Niendelee Kuswali Jamaa Na Msikiti Unaosomwa Qunuut Kila Siku Au Bora Niswali Pekee Yangu Nyumbani?

SWALI:

 

ASSALAMU ALAYKUM WARAHMATU LLAHI WABARAKATU SUALI LANGU KUHUSU SWALA YA ASUBUHI JE HII DUA YA KUNUTI KWENYE SWALA HII INAKNIPA UGUMU KWA VILE MIMI NINAISHI KWENYE MISIKITI AMBAYO HUWA INALETA KUNUTI NA IKITOKEZEA KUWACHA SIKU MOJA TU HUWA WATU WENGI WANAONA KAMA SWALA YAO HAIKUSIHI SASA MIMI NIFANYEJE NISALI NYUMBANI WAKATI HUO AU NIENDE NIKASALI HIYO KUNUTI HAINA MATATIZO. 

 


 

 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuswali katika Msikiti ambao ndani yake kunasomwa Qunuut.

 

Tufahamu kuwa Swalah ya jama’ah ina fadhila kubwa sana katika Uislamu. Thawabu za kuswali kwa jama’ah ukilinganisha na Swalah ya mtu peke yake ni kupata daraja ya ziada ya mara 23 mpaka 27.

 

 

Na endapo utaswali nyuma ya Imaam anayesoma Qunuut katika Swalah ya Alfajiri, basi unatakiwa umfuate na Swalah yako ni sahihi, kwani kumfuata Imaam ni wajibu, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

"Imam amechaguliwa ili afuatwe" na akasema: "Msitofautiane na Maimam wenu",

na pia katika Swahiyh Al-Bukhaariy amesema:

"Wanawaongoza katika Swalah; ikiwa wamepatia, (ujira) ni wenu na wao, na wakikosea, (ujira) ni wenu na (dhambi) ni zao."

 

Ni kinyume na Sunnah kuisoma Qunuut kwenye Swalah za asubuhi na kudumu nayo kama inavyofanywa kwani hilo halijathibiti katika Hadiyth sahihi kutoka kwa Mtume (Swallah Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam).

Tafadhali soma zaidi kwenye viungo hapa chini ambapo kuna maelezo yanayofanana na swali lako:

Kusoma Du’aa Ya Qunuut Katika Swalah Ya Alfajiri Ni Sunnah?

 

Anamkhalif Imaam Kwa Kusoma Du’aa Ya Qunuut Wakati Imaam Anasujudu

 

Du’aa za Qunut Ziko Ngapi Na Je Lazima Zisomwe Katika Swalah Ya Alfajiri?

 

Kwa hiyo, si vyema kuacha kuswali kwa jama’ah kwa ajili ya Qunuut kwani hiyo haitoathiri Swalah yako hiyo. Imaam Ahmad aliulizwa kuhusu watu wenye kusoma Qunuut huko Basrah (Iraq): “Je, waonaje kuhusu Swalah ya mwenye kuswali nyuma ya anayesoma Qunuut?” Akasema: “Hakika walikuwa Waislamu wakiswali nyuma ya mwenye kusoma Qunuut na nyuma ya wasioleta Qunuut” (Abu Maalik Kamaal as-Sayyid Saalim, Swahiyh Fiqhus Sunnah, mj. 1, uk. 367).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share