Mume Achukue Hatua Gani Ikiwa Mke Hataki Kuswali?

 

SWALI:

 

Asalamu alaikuwarahmatu llah,

 

Nawashukuru sa kwa kuupoteza muda wenu kwa kuyajibu maswali yetu.

 

Suala langu ni kwamba, Endapo umeoa lakini mke wako hataki kusali au anasali kwa siku anazopenda yeye mwenyewe tu. Lakini anaamini kwamba swala ni wajibu kwake. Na unamkumbusha kila swala na anasema "nitasali" lakini hasali. Je, kama ni mume wa kiislam natakiwa nichukue hatua gani ili nisije kuwa mas-ul siku ya kiyama?

 


 

 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke asiyeswali.

 

Mara nyingi kama vile wanawake wanashindwa kufuata maagizo ya kuchagua mume wa sawa Kidini ndivyo wanaume wanavyofanya makosa hayo hayo. Mume wa Kiislamu anatakiwa amchague mke mwenye Dini na Imani, maadili na tabia nzuri. Kukosa kufuata maagizo hayo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio kunatokea matatizo kama hayo.

 

Hata hivyo, kosa lishatokea na inabidi tupate suluhisho kwa suala hilo nyeti. Kulingana na maelezo yako ni kuwa mkeo inaonyesha bado ana Uislamu na Imani, hivyo anataka msukumo wa kuweza kutekeleza wajibu huo bila ya tatizo. Jambo ambalo unatakiwa mwanzo kabisa kufanya ni kumnasihi mkeo kwa njia nzuri, kwani Allaah Aliyetukuka Anatuambia: “Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora” (16: 125).

 

Inatakiwa utumie mbinu tofauti za kuweza kumvutia katika kuswali bila ya yeye kuwa na kinyongo juu ya suala hilo. Mpatie vipeperushi kuhusu umuhimu wa Swalah na madhara ya kuacha, vitabu, kanda, kaseti na njia nyingine.

 

Ikiwa imeshindikana hilo, itabidi sasa uingize mkono wa wazazi wenu kama inavyotaka sheria. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na ambao mnachelea kutoka katika utiifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikutiini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Allaah ndiye Aliye juu na Mkuu. Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari” (: 34 – 35).

 

 

Hivyo inatakiwa ufuate mfumo ufuatao:

 

1.     Kuwanasihi katika ya haki na ukweli.

2.     Mhame katika malazi.

3.     Mpige mkeo kipigo ambacho hakitamuumiza bali cha kumtisha wala usimpige uso.

4.     Kuwe na suluhisho kwa kutumia waamuzi kutoka upande wa mke na mume ili waamue hilo.

 

Ikiwa hakukupatikana suluhisho lolote na wala mkeo hakubadilika basi itabidi umuache. Na ikiwa itatokea hilo itabidi usirudie kosa tena unapotaka kuoa mwingine. Hata hivyo, tunaamini kuwa haitofikia hapo, InshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share