uvaaji wa Hariri, pombe (unywaji) na ma’aazif (ala za muziki)" [al-Bukhaariy].

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwisho wa zama (dunia) kutakuwa na maporomoko ya ardhi, mawe kutoka mbinguni na kugeuza kwa wanyama, wakati ambapo ala za muziki na waimbaji wanawake watakapoenea na pombe kuruhusiwa" [atw-Twabaraniy].

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Watu katika ummah wangu watakunywa pombe, kuiita kwa jina jingine. Watatiwa furaha kwa uchezaji wa ala za muziki na uimbaji wa wanawake (watakao waimbia). Allaah Ataifanya ardhi kuwameza wote na kuwageuza kuwa nyani na nguruwe". [Ibn Maajah].

 

 

Na Allaah Aliyetukuka Amesema:

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾

Na miongoni mwa watu, yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) njia ya Allaah bila elimu, na huichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha. [Luqmaan : 6].

 

Ibn Jariyr atw-Twabariy katika Jaami‘ul Bayaan amesema kuwa rai ya mufasirina wa Qur-aan kuhusiana na maana ya ibara “Lahwal Hadiyth (maneno ya upuuzi)” inaweza kugawanywa katika aina tatu. Nazo ni:

 

1.     Uimbaji na kusikiliza nyimbo.

2.     Kuajiri au kununua waimbaji wataalamu, wanaume na wanawake.

3.     Kununua ala za starehe.

 

 

Rai hii ndio iliyokuwa rai ya Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Ibn Mas‘ud, Jaabir bin ‘Abdillaah na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhum) {al-Kanadi Mustafa Abu Bilaal, The Islamic Ruling on Music and Singing in the Light of the Qur’an, Sunnah and the Consensus of the Salaf (Hukumu ya Kiislamu ya Muziki na Nyimbo katika Muono wa Qur-aan, Sunnah na Ijmaa ya Watangu Wema, uk. 9}.

 

 

Na pale Ibn Mas‘ud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipoulizwa kuhusu Aayah hii, alijibu: "Kwa Yule ambaye hakuna Rabb ila Yeye kuwa Aayah hii inamaanisha muziki". Naye aliikariri ibara hiyo mara tatu kuitilia mkazo rai yake hiyo. Na waliokuwa na rai hiyo katika Tabi‘iyn ni ‘Ikrimah, Mujaahid, Makhuul, ‘Umar bin Shu‘ayb na wengineo.

 

Hata hivyo, upo wakati ambao mashairi yanaruhusiwa kuimbwa bila ya kuwepo kwa ala za muziki isipokuwa daff (dufu, twari) tu kwa wanawake. Na hali hizo ni kama:

 

1.   Wakati wa Jihaad na mapambano mengine katika Njia ya Allaah Aliyetukuka. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiimba wakati wa Vita vya Khandaq (Muslim).

 

2.   Wakati wa sherehe za Kiislamu kama ‘Iyd al-Fitwr na ‘Iyd Al-Adhwhaa.

 

3.   Pia ruhusa imetolewa kwa wanawake na wasichana kuimba na kupiga daff (dufu) wakati wa harusi.

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

 

Hukmu Ya Muziki Katika Qur-aan Na Sunnah - Ewe Upendaye Nyimbo Na Muziki, Haujafika Wakati Wa Kuogopa Adhabu Kali Za Allaah?

 

Ngoma, Muziki Haramu

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share